Jeshi la Ujerumani kufanyiwa mageuzi baada ya kashfa-Waziri | Matukio ya Kisiasa | DW | 10.05.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Jeshi la Ujerumani kufanyiwa mageuzi baada ya kashfa-Waziri

Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Ursula von der Leyen  amesema ataanzisha mageuzi katika jeshi la nchi hiyo, kufuatia ugunduzi wa mienendo ya kushabikia unazi miongoni mwa wanajeshi.

Deutschland Von der Leyen mit Volker Wieker nach der Sondersitzung (picture-alliance/dpa/M. Kappeler)

Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Ursula von der Leyen (kulia)

Waziri Ursula von der Leyen ameitangaza azma hiyo mjini Berlin, wakati uchunguzi ukiwa tayari unaendelea kuhusu visa vya wanajeshi wa Ujerumani kubainika na mienendo inayoashiria misimamo mikali ya kizalendo, ambayo imezusha masuali kuhusu uwezo wa uongozi kwa upande wa Bi von der Leyen. Akizungumza asubuhi leo mbele ya kamati ya bunge inayohusika na masuala ya ulinzi, waziri huyo amesema mchakato wa mageuzi utakuwa mpana, na utawagusa wanajeshi wengi, kuanzia ngazi ya chini hadi ya juu kabisa.

''Nimewasilisha hatua tofauti ambazo tutazichukua kuanzia kanuni za kinidhamu jeshini hadi mpango mpya wa uongozi wa ndani katika jeshi'' amesema von der Leyen na kuongeza kuwa hayo yatajumuisha kwa aina ya pekee kutazama upya maagizo yaliyokuwepo, na pia kutathmini upya elimu ya siasa katika jeshi letu. 

Mkururo wa kashfa za siasa kali

Deutschland Von der Leyen trifft Führungskräfte der Bundeswehr (picture-alliance/dpa/M. Kappeler)

Sura ya Jeshi la Ujerumani (Bundeswehr) imetiwa doa na mienendo ya siasa kali za mrengo wa kulia miongoni mwa baadhi ya wanajeshi.

Juhudi hizi zinakuja siku moja baada ya kukamatwa kwa mwanajeshi aliyetambulishwa kama Maximilian T, kama mshukiwa katika njama ya kufanya mashambulizi yenye kushawishiwa na mtizamo mkali wa kizalendo, kuwalenga maafisa wa ngazi ya juu nchini Ujerumani, mashambulizi ambayo wakimbizi wangesingiziwa kuyafanya.

Maximilian T. anahusishwa na mshukiwa mwingine anayejulikana na Franco A., afisa mwingine wa jeshi la Ujerumani ambaye alitaka kujifanya mkimbizi kutoka Syria, ili lawama dhidi ya mashambulizi aliyopanga kuyafanya ziwaendee wakimbizi.

Waziri Ursula von der Leyen ambaye anatoka katika chama cha Christian Democratic Union CDU cha Kansela Angela Merkel, amekuwa akishambuliwa kutoka kila upande wa kisiasa, kwa kushindwa kung'amua mapema mfumo wa siasa kali za kizalendo miongoni mwa wanajeshi.

Jeshi la Ujerumani, Bundeswehr kwa wakati huu linaendesha msako katika kambi zote za jeshi kutafuta vitu vya ukumbusho wa enzi za utawala wa wanazi, katika mchakato mzima wa kuwatambua wanajeshi wenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia. Vitu vya aina hiyo viligunduliwa katika kambi mbili, moja wapo ikiwa Illkirch alikokuwa akiishi mshukiwa Franco A.

Msako wa washukiwa wa ugaidi

Deutschland Hildesheim Polizei verhaftet Islamisten (Getty Images/A. Koerner)

Polisi wa Ujerumani katika upekuzi wa nyumba za washukiwa wa ugaidi

Wakati mageuzi hayo yakipendekezwa jeshini, ofisi ya Mwendeshamashtaka wa Shirikisho la Ujerumani Frauke Koehler amesema polisi wamefanya upekuzi kwenye nyumba za watu katika majimbo manne, kuhusiana na watu watatu wanaoshukiwa kuwa na mafungamano na kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS. Majimbo yaliyohusika katika upekuzi huo ni Berlin, Bavaria, Saxon na Saxony-Anhalt.

Washukiwa wawili kuhusiana na msako huo wanatuhumiwa kuwa wanachama wa kundi la kigaidi, huku wa tatu akishukiwa kuunga mkono kundi hilo.

Waendeshamashitaka wamesema washukiwa hao wana uhusiano na raia wa Syria aliyekamatwa mwaka 2016, akituhumiwa kutaka kufanya shambulio la bomu, na pia msyria mwingine aliyekamatwa wiki iliyopita mjini Leipzig, ambaye pia anakabiliwa na mashitaka ya kuwa mwanachama wa kundi la IS.

Mwandishi: Daniel Gakuba/ape, dpae, rtre

Mhariri: Iddi Ssessanga

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com