Jeshi, waandamanaji Sudan wakubaliana kugawana madaraka | Matukio ya Afrika | DW | 05.07.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Jeshi, waandamanaji Sudan wakubaliana kugawana madaraka

Wapatanishi wa Umoja wa Afrika wamesema majenerali wa kijeshi nchini Sundan wamefikia makubaliano na viongozi wa maandamano juu ya kugawana madaraka, katika mafanikio yaliofuatia wiki kadhaa za mkwamo wa kisiasa.

Makubaliano hayo ya kihitosria yamekuja baada ya siku mbili za mazungumzo, kufuatia kuvunjika kwa duru ya mwisho ya majadiliano mwezi Mei kuhusiana na nani anapaswa kuongoza chombo kipya cha utawala kati ya raia na jeshi.

"Pande mbili zimakubaliana kuunda baraza huru lenye uwakilishi sawa kati yao, jeshi na raia, kwa muda wa miaka mitatu au zaidi na pia wamekubaliana juu ya serikali huru ya kiraia, inayoongozwa na waziri mkuu msomi, ambayo itakuwa na uwezo na kutumikia taifa," alisema mpatanishi wa Umoja wa Afrika Mohamed El Hacen Lebatt katika mkutano na waandishi habari mjini Khartoum.

Sudan ametikiswa na mgogoro wa kisiasa tangu jeshi lilipomuondoa kiongozi wa muda mrefu Omar al- Bashir mwezi Aprili kufuatia maandamano ya umma dhidi ya utawala wale, ambapo majenerali waliotwaa madaraka walikataa matakwa ya waandamanaji kukabidhi mamlaka kwa utawala wa kiraia.

Zehntausende Menschen marschieren in Khartoum auf den Straßen (Reuters/U. Bektas)

Waandamanaji wakiwa katika mojawapo ya maandamano kudai mamlaka ya kiraia mjini Khartoum, Sudan, Juni 30, 2019.

Naibu kiongozi wa baraza la kijeshi Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo, amesema makubaliano ya sasa hayambaguwi yeyote.

"Tungependa kuvifahamisha vyama vyote vya kisiasa na mavuguvugu yote na vijana wote waliochangia kwenye mapinduzi, na wanawake wote,kwamba makubaliano haya yatakuwa makubaliano jumla bila kumuacha yeyote nje na inapaswa kuwa Wasudan wote na mapinduzi yao."

Muundo wa serikali mpya

Mzozo kati ya pande mbili uliongezeka baada ya uvamizi wa kikatili dhidi ya kambi ya muda mrefu ya maandamano nje ya makao makuu ya jeshi mjini Khartoum uliosababisha vifo vya dazeni kadhaa za watu na kuwajeruhi mamia Juni 3.

Lebatt hakuzungumzia muundo kamili wa chombo kipya tawala, lakini kiongozi maarufu wa maandamano Ahmed al-Rabie amesema kitajumlisha raia sita, wakiwemo watano kutoka vuruguvugu la maandamano, na wanachama watano wa jeshi.

Sudan Khartum | General Mohamed Hamdan Dagalo, Rapid Support Forces (RSF) (Reuters/M.N. Abdallah)

Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo, naibu mkuu wa Baraza la kijeshi la Sudan, na kiongozi wa kikosi chenye nguvu cha Rapid Support Forces (RSF).

Duru hii ya karibuni ya mazungumzo ilianza tena siku ya Jumatano baada ya upatanishi mkubwa wa wajumbe wa Ethiopia na Umoja wa Afrika, ambao waliwasilisha muswada wa pendekezo ili kumaliza mkwamo uliodumu kwa wiki kadhaa.

Mpango huo unapendekeza kuwepo kipindi cha mpito cha miaka mitatu, ambapo urais wa chombo tawala utashikiliwa na jeshi kwa kipindi cha miezi 18 ya kwanza na kisha raia kwa kipindi cha pili. Hata hivyo, haikuwa bayana bado iwapo pande zote zimekubaliana juu ya jeshi kushika wadhifa huo kwanza.

Lebatt amesema hata hivyo kwamba pande hizo mbili zimekubaliana kuahirisha uundwaji wa bunge jipya la mpito, ambalo lilikuwa limekubaliwa kabla ya kuvunjika kwa makubaliano ya awali, likiwa na wawakilishi 300, theluthi mbili kati yao wakitokea vuguvugu la maandamano.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afptv,ape,rtre

Mhariri: Daniel Gakuba