1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroSudan

Mazungumzo ya suluhu ya amani Sudan kuanza tena

27 Machi 2024

Marekani imesema inayo matumaini ya kufufuliwa kwa mazungumzo ya kujaribu kumaliza vita baina ya pande hasimu nchini Sudan katikati mwa mwezi unaokuja baada ya kumalizika kwa mwezi mtukufu wa Ramadhan.

https://p.dw.com/p/4eCDa
Sudan 2019 | Angehörige der Rapid Support Forces
Picha: Hussein Malla/AP Photo/picture alliance

Matumaini ya kufufuliwa kwa mazungumzo hayo ya kusaka amani kati ya pande zinazopigana vita nchini Sudan, yametangazwa na Mjumbe Maalum wa Marekani kwa ajili ya taifa hilo la kaskazini mashariki mwa Afrika, Tom Perriello.

Mjumbe huyo alikuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini Washington, Marekani baada ya kufanya ziara ndefu ya kuyatembelea mataifa 7 ikiwemo Sudan kutafuta njia ya kuanzisha duru mpya ya majadiliano ya kukomesha mapigano.

Perriello ambaye aliteuliwa wiki za karibuni kuchukua wadhifa huo wa mjumbe maalum, amesema ishara zote zinaonesha kwamba hakuna upande utakaoibuka mshindi kwenye vita vinavyoendelea na kwa hivyo busara inafaa kuwaongoza wale wanaopigana kukutana mbele ya meza ya usuluhishi.

Amesema vita hivyo vya karibu miezi 12 vimeleta madhila makubwa kwa umma wa Sudan pamoja kanda nzima na sasa vimegeuka kuwa uhasama kwa misingi ya rangi na maeneo.

Soma pia: Jeshi la Sudan lafuta uwezekano wa kusitishwa mapigano

Vita vya Sudan vinahusisha pande mbili hasimu ambazo ni jeshi la taifa linaloongozwa na Mkuu wa Majeshi na kiongozi wa Baraza Tawala Abdul-Fattah al-Burhan dhidi ya aliyewahi kuwa naibu wake anayeongoza kikosi cha mgambo walioasi cha RSF Mohammed Hamdan Dagalo.

Sudan | Mohamed Hamdan Daglo
Kiongozi wa kikosi cha wanamgambo wa RSF Jeneral Mohamed Hamdan Daglo alionyesha utayari wa kusitisha mapigano angalau wakati wa Ramadhan, ingawa jeshi lilikataaPicha: Ashraf Shazly/AFP

Kwa mujibu wa Perriello uwezekano wa pande hizo hasimu kukutana umewekwa kuanzia Aprili 18 baada ya kumalizika kwa mwezi wa Ramadhan na pia kutokana na ratiba ya mkutano wa hisani wa kuchangisha fedha za kuwasaiida waathiriwa wa vita uliopangwa kufanyika Aprili 15, mjini Paris, Ufaransa.

Soma pia:Watu milioni 5 wako hatarini kufikwa na njaa, Sudan

Amesisitiza dhamiri ya serikali mjini Washington ya kuifanya duru hiyo mpya ya mazungumzo kuwa jumuishi. Mwanadiplomasia huyo amesema Marekani ingependelea kuona pamoja na pande mbili hasimu, meza ya mazungumzo iwajumuishe washirika na waitifaki wengine walio na usemi kwenye mzozo huo hususani mataifa ya Misri, Umoja wa Falme za Kiarabu, Jumuiya ya kikanda ya IGAD na Umoja wa Afrika.

Juhudi hizo za upatanishi bado zitaongozwa na Saudi Arabia kwa kushirikiana na Marekani kama ilivyofanyika mwaka uliopita bila mafanikio. Ingawa haijafahamika iwapo mji wa mwambao wa Jeddah utasalia kuwa eneo la makutano.

Soma Pia:Umoja wa Mataifa waomba Wasudan wasisahauliwe

Hata hivyo upo wasiwasi kuwa matamanio hayo ya Marekani huenda hayatatimia kutokana na msimamo wa jeshi la Sudan ambalo limeapa kwamba kamwe hakutakuwa na mazungumzo mengine au usitishaji mapigano kati yake na RSF hadi kundi hilo litakaposambaratishwa.

Nchini Sudan kwenyewe mapigano bado yamepamba moto. Jeshi limewataka raia kuondoka kwenye maeno yanayodhibitiwa na kundi la RSF likisema linaweza kuyalenga kwa kutumia ndege za kivita. Mwito huo unafuatia lawama iliyoliangua jeshi hivi karibuni baada ya kutuhumiwa kuwaua raia wanane kwenye mashambulizi iliyoyafanya kaskazini mwa jimbo la Darfur.