1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi la Ukraine kutoondowa silaha nzito

23 Februari 2015

Jeshi la Ukraine limesema Jumatatu (23.02.2015) haliwezi kuanza kuondowa silaha nzito kutoka eneo la mapambano wakati waasi wanaoiunga mkono Urusi wakiendelea kushambulia vikosi vya serikali.

https://p.dw.com/p/1Eg07
Wanajeshi wa serikali mashariki mwa Ukraine.
Wanajeshi wa serikali mashariki mwa Ukraine.Picha: Reuters/G. Garanich

Mwishoni mwa juma waasi na jeshi la serikali wamesema wamefikia makubaliano ya kuanza mchakato wa kuondowa silaha nzito kama ilivyotakiwa na makubaliano ya kusitisha mapigano ambayo yameanza kufanya kazi tarehe 15 mwezi wa Februari.

Msemaji wa jeshi la Ukraine Anatoly Stelmakh amesema matumizi ya nguvu yamepunguwa sana katika siku za hivi karibuni lakini waasi wameshambulia vikosi vya serikali mara mbili jana usiku.

Msemaji mwengine wa jeshi akizungumza kupitia televisheni amesema kutokana na kuendelea kushambuliwa kwa maeneo yanayoshikiliwa na wanajeshi wa Ukraine hakuwezi kuwepo kwa mazungumzo yoyote yale ya kundowa silaha nzito.Waraka wa makubaliano ya kuondowa silaha ulisainiwa jana usiku ambapo zoezi hilo lilitakiwa liwe limekamilika katika kipindi kisichozidi wiki mbili.

Mchakato wa amani

Vikosi vya waasi mashariki mwa Ukraine.
Vikosi vya waasi mashariki mwa Ukraine.Picha: Reuters/B. Ratner

Uratibu wa kuondowa silaha kwa pamoja umetajwa katika makubaliano ya kusitisha mapigano yaliosaniwa katika mji mkuu wa Balarus Minsk lakini utekelezaji wake umecheleweshwa kutoka na mapigano katika mji wa Debaltseve kituo kikuu cha usafiri wa reli ambapo vikosi vya serikali vilijiondowa hapo.

Waraka wa makubaliano ya kuondowa silaha ulisainiwa jana usiku ambapo zoezi hilo lilitakiwa liwe limekamilika katika kipindi kisichozidi wiki mbili.Jumatano.Hapo Jumamosi pande hizo mbili pia zilibadishana wafungwa 191.

Mripuko wa bomu katika maandamano ya wafuasi wa serikali katika mji wa mashariki wa Kharkiv umeuwa watu wawili na kutia dosari juhudi za kupiga hatua kwa mpango wa amani mashariki mwa Ukraine.

Kumbukumbu ya mapinduzi

Hata hivyo mjini Kiev maandamano kama hayo kuadhimisha kumbukumbu ya mwaka mmoja ya mapinduzi ya Maidan yamefanyika bila ya vurugu zozote zile za matumizi ya nguvu.

Wananchi walioandamana Kiev. (22.02.2015)
Wananchi walioandamana Kiev. (22.02.2015)Picha: Reuters/V. Ogirenko

Zaidi ya waandamanaji 100 wanaounga mkono mataifa ya magharibi waliuwawa mwaka mmoja uliopita wakati aliyekuwa rais wakati huo Viktor Yanukovych alipotumia nguvu kuvunja maandamano ya watu waliokuwa wakitaka aondolewe.Alikimbilia Urusi tarehe 22 Februari mwaka 2014.

Petro Poroshenko ambaye baadae alichaguliwa kuchukuwa nafasi yake aliwaalika marais wa Ujerumani, Poland, Lituhuania, Slovakia na Georgia kuhudhuria maandamano hayo katika uwanja mkuu wa Kiev Maidan ambao ulikuwa kitovu cha maandamano ya kudai demokrasia na kuunga mkono mataifa ya magharibi.

Gwaride la Utu

Poroshenko alitia ngosho na kutembea bega kwa bega na Rais wa Ujerumani Joachim Gauck na viongozi wengine wa kigeni kupita katika maeneo ya kumbukumbu ya wahanga hadi katika uwanja wa Maidan yaani Uwanja wa Uhuru nchini Ukraine.

Rais Petro Poroshenko wa Ukraine(kushoto) na Rais wa Ujerumani Joachim Gauck (katikati) wakati wa maandamano mjini Kiev.(22.02.2015)
Rais Petro Poroshenko wa Ukraine(kushoto) na Rais wa Ujerumani Joachim Gauck (katikati) wakati wa maandamano mjini Kiev.(22.02.2015)Picha: S. Gallup/Getty Images

Rais Gauck wa Ujerumani amesema amekwenda Kiev kuonyesha mshikamano na vuguvugu la demokrasia la Ukraine.

Takriban watu 10,000 inakadiriwa kuwa walijitokeza kwa ajili ya maandamano hayo yaliyopewa jina la "Gwaride la Utu". Wengi wao walikuwa wakipeperusha bendera za Ukraine na kuchukuwa mabango yenye kusomeka "Sisi ni watu wa Ulaya."

Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters/dpa

Mhariri : Iddi Ssessanga