Jimbo la Abyei kujiunga Sudan au Sudan Kusini? | Matukio ya Afrika | DW | 31.10.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Jimbo la Abyei kujiunga Sudan au Sudan Kusini?

Wananchi wa Sudan na Sudan Kusini wamepiga kura ya maoni kutaka Jimbo la Abyei lililopo mpakani mwa nchi hizo mbili kujiunga na moja ya Nchi hizo, Jimbo hilo limeharibiwa kufuatia vita vya wenyewe kwa wenyewe.

default

Jimbo hilo lenye ukubwa wa Kilomita 10,000 za mraba na lenye utajiri wa mafuta na ardhi yenye rutuba, hivi sasa linagombaniwa na nchi zote mbili ambazo zote zinadai kuwa eneo hilo linapaswa kuwa upande wake.

Hivi sasa, waliokuwa wakazi wa Jimbo hilo wanafanya juhudi za kulijenga upya, huku zoezi la kupiga kura ikiwa jimbo hilo litajiunga na Sudan Kusini au Sudan likiwa limekamilika Jumanne wiki hii.

Pamoja na mkataba wa amani wa mwaka 2005, uliofanikisha kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe na kuipa uhuru Sudan Kusini, lakini mgogoro katika Jimbo la Abyei haujapatiwa ufumbuzi.

Vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan, vilisababisha wakazi wengi kuyakimbia maeneo yao, wengi kutoka Jimbo la Abyei ambapo mmoja wa waliokimbia, Chris Bak na familia yake wameamua kurejea.

Familia hiyo ilikimbilia katika eneo la mji wa Aweli, uliopo saa chache magharibi mwa mji wa Abyei.

Wakazi warejea Jimboni Abyei

Bak na familia yake sasa, wameamua kurejea lakini baada ya kurejea Jimboni Abyei wiki mbili zilizopita, wakati zoezi la upigaji kura ikiwa jimbo hilo litabaki Sudan Kusini au Sudan lilipokuwa likiendelea, aligundua mabadiliko makubwa, ikiwemo kuchafuliwa vibaya kwa jimbo hilo, alikokufananisha na jangwa.

Bak, ameliambia Shirika la habari la IPS kuwa wamekuwa wakizunguka huku na huko bila kulitambua eneo hilo alikozaliwa.

Hata hivyo anasema, alirejea kijiji mwake akiwa na matumaini mapya, lakini aliporudi kwenye darasa alilokuwa akisoma lilikuwa likivuja kutokana na kutoezekwa na alikuwa akilala katika chumba na rafiki yake aliyekuwa akiugua ugonjwa wa malaria na alijaribu kumtafutia daktari kwa siku tatu mfululizo bila mafanikio.

Konflik Sudan Südsudan

Vita vya wenyewe kwa wenyenye nchini Sudan vimesababisha hasara kubwa.

Jimbo hilo bado linakabiliwa na matatizo mengi, yakiwemo ya ukosefu wa elimu na huduma nyingine muhimu na ndiyo maana wananchi wanataka lijengwe upya.

Suda yagoma kusaini mkataba

Hata hivyo Sudan imegoma kusaini mkataba kuhusu kutoa kura za maoni, kwa madai kuwa zoezi hilo halikuihusisha jamii ya Misseriya inayoipinga nchi hiyo, ambayo mara nyingi huingia Jimboni humo kwa shughuli za ufugaji.

Kutokana na tofauti ilizoonyeshwa na serikali ya Sudan, mjini Khartoum, kutaka kupinga zoezi la upigaji wa kura za maoni, Umoja wa Afrika ulishindwa kufanya maandalizi ya kufanyika kwa kura ya maoni wala kuwasilisha maombi mapya.

Lakini, kauli ya Umoja wa Afrika haikukwamisha mipango ya makabila mbalimbali ya nchi hizo mbili kuendelea na zoezi hilo, ambapo jamii ya watu wa Dinka Ngok waliendelea na mchakato wa kupiga kura hizo.

Pia shirikisho la viongozi wa makabila lililojiita kamati kuu ya kupiga kura ya maoni ya Jimbo la Abyei, nao mwezi uliopita walianza kuwakusanya watu kupiga kura za maoni, ambao wanadai kupata idadi ya watu 100,000 wanaotaka kurejea katika Jimbo hilo, ingawa ni vigumu kuhakikisha ikiwa idadi hiyo ni ya kweli.

Wanatarajia kutoa matokeo ramsi mwezi ujao, ingawa wanaonekana wazi wamelipigia kura jimbo hilo kujiunga na Sudan Kusini.

Kwa mujibu wa msemaji wa serikali ya Sudan Kusini, Michael Makuei Lueth, raia ndiyo watakaoamua ikiwa Jimbo hilo lijiunge na Sudan Kusini au Sudan, kwa kuwa wameahidi kupiga kura bila kuzishirikisha serikali hizo mbili.

Umoja wa Afrika kutotambua matokeo ya kura

Hata hivyo, Profesa Alfred Lokuji katika chuo kikuu cha Juba anayeshughulikia masuala ya amani na maendeleo vijijini, ameliambia shirika la habari la IPS kuwa kura hizo za maoni hazitasaidia chochote kutokana na Umoja wa Afrika na uongozi wa Sudan Kusini kusema wazi kuwa hawatayatambua matokeo hayo.

Omar Hassan al-Bashir Präsident Sudan Besuch in Libyen

Rais wa Sudan Kusini, Omar Hassan al-Bashir

Rais wa Sudan Kusini, Omar Hassan al-Bashir alifanya mazungumzo na Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini wiki iliyopita mjini Juba, na kukubaliana kuungana pamoja katika kushughulikia mgogoro wa Jimbo la Abyei, ingawa hawakupanga muda kamili na ni lini wataanza utekelezaji.

Vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan vilizuka mwaka 2008, kati ya vikundi vya waasi na jeshi la serikali, na kusababisha mauaji ya raia, ambapo shirika la haki za binaadamu linakadiria kuwa watu 60,000 waliyakimbia mapigano hayo.

Mapigano hayo yaliripuka tena mwaka 2011, wiki chache tu kabla Sudan Kusini haijatangazwa rasmi kujitoa kutoka Sudan na kuwa nchi mpya Duniani, na kuliacha Jimbo la Abyei bila mwelekeo.

Mwandishi: Flora Nzema/IPS

Mhariri: Josephat Nyiro Charo