1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi lashinikizwa likabidhi Madaraka Burkina Faso

4 Novemba 2014

Umoja wa Afrika umewapa muda wa wiki mbili wanajeshi wa Burkina Faso wakabidhi madaraka kwa raia na kumteuwa waziri mkuu wa zamani wa Togo Edem Kodjo kuwa mjumbe wake maalum nchini humo.

https://p.dw.com/p/1DgT1
Luteni kanali Zida na kiongozi wa upinzani DiabrePicha: Reuters/J. Penney

Umoja wa Afrika umetangaza kipindi cha wiki mbili kwa jeshi kukabidhi hatamu za uongozi kwa raia baada ya afisa mmoja kutwaa uongozi wa kipindi cha mpito mara baada ya Blaise Compaoré kujiuzulu.

Mwenyekiti wa halmashauri ya Umoja wa Afrika bibi Nkosazana Dlamini Zuma aliyetangaza uamuzi wa kuteuliwa Edem Kodjo amesema katika taarifa yake kwamba uamuzi huo ni sehemu ya juhudi za Umoja wa Afrika zilizolengwa kurahisisha kupatikana ufumbuzi wa mzozo wa Burkina Faso na hasa kwa kubuniwa haraka kipindi cha mpito cha kidemokrasia kitakachoanzishwa kwa ridhaa ya pande zote na kupelekea kuitishwa haraka iwezekanavyo uchaguzi huru na wa uwazi.

"Bwana Kodjo atasimamia juhudi za Umoja wa Afrika kwa ushirikiano pamoja na jumuia ya ushirikiano wa kiuchumi wa nchi za Afrika magharibi-ECOWAS,Umoja wa mataifa na mashirika mengineyo husika ya kimataifa"-taarifa ya Umoja wa Afrika imesema.

Baada ya kujiuzulu rais wa zamani wa Burkina Faso Blaise Compaoré,kufuatia shinikizo la wananchi majiani,na baada ya kuitawala nchi hiyo kwa muda wa miaka 27,jeshi lilimteua mwenzao luteni nali Zida asimamie kipindi cha mpito.

Uamuzi huo wa jeshi haukuwaridhisha wananchi wala jumuia ya kimataifa waliowataka wanajeshi wawakabidhi raia haraka hatamu za uongozi wa kipindi cha mpito.

Luteni kanali Zida adhihirika kuheshimu katiba

Luteni kanali Isaac Zida ameahidi kuunda kipindi cha mpito "Kuambatana na katiba",akiashiria kuwakabidhi hatamu za uongozi raia.

Burkina Faso - Oberst Isaac Zida
Luteni kanali Isaac ZidaPicha: ISSOUF SANOGO/AFP/Getty Images

Katika mkutano pamoja na mabalozi wa nchi za nje mjini Ouagadougou,luteni kanali Isaac Zida alithibitisha hatamu za uongozi zitaendeshwa na taasisi ya mpito kuambatana na katiba.Taasisi hiyo ya mpito itateuliwa na pande zote zinazohusika nchini Burkina Faso amesema na kusisitiza angependelea jambo hilo lifanyike haraka.

"Hatukuja kutumia vibaya madaraka" alisema baadae luteni kanali Zida mbele ya waandishi habari.

Kwa mujibu wa katiba iliyosimamishwa na jeshi tangu ijumaa,spika wa bunge ndie anaestahiki kukabidhiwa uongozi pindi rais akiwa hayuko.Lakini na bunge pia limevunjwa muda mfupi baada ya jeshi kutwaa madaraka,na spika hajulikani aliko.

Kwa mujibu wa kiongozi wa upinzani Ablassé Ouedraogo,Zida amedhamiria kweli kuheshimu katiba.

Hali imeanza kuwa ya kawaida Ouagadougou

Tangazo la luteni kanali Zida linaloashiria raia huenda akakabidhiwa hatamu za uongozi za kipindi cha mpito,limefuatia shinikizo la Marekani,Ufaransa,Umoja wa Afrika ,jumuia ya ECOWAS, Umoja wa Ulaya na mashirika mengine ya kimataifa linalowataka wanajeshi wakabidhi haraka madraka kwa raia.

Karte Burkina Faso Französisch
Ramani ya Burkina Faso

Mjini Ouagadougou hali inasemekana ni shuwari,shughuli za usafiri zimerejea kuwa za kawaida,soko kuu ambalo lilifungwa tangu siku sita zilizopita kwasababu ya machafuko,limefunguliwa upya ,sawa na shule ambazo zilifungwa tangu octoba 27 iliyopita.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman