1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Juhudi za kupambana na ogezeko la ujoto duniani

P.Martin25 Septemba 2007

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,Ban Ki-Moon alipofungua mkutano wa kilele ulioitishwa kujadili tatizo la ongezeko la ujoto duniani, alizilaumu nchi zilizoendelea kiviwanda kuwa hazikuchukua hatua za dhati kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa duniani.

https://p.dw.com/p/CB11
Ban Ki Moon
Ban Ki MoonPicha: AP

Ban Ki-Moon akiamini kuwa mabadiliko ya hali ya hewa ni kitisho kikubwa kwa maendeleo,amewakutanisha viongozi wa kimataifa kujadili njia za kupambana na tatizo la ongezeka la ujoto duniani.Amesema,haiwezekani tena kukubali vile viwango vya gesi zinazochafua mazingira kutoka viwanda vya nchi zilizoendelea.

Katibu Mkuu Ban alipozikosoa nchi za viwanda, hakuitaja Marekani kwa jina,lakini aliashiria msimamo wa kujitenga unaochukuliwa na serikali ya Washington kuhusu suala la mazingira.Rais George W.Bush hakuhudhuria mkutano wa viongozi mjini New York,licha ya kujulikana kuwa nchi yake ni mzalishaji mkubwa kabisa wa gesi zinazochafua mazingira duniani.

Baadhi kubwa ya nchi zinazoendelea,zinaamini kuna umuhimu wa kuwepo mfumo wa kimataifa utakaohakikisha ushirikiano wa hali ya juu,kati ya nchi zote,ili tatizo la mabadiliko ya hali ya hewa liweze kukabiliwa kwa mafanikio.

Wakati huo huo Kansela wa Ujerumani,Angela Merkel anaeongoza juhudi za kimataifa,kuhifadhi mazingira,alipozungumza mjini New York,alitoa mwito wa kuchukuliwa hatua imara kupambana na tatizo hilo.

Kwa upande mwingine makundi ya jamii za kiraia yanasema,nchi tajiri zenye viwanda zinapaswa kuitikia mwito wa Katibu Mkuu Ban,ili suluhisho la haraka liweze kupatikana kuhusu mazingira yetu.Wajumbe wa makundi hayo wamekumbusha kuwa mabadiliko ya hali ya hewa huwaathiri zaidi watu masikini wasiohusika na uchafuzi wa mazingira.

Mkutano wa Umoja wa Mataifa uliokusanya wajumbe kutoka nchi 150 ni hatua muhimu kuelekea Bali,Indonesia ambako kutafanywa majadiliano yenye azma ya kurefusha Itifaki ya Kyoto,ambao ni mwongozo wa njia za kuhifadhi mazingira na kupambana na ogezeko la ujoto duniani.