1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Juhudi za kuufumbua mzozo wa Guine

Oumilkher Hamidou6 Oktoba 2009

Upande wa upinzani na jumuia zinazopigania masilahi ya jamii,zinataka utawala wa kijeshi ung'oke madarakani

https://p.dw.com/p/K0BZ
Mpatanishi wa ECOWAS Compaore akipeana mkono na mkuu wa utawala wa kijeshi wa Guine,Dadis CamaraPicha: AP

Rais Blaise Compaore wa Bourkina Fasso anaepatanisha katika mzozo wa Guinea ya Conakry ameshauri kuwakutanisha wawakilishi wa utawala wa kijeshi na upande wa upinzani hivi karibuni mjini Ouagadougou,baada ya maandamano ya umma kuvunjwa nguvu kikatili kabisa na vikosi vya usalama September 28 iliyopita.

Rais Blaise Compaore alifika ziarani mjini Conakry,akiwa na jukumu "la kurahisisha mambo" katika mzozo wa Guinee-juklumu alilotwikwa na jumuia ya ushirikiano wa kiuchumi ya mataifa ya Afrika magharibi ECOWAS.

"Lazma watu waketi pamoja,wajadili matatizo yaliyoko ana kwa ana."Na hili ndilo nililopendekeza mbele ya viongozi wa baraza la taifa la demokrasia na maendeleo-CNDD-na makundi yote ya kisiasa ya upande wa upinzani."Amesema rais Compaore wakati wa mkutano pamoja na waandishi wa habari mwishoni mwa ziara yake mjini Conakry.

Kiongozi wa utawala wa kijeshi ulionyakua madaraka tangu miezi tisaa iliyopita,kepteni Moussa Dadis Camara,hajashiriki katika mkutano huo pamoja na waandishi habari.Lakini mshauri wake maalum,Idrissa Cheriff amehakikisha watakwenda Ougadougou,japo kama tarehe bado haijapangwa.

Wanajeshi wang'oke madarakani

Upande wa upinzani umesema utahudhuria mkutano wa Ougadougou.Waziri mkuu wa zamani Sydia Touré amesema tunanukuu "tutakwenda bila ya shaka na haraka iwezekanavyo Ougadougou."Mwisho wa kumnukuu.

Wawakilishi wa vyama vya upinzani,vyama vya wafanyakazi,na mashirika ya huduma za jamii wamemkabidhi mpatanishi huyo wa jumuia ya ECOWAS orodha ya madai yao.

Wanataka utawala wa kijeshi wa CNDD ung'oke madarakani na kuundwa serikali ya kiraia kusimamia kipindi cha mpito hadi uchaguzi mkuu utakapoitishwa january mwakani.

Ziara ya rais Blaise Compaore imefanyika wiki moja baada ya vikosi vya usalama,kuvunja nguvu kongamano la upande wa upinzani katika uwanja wa michezo wa mjini Conakry September 28 iliyopita .Watu wasiopungua 150 waliuwawa.

Mpatanishi huyo wa jumuia ya ushirikiano wa kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi ECOWAS amesema amemkabidhi mapendekezo kadhaa kiongozi wa utawala wa kijeshi Moussa Dadis Camara.Hata hivyo rais Compaore ameendelea kusema:

"Uwezo wangu wa kusimamia ujumbe kama huu wa kurahisisha mambo,si rahisi kuutathmini.Itabidi watu wasubiri matokeo ya mwisho ili kukadiria hatima ya juhudi zetu."

Mwenyekiti wa kongamano la Afrika kwaajili ya kuhifadhi haki za binaadam,Alioune Tine amesema tunanukuu" jukumu la Compaore halina nafasi ya kufanikiwa.Ingekua bora wahusika wa visa vya umwagaji damu vya september 28 wangematwa badala ya kujaribu kupatanisha."Mwisho wa kumnukuu Alioune Tine.

Umoja wa ulaya unaojiandaa kuwawekea vikwazo viongozi wa kijeshi wa Guinee,umeahidi hii leo kuwasiliana moja kwa moja pamoja na mpatanishi wa jumuia ya ECOWAS,Blaise Compaore,Umoja wa Afrika na Umoja wa mataifa ili kusaka ufumbuzi wa amani na wa kudumu wa mzozo wa Guinea.

Mwandishi:Oummilkheir Hamidou /afp/rtr/

Mhariri:M.Abdul-Rahman