1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Juhudi za amani za Misri

Hamidou, Oumilkher21 Oktoba 2008

Serikali ya Cairo inajaribu kuwapatanisha wapalastina

https://p.dw.com/p/Fe0l
Kiongozi wa utawala wa ndani wa Palastina Mahmoud AbbasPicha: AP


Misri imependekeza mpango wa pointi nne ili kujaribu kuufumbua mzozo unaowatenganisha wapalastina,kati ya wale wanaoelemea upande wa Hamas na wenzao wanaomuunga mkono kiongozi wa utawala wa ndani Mahmoud Abbas.



Serikali ya mjini Cairo iliyojitolea kuwa mpatanishi katika ugonvi huu,imeshauri katika pendekezo hilo ambalo nakala yake imelifikia shirika la habari la Uengereza Reuters,paundwe ya umoja wa taifa na kufanyiwa marekebisho vikosi vya usalama vya Palastina.


Misri inaamini pia kwamba kiongozi wa utawala wa ndani Mahmoud Abbas anastahiki kuendeleza mazungumzo ya amani pamoja na Israel,lakini mswaada wowote wa makubaliano unabidi upate ridhaa ya Hamas na makundi yote mengine ya wapalastina.


Mnamo wiki za hivi karibuni wapatanishi wa Misri walikutana na wawakilishi wa makundi yote ya wapalastina,kabla ya kuratibu mpango  huo wa amani utakaokabidhiwa pia pande zote zinazohasimiana, mkutano wa kilele utakapoitishwa November tisaa ijayo mjini Cairo.



Misri inashauri paundwe serikali ya umoja wa taifa na yafikiwe makubaliano kuhusu tarehe ya kuitishwa chaguzi mpya.


Fatah wanapendelea kuona chaguzi za bunge na rais zinaitishwa kwa pamoja mnamo mwaka 2010.Hamas lakini wamekumbusha kwamba mhula wa Mahmoud Abbas  kama kiongozi wa utawala wa ndani unamalizika kimsingi  mwezi January mwakani.Misri inaunga mkono chaguzi zote mbili ziitishwe kwa wakati mmoja.


Serikali ya mjini Cairo inahisi pia vikosi vya usalama vya Hamas na vile vya Fatah ambavyo vimeshawahi  mara kadhaa kushambuliana,visijihusishe na makundi ya kisiasa na badala yake viungane na kua vikosi vya taifa.


Zaidi ya hayo mpango wa amani wa Misri unashauri makubaliano yoyote ya amani pamoja na Israel yapigiwe kura ya maoni na wananchi au yafikishwe katika halmashauri ya ukombozi wa Palastina itakayoyaleta pamoja makundi ya Hamas,Fatah na makundi mengineyo ya wapalastina.


Msemaji wa Hamas,Sami Abou Zouhri,amesema bila ya kutoa maelezo zaidi kwamba Hamas wataukubali mpango wa amani wa Misri,baada ya kufanyiwa marekebisho na baadhi ya mambo kufafanuliwa.


Fatah pia wanasema wako tayari kuukubali mpango wa Misri ikiwa mambo mawili yataingizwa.Nayo ni kuhakikisha kwamba serikali yoyote ya mpito itayatambua makubaliano yaliyofikiwa hapo awali na chama cha ukombozi wa Palastina PLO na kwamba Mahmoud Abbas na PLO wanaendelea kua wadhamini pekee wa mazungumzo ya amani pamoja na Israel.