1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi lajaribu kutuliza waandamanaji

31 Januari 2011

Jeshi la Misri linajaribu kuwatuliza waandamanaji waliokusanyika katika uwanja wa Tahrir mjini Cairo, huku serikali ikiahidi kuzungumza na upinzani ili kumaliza mkwamo wa kisiasa uliosababishwa na maandamano hayo.

https://p.dw.com/p/107iM
Waandamanaji mjini Cairo
Waandamanaji mjini CairoPicha: dapd

Maandamano dhidi ya utawala wa Rais Hosni Mubarak, yanaingia siku yake ya saba. Leo waandaaji wake wameitisha mgomo mkubwa wa kitaifa, na kesho wameitangaza kuwa ni siku ya maandamano makubwa zaidi wanayoyaita "Maandamano ya Watu Milioni Moja".

Tangu jana wamekusanyika kwenye uwanja wa Tahrir, wakikaidi amri ya serikali ya kuwataka wachawanyike na kutotoka nje saa za usiku.

Mubarak atembelea majeshi

Rais Hosni Mubarak
Rais Hosni MubarakPicha: dapd

Kwa mujibu wa televisheni ya taifa ya nchi hiyo, Rais Mubarak amemuagiza rasmi waziri mkuu aliyemteua jana, Ahmed Shafiq, alishughulikie mara moja suala na ukosefu wa ajira, na pia kuitisha mdahalo wa moja kwa moja na vyama vya siasa, ili kuruhusu ushiriki mpana wa umma wa Misri kwenye utawala wa nchi yao.

Lakini yote haya hayaonekani kuwatosha waandamanaji, kwani waandamanaji wanasema wanachokitaka wao ni kuondoka tu kwa Mubarak na kundi lake.

"Tunataka watu ndio waunde serikali, hatumtaki (rais) Mubarak wala (makamo wa rais, Omar) Suleiman. Mubarak aihame kabisa nchi yetu ili kuepuka umwagikaji damu zaidi, na hatumuungi mkono Suleiman wala waziri mkuu mpya (Ahmed Shafiq). Tunachotaka ni mageuzi kamili kutoka utawala huu." Amesema mmoja wa waandamaji.

Upinzani wajipanga upya

Mohammed El-Baradei
Mohammed El-BaradeiPicha: AP

Kwa upande mwengine, tayari upinzani umejikusanya pamoja kwa ajili ya mazungumzo na utawala wa Mubarak, huku kundi kubwa zaidi likiwa la Ikhawanul-Muslimin (Ndugu wa Kiislamu), ambalo limemuidhinisha mshindi wa amani ya Nobel, Mohammed El-Baradei, kuwawakilisha kwa niaba ya upinzani wote.

Vile vile, makundi mengine ya upinzani, yanasema yanakusudia kuzungumza na jeshi, chombo kinachoheshimiwa sana nchini Misri, na ambacho hadi sasa kimejiepusha na kutumia nguvu dhidi ya raia, ingawa hakijaonekana kumuacha mkono moja kwa moja Mubarak.

Tangu jana, televisheni ya serikali imekuwa ikimuonesha Mubarak akivitembelea vikosi vya jeshi, katika kile kinachoonekana kuwa ni kuuthibitishia ulimwengu, kwamba bado yeye ndiye anayeshikilia hatamu za nchi.

Baraza la mawaziri bado

Mwandamanaji na bango linalosomeka: "Mubarak ng'oka!"
Mwandamanaji na bango linalosomeka: "Mubarak ng'oka!"Picha: AP

Bado waziri mkuu mteule, Shafiq, hajatangaza baraza lake la mawaziri, na Wamisri wanasubiri kuona ikiwa atamrudisha kwenye nafasi yake Waziri wa Mambo ya Ndani, Habib Al-Adly, ambaye wanamshutumu kwa kuamrisha vikosi vya usalama kuwafyatulia risasi raia na kutekeleza aina nyengine za mateso, si katika maandamano haya tu, bali kwa miaka mingi huko nyuma.

Kwengineko, katika mitaa mbalimbali, kunaripotiwa kuwa askari-kanzu wameanza kuonekana barabarani, baada ya kutoweka kwa zaidi ya siku mbili.

Baadhi ya maofisa wa polisi wanashukiwa kushiriki kwenye uporaji wa mali za raia na serikali, jambo ambalo liliwalazimu wananchi kuweka ulinzi wao wenyewe kwenye mitaa na majengo ya serikali.

Mtikisiko katika uchumi wa dunia

Maandamano ya kuwaunga mkono Wamisri mjini Berlin, Ujerumani
Maandamano ya kuwaunga mkono Wamisri mjini Berlin, UjerumaniPicha: dapd

Wakati huo huo, masoko ya fedha hapa Ulaya yameendelea kuathiriwa na hali ya hali inayoendelea nchini Misri. Asubuhi ya leo, thamani ya hisa zilishuka kwa asilimia 0.4 sawa na alama 1,139.58, huku katika mabenki makubwa kama vile Barclays, Societe Generale na UniCredit, ikianguka baina ya asilimia 1.2 na 2.8.

Katika soko la dunia, bei ya pipa moja la mafuta yasiyosafishwa imefikia dola 100 za Kimarekani.

Eneo la Mashariki ya Kati na Afrika ya Kaskazini linatoa robo tatu ya mafuta duniani, na migogoro katika nchi nyingi za eneo hili, inatazamiwa kuathiri uchumi wa dunia kwa kiasi kikubwa kabisa kuwahi kutokea katika siku za karibuni.

Mwandishi: Mohammed Khelef/DPAE/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman