John Juma | Media Center | DW | 23.01.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Media Center

John Juma

John Juma ni mwanahabari kutoka Kenya, ni mtangazaji wa televisheni na redio na pia mwandishi wa habari za mitandaoni, akiwa na uzoefu wa miaka minane kwenye tasnia hii.

 

Baada ya kufanya kazi nchini kwake, sasa John Juma amejiunga na Idhaa ya Kimataifa ya Kiswahili ya Deutsche Welle (DW-Kiswahili) mjini Bonn, Ujerumani, ambako amekuwa muandaaji na mtangazaji wa vipindi kadhaa, vikiwemo vya habari, makala na uchambuzi.

Deutsche Welle ni shirika la habari la kimataifa lenye makao yake makuu nchini Ujerumani. Lina vituo vya televisheni kwa lugha za Kiingereza, Kijerumani, Kihispania na Kiarabu na pia idhaa za radio zinazotangaza kwa lugha 30 kote duniani na kupitia mitandao. Matangazo ya DW huangazia yote, yakiwemo makala na habari za siasa, sanaa na utamaduni, michezo, sayansi, biashara na mengine mengi.

DW imekuwa chanzo cha kuaminika cha taarifa na habari zisizoegemea upande wowote, ikiwapa watu barani Afrika uchambuzi wa kina na makini juu ya masuala yanayowahusu kwa kiasi kikubwa. DW huwafikia watu milioni 135 kila wiki ulimwenguni kote.

Zaidi kuhusu DW-Kiswahili

Idhaa ya Kiswahili ya DW ambayo ilianzishwa zaidi ya miaka 50, hutangaza kwa masaa matatu kila siku. Wasikilizaji wakubwa wa Idhaa hii wako Afrika Mashariki na mataifa ya ukanda wa Maziwa Makuu. DW Kiswahili huwaandalia wasikilizaji wake ripoti, uchambuzi na vidio kwenye tovuti yake na mitandao yake mingine ya kijamii. Nchini Tanzania, Idhaa hii inafikia 40% ya watu nchini humo, na 30% ya maeneo ya mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. DW Kiswahili imetuzwa mara kwa mara kutokana na utangazaji wake kwa kutumia Kiswahili Sanifu zaidi miongoni mwa idhaa nyinginezo za kimataifa.

John Juma alijiunga na DW-Kiswahili mwezi Februari mwaka 2016 kwa mafunzo ya kazi kwa vitendo, kisha akaajiriwa rasmi mwezi Oktoba mwaka 2016 kama msomaji habari, ripota, mtayarishaji wa vipindi vya redio na video za habari za mtandao ziitwazo "Papo kwa Papo", majukumu anayoendelea nayo hadi sasa. Kadhalika anaongoza matangazo na kufanya mahojiano kwa ajili ya habari na uchambuzi.

Tuzo

Kabla ya kujiunga na DW-Kiswahili, John Juma alifanya kazi na shirika binafsi la habari Standard Group ambapo alikuwa ripota katika televisheni ya KTN (Kenya Television Network) kuanzia mwaka 2008 hadi 2016, na pia msomaji habari na mtayarishaji vipindi katika Radio Maisha.

Juma amepokea tuzo kadhaa kutoka kwa Baraza la Habari Kenya (Media Council of Kenya). Mfano:

2014 - Mwandishi bora wa runinga katika habari zinazohusu masuala ya Sanaa na Utamaduni

2015 - Mwandishi bora wa runinga katika habari zinazohusu masuala ya Sanaa na Utamaduni

2016 - Mwandishi bora wa runinga katika habari zinazohusu Teknolojia, Habari na Mawasiliano

John Juma ana shahada ya kwanza ya Sayansi ya Mawasiliano na Uhusiano Mwema kutoka Chuo Kikuu cha Moi nchini Kenya mwaka 2015. Aidha ana stashahada ya Utangazaji Habari na Uandalizi wa Vipindi vya Runinga kutoka Taasisi ya Masomo ya Habari ya Kenya (Kenya Institute of Mass Communication) aliyotunukiwa mwaka 2008.