Jopo la uchunguzi dhidi ya Israel latangazwa. | Matukio ya Kisiasa | DW | 03.08.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Jopo la uchunguzi dhidi ya Israel latangazwa.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ametangaza jopo la watu wanne kuchunguza shambulio la mauaji lililofanywa na Israel dhidi ya meli ya misaada iliyokuwa ikielekea Gaza.

Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-moon.

Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-moon.

Shambulio ambalo lilifanywa mwezi Mei mwaka huu na kusababisha vifo vya wanaharakati tisa wa Kituruki.

Katibu Mkuu ametangaza jopo hilo la uchunguzi, baada ya Israel kukubali kuunga mkono uchunguzi huo.

Jopo hilo la watu wanne lililotangazwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa litakuwa chini ya Uenyekiti wa Waziri Mkuu wa zamani wa New Zeland Geoffrey Palmer na Rais wa Colombia anayemaliza muda wake Alvaro Uribe ameteuliwa kuwa Makamu mwenyekiti.

Jopo hilo pia linamjumuisha Muisrael mmoja na Mturuki na kwamba litaanza kufanya kazi Agusti 10 na kuwasilisha ripoti yake ya kwanza katikati ya mwezi Septemba mwaka huu.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, BanKi Moon, ambaye alikutana katika dakika za mwisho kwa mashauriano na viongozi wa Israel na Uturuki, mwishoni mwa wiki iliyopita, amesema jopo hilo litampatia pendekezo kwa ajili ya kuzuia kutokea tena kwa matukio kama hayo.

Aidha amewashukuru viongozi wa Israel na Uturuki kwa kukubali kutoa ushirikiano, ambapo ameelezea kuwa kama ni maendeleo yasiyotarajiwa.

Amesema makubaliano hayo pia yataleta hali nzuri katika uhusiano wa Israel na Uturuki na pia hali jumla katika eneo la Mashariki ya kati.

Uamuzi wa Israel kuunga mkono jopo hilo haukutarajiwa kutokana na kwamba wiki kadhaa ilikuwa ikisisitizia haitashiriki katika uchunguzi wowote wa kimataifa na badala yake kuanzisha chunguzi mbili za ndani.

Akizungumzia jopo hilo, Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema kwa hakika hilo ni jopo lililo na mizani sawa na kwamba Israel haina cha kuficha.

Kwa upande wa Uturuki na Marekani kwa pamoja wamepongeza uchunguzi huo wa Umoja wa Mataifa.

Waziri wa Mambo ya nchi za nje wa Uturuki Ahmet Davutoglu amesema ni mara ya kwanza Israel kukubali uchunguzi wa kimataifa, hali ambayo inaonesha kuwa nchi zote zinawajibika katika sheria za kimataifa.

Naye balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Susan Rice ameelezea matumaini yake kwamba jopo hilo litakuwa chombo kitakachoiwezesha Israel na Uturuki kuondokana na mivutano ya kidiplomasia iliyopo hivi sasa na kuimarisha uhusiano wao thabiti wa kihistoria. Ameongeza kuwa Marekani ina matumaini jopo hilo litafanya kazi kwa uwazi na uaminifu.

Katika hatua nyingine Msemaji wa Umoja wa mataifa Martin Nesirky amesisitizia kuwa uchunguzi huo hautakuwa wa kihalifu na kwamba katibu mkuu wa umoja huo katika siku chache zijazo atatangaza majina ya Muisrael na Mturuki watakaokuwa katika jopo hilo.

Mwezi uliopita Baraza la haki za binadamu la UImoja wa Mataifa lenye makao yake mjini Geneva, Uswisi lilitangaza jopo lake la wataalamu kuchunguza kama shambulio la Israel katika meli hiyo ya misaada lilivunja sheria za kimataifa.

Lakini Israel illikataa kushiriki katika uchunguzi huo kwa sababu, kwa mtazamo wake baraza hilo linapendelea.

Mwandishi: Halima Nyanza(afp)

Mhariri: Josephat Charo

 • Tarehe 03.08.2010
 • Mwandishi Halima Nyanza
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Oadm
 • Tarehe 03.08.2010
 • Mwandishi Halima Nyanza
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Oadm
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com