1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Juhudi za kidiplomasia katika mgogoro wa Kaukasus

M.Soric/(P.Martin)12 Agosti 2008

Juhudi za kimataifa kufumbua mzozo wa Kaukasus kati ya Urusi na Georgia zimeshika kasi.Lakini katika ufumbuzi huo,ni Ulaya na sio Marekani inayohitajiwa.

https://p.dw.com/p/EvVr
Majeshi ya Urusi,Ossetia ya KusiniPicha: AP

Nchi yenye mchanganyiko wa makabila na inayojikuta kijiografia na kisiasa katika hali kama ile ya Georgia,inahitaji hadhari na uangalifu.Hayo alielewa vizuri Eduard Schewardnadse aliekuwa rais wa Georgia mwanzoni mwa miaka ya tisini.Lakini mrithi wake,Michail Saakaschvilli hana yote mawili.Mbaya zaidi ni kuwa Rais Saakaschvili amechagua kupigana na jirani mwenye nguvu kubwa;alipoona Urusi imejibu kwa kupeleka vifaru na majeshi yake,aliomba kusaidiwa na nchi za kigeni.

Ulimwengu mzima unauliza ni kitu gani kilichomfanya Saaakaschvili kuufufua mgogoro huo?Huenda ikawa ametaka kuilazimisha Marekani kuingia katika mzozo huo na Urusi.Kwani tangu miaka mingi,Georgia inapatiwa silaha na Marekani na vile vile ushauri wa kijeshi kutoka mamia ya maafisa wa Kimarekani waliokuwepo huko huko Georgia.

Au,Saakaschvilli alitumaini kuwa Marekani kwa njia moja au nyingine, ingetumbukizwa katika mzozo huo na hivyo Moscow ingerudi nyuma,ili kuzuia mapambano ya moja kwa moja na Washington.Ikiwa hayo ni mambo yaliyomchochea Rais wa Georgia kutuma majeshi yake katika jimbo la Ossetia ya Kusini lililojitenga na linaloungwa mkono na Urusi,basi safari hii amekwenda kombo.

Vile vile amesababisha umwagaji damu wa kikatili katika eneohilo la Kaukasus.Maelfu ya watu wamepoteza maisha yao.Maelfu wengine wameondoka makwao kukimbia mapigano.Siku moja Rais Saakaschvili hatokuwa na budi ila kuwajibika kwa maafa hayo.

Kwa upande mwingine,Urusi itatumia fursa hii kuuonyesha ulimwengu mzima faida ya kusaidiwa na Marekani- msaada huo hauna manufaa -hivyo ndivyo angalau Moscow inavyoona.Kinyume na Saakaschvili aliechukua maamuzi ya haraka,Rais wa Marekani George Bush anatumia busara kutojitumbukiza vitani na dola lenye nguvu za nyuklia Urusi,kwa sababu ya mgogoro wa kimkoa.Kwani Ikulu ya Washington inaelewa vyema kuwa vita hivyo vikiendelea kwa muda mrefu,basi hatimae bei za mafuta na gesi zitaongezeka katika masoko ya dunia.

Tukio kama hilo litaathiri vibaya mno uchumi wa Marekani,lakini Urusi kama mzalishaji mkubwa wa gesi na mafuta,itanufaika kwa kuingiza mabilioni ya fedha.Kijeshi,Georgia imeshashindwa vita hivi.Itaweza kujitoa kimaso maso kwa msaada wa kidiplomasia,ikiwa baada ya mapigano kusitishwa,Urusi haitoweka vikosi vyake kwenye mipaka ya Ossetia ya Kusini na Abkhazia.