1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Juhudi za kupiga vita UKIMWI zapata moyo

22 Julai 2014

Juhudi ngumu za kutafuta tiba ya kirusi cha HIV zimeonekana kuimarika katika mkutano wa UKIMWI wakati wanasayansi wakisema kwamba wamekilazimihsa kirusi hicho kutoka kwenye maficho yake baada ya kushambuliwa na madawa.

https://p.dw.com/p/1CgaX
Mkutano wa Kimataifa wa 20 wa UKIMWI Melbourne, Australia.
Mkutano wa Kimataifa wa 20 wa UKIMWI Melbourne, Australia.Picha: Reuters

Majaribio ya tiba hiyo yaliyofanywa kwa waathirika sita wenye virusi vya HIV waliojitolea ni hatua muhimu katika kile kinachojulikana kama mkakati wa tiba wa "kukitimua na kukiua " kirusi hicho.

Mbinu hiyo inakusudia kukilazimisha kirusi hicho cha HIV chenye kudhoofisha uwezo wa mwili kujikinga na maradhi kutoka ngome yake ya mwisho baada ya kushambuliwa na madawa ya kupunguza makali ya UKIMWI.

Madawa haya mapya yanaweza kukiweka kirusi cha HIV katika damu kwa kiwango cha chini cha kuweza kugundulika na kuwawezesha wagonjwa wenye kuuguwa kurudi kimiujiza katika hali ya maisha ya kawaida.Lakini madawa hayo inabidi yatumiwe kila siku, yana gharama kubwa na yana madhara ya pembeni.

Mradi wa majaribio

Iwapo madawa hayo yanasitishwa kutumiwa kwa kawada virusi vya HIV hurudi tena kwenye kipindi cha wiki chache na kuanza tena kuziambukiza seli nyengine za kujikinga na maradhi .Kwa hiyo wanasayansi kwa miaka mitatu iliopita wamekuwa wakielekeza mkakati wao katika kukitowa kirusi hicho cha HV kwenye ngome yake na baadae kuziua seli zake zinazojificha.

Wajumbe katika Mkutano wa Kimataifa wa 20 wa UKIMWI Melbourne, Australia.
Wajumbe katika Mkutano wa Kimataifa wa 20 wa UKIMWI Melbourne, Australia.Picha: Reuters

Katika mhadhara waliouwasilisha Jumanne (22.07.2014) katika mkutano wa kimataifa wa UKIMWI huko Melbourne watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Arhus nchini Denmark wameielezea hatua hiyo kuwa ni kubwa katika mchakato wake wa kwanza.

Wagonjwa sita ambao walikuwa wakitumia madawa ya kupambana na makali ya ugonjwa wa UKIMWI walitumia madawa ya kupambana na saratani yanayoitwa romidepsin ambayo yalisababisha uzalishaji wa seli zilizoambukizwa na kirusi cha HIV kuongezeka kiwango kati ya kipimo cha 2.1 na 3.9 juu ya kiwango cha kawaida.

Kwa wagonjwa watano kiwango cha virusi vya HIV kilioko kwenye damu kiliongezeka kufikia kiwango cha kuweza kupimika hatua inayoonekana kuwa muhimu.

Hatua muhimu

Mradi huo wa majaribio ulikuwa ukitaka kujuwa iwapo inawezekana kukichomowa kirusi hicho kinachojibanza na kukifanya kiweze kuonekana.

Nembo ya UKIMWI ya Utepe Mwekundu.
Nembo ya UKIMWI ya Utepe Mwekundu.

Mtafiti mkuu wa mradi huo Ole Schmeltz Sogaard amesema hii ni hatua kwenye mwelekeo sahihi lakini bado safari ni refu na kuna vikwazo vingi vya kukiukwa kabla ya kuanza kuzungumzia juu ya tiba dhidi ya UKIMWI.

Shirika la Kimataifa la Madaktari Wasiokuwa na Mipaka limesema madawa ya kupambana na UKIMWI bado ni ya ghali ya mno kwa wagonjwa wengi hususan wale wanaoishi katika nchi zilizoendelea.

Shirika hilo limesema wahanga wa ugonjwa huo katika nchi za kimaskini hawaathiriki sana na gharama kubwa za madawa hayo na hutumia kama euro 100 tu kwa mwaka kwa madawa ya kupambana na ugonjwa huo lakini kampuni za madawa zinawatoza gharama kubwa wagonjwa walioko kwenye nchi zilizoendelea.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP/DW

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman