Jeshi laingilia mzozo wa kisiasa Pakistan | Matukio ya Kisiasa | DW | 29.08.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Jeshi laingilia mzozo wa kisiasa Pakistan

Jeshi la Pakistan limeamua kuwa mpatanishi kati ya Waziri Mkuu Nawaz Sharif na upinzani, ingawa wengine wanahofia kuwa hiyo ni njia ya kuzidisha ushawishi wake kwenye mzozo huo wa madaraka.

Mkuu wa Majeshi wa Pakistan, Jenerali Raheel Sharif, akizungumza na Waziri Mkuu Nawaz Sharif.

Mkuu wa Majeshi wa Pakistan, Jenerali Raheel Sharif, akizungumza na Waziri Mkuu Nawaz Sharif.

Mkuu wa majeshi wa Pakistan, Jenerali Raheel Sharif, ametangazwa kwamba sasa ndiye mpatanishi mkuu kati ya kambi mbili zinazolumbana, lakini kuna uvumi huenda jeshi likayatumia maandamano yanayofanyika dhidi ya Nawaz Sharif kutanua makucha dhidi ya serikali iliyopatikana kwa njia ya kura.

Kwa zaidi ya wiki mbili sasa, Pakistan imekuwa ikishuhudia maandamano ya umma, ambapo waandamanaji wanaoongozwa na ulamaa mwenye ushawishi mkubwa, Tahir ul-Qadri, na bingwa wa zamani wa kriketi aliyegeuka kuwa mwanasiasa, Imran Khan, wamepiga kambi nje ya jengo la bunge wakimtaka Sharif ajiuzulu.

Majaribio kadhaa ya kuutatua mzozo huu yamekwama hadi sasa, hali inayotishia kuugeuza kuwa fujo kwani maelfu ya watu wanazidi kumiminika kwenye mji mkuu kila uchao, wengine wakiwa na silaha za kienyeji kama vile bakora.

Akizungumza na umati wa wafuasi wake usiku wa jana, Qadri jeshi ndilo lililokuwa limetoa pendekezo la kuwa mpatanishi, ambalo naye amelikubali.

"Nataka nimshukuru mkuu wa majeshi na jeshi la Pakistan kama taasisi, kwa kujitokeza kuuafuti mgogoro huu suluhisho la kisiasa. Sikumbuki mfano wowote kwenye historia yetu ambapo nguvu ya umma iligongana na serikali kuu ya shirikisho na jeshi la Pakistan limejitokeza rasmi kuwa mpatanishi na mhakikishaji wa usalama." Alisema Qadri.

Hofu za ushawishi wa jeshi

Kiongozi wa chama cha Pakistan Awami Tehreek, Tahir ul Qadri.

Kiongozi wa chama cha Pakistan Awami Tehreek, Tahir ul Qadri.

Qadri alidai kuwa mkuu wa majeshi amemuomba ampe masaa 24 tu kuutatua mzozo huu, ambapo ndani ya kipindi hicho jeshi litakusanya na kuyaweka pamoja madai ya waandamanaji na kuhakikisha yanatekelezwa.

Naye Khan, akizungumza muda mfupi baada ya ulamaa huyo, alithibitisha kwamba mazungumzo yataendelea. "Sasa ninakwenda kwenye majadiliano. Na Mungu akipenda, ama kesho tutakuwa na sherehe hapa hapa, au vuguvugu hili litapaswa kuchukuwa muelekeo mpya."

Idara ya habari ya jeshi ilituma taarifa kwenye mtandao wa Twitter kwamba mkuu wa majeshi, Jenerali Raheel Sharif, angelikutana na upinzani baadaye jioni ya jana, ingawa hakukuwa na taarifa nyengine yoyote rasmi iliyotolewa.

Pakistan, ambalo ni taifa lenye nguvu za nyuklia likiwa na raia milioni 180, limekuwa likiongozwa kijeshi kwa takribani nusu ya historia yake na mara kwa mara limekuwa likining'inia baina ya demokrasia na utawala wa kijeshi. Nawaz Sharif mwenyewe alipinduliwa na jeshi mwaka 1999 wakati akiwa madarakani.

Baadhi ya maafisa kwenye serikali ya Sharif wamelishutumu jeshi lenyewe kwa kuchochea maandamano haya kama njia ya kumdhoofisha waziri huyo mkuu, na wengi wanaamini majaaliwa ya vuguvugu hili la kuipinga serikali yamo hasa mikononi mwa jeshi.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AP/AFP
Mhariri: Saumu Yussuf

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com