1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

Jeshi la Sudan lasema al-Bashir yuko hospitali ya kijeshi

26 Aprili 2023

Kikosi cha Rapid Support Forces, RSF, cha Sudan kilivunja magereza matano na kuwaachia wafungwa, ikiwemo gereza la Kober, Khartoum ambako rais wa zamani Omar Hassan al-Bashir na maafisa wa zamani walikuwa wanashikiliwa.

https://p.dw.com/p/4QZrP
Sudan | Präsident Omar al-Bashir
Picha: Mohamed Khidir/Xinhua/Imago

Jeshi la Sudan limesema rais wa zamani aliepinduliwa Omar Hassan al-Bashir anashikiliwa katika hospitali ya kijeshi chini ya usimamizi wa polisi, huku wizara ya mambo ya ndani ikisema leo kuwa wapiganaji wa kikosi kinachopambana dhidi ya jeshi cha Rapid Support Forces, RSF, walivunja magereza matano na kuwaachilia huru wafungwa, likiwemo gereza la Kober lililopo mji mkuu wa Khartoum, ambako rais huyo wa zamani na maafisa wengine wa ngazi ya juu walikuwa wanashikiliwa.

Polisi imesema uvamizi dhidi ya gereza la Kober ulipelekea kuuawa na kuwajeruhiwa kwa maafisa kadhaa wa magereza, na kuongeza kuwa RSF iliwaachia wote waliokuwa wanashikiliwa katika gereza hilo, katika uvamizi uliofanyika kati ya Aprili 21 hadi 24.

Soma pia: Ujerumani yakamilisha zoezi la kuwahamisha watu wake kutoka Sudan

Hata hivyo jeshi limesema Bashir alikuwa amehamishwa kutoka gereza la Kober kabla ya kuzuka mapigano kati ya jeshi na RSF, kufuatia ushauri wa wafanyakazi wa afya.

Maswali kuhusu wapi alipo al-Bashir yalianza kuibuka baada ya waziri wa zamani katika serikali yake, ambaye anatakiwa na mahakama ya kimataifa ya uhalifu, ICC, Ahmed Haroun, kutoroka kutoka gereza hilo la Kober.

Sudan | Präsident Omar al-Bashir
Rais wa zamani wa Sudan Omar Hassan al-Bashir akiwa kwenye kampeni enzi za utawala wake. Jeshi la Sudan limesema Badhir hivi sasa anashikiliwa katika hospitali ya kijeshi ya Aliyaa mjini Khartoum chini ya uangalizi wa uangalizi wa polisi.Picha: Ashraf Shazly/AFP/Getty Images

Haroun alisema yeye na maafisa wengine wa zamani katika serikali ya Bashir waliondoka Kober na watachukuwa dhamana ya kujilinda wenyewe, katika taarifa iliorushwa kupitia kituo cha televisheni cha Tayba jana Jumanne.

Kwa mujibu wa taarifa ya jeshi, al-Bashir, waziri wa zamani wa ulinzi Abdel-Rahim Muhammad Hussein na maafisa wengine wa zamani walikuwa wamehamishiwa hospitali ya Aliyaa inayoendeshwa na jeshi kabla ya kuaanza kwa makabiliano Aprili 15.

Bashir aliondolewa madarakani mnamo 2019 katikati mwa maandamano makubwa ya umma. Yeye na Hussein wanatakiwa na ICC kwa makosa ya mauaji ya kimbari, uhalifu dhidi ya ubinadamu na uhalifu wa kivita kuhusiana na mzozo wa Darfur.

Khartoum, Omduruman yaripoti mapigano

Mapema Jumatano mji mkuu wa Kharotum na mji jirani wa Omdurman imeripoti makabiliano ya hapa na pale kati ya jeshi la RSF, lakini imesema ukubwa wa mapigano umepungua katika siku ya pili ya mapatano ya kusitisha mapigano ya siku ya tatu.

Soma pia: Mapigano kusitishwa kwa masaa 72 nchini Sudan

Wakaazi wengi wa mji mkuu walijitokeza kutoka majumbani mwao kutafuta chakula na maji, wakipanga foreni kwenye maduka ya kuoka mikate na maduka ya chakula, walisema mashuhuda. Baadhi walikagua maduka na nyumba ambavyo vimeharibiwa au kuporwa wakati wa mapigano. Wengine waliungana na maelfu waliokuwa wanaondoka kutoka mjini humo katika siku za karibuni.

"Kuna hali ya utulivu katika eneo langu na vitongoji," alisema Mahasen Ali, muuzaji chai ambaye anaishi katika kitongoji cha kusini cha Khartoum cha May. "Lakini wote wanahofia kitakachofuata." Alisema licha ya utulivu kiasi, milio ya risasi na milipuko bado ilisikika jijini.

Mapigano yalijikita katika maeneo machache ya Khartoum na Omdurman, wakaazi walisema, hasa karibu na makao makuu ya jeshi na Ikulu ya Jamhuri, makao makuu ya mamlaka. Majibizano ya risasi yalitanda katika kitongoji cha juu cha Kafouri, ambapo wapiganaji wengi kutoka kwa Kikosi cha cha kijeshi cha RSF wamepelekwa.

Kombobild Abdul Fattah Al-Burhan und Mohamed Hamdan Dagalo
Majenerali hasimu wanaowania udhibiti wa Sudan, Mkuu wa Majeshi Abdel Fattah al-Burhan, kushoto, na mkuu wa kikosi cha kijeshi cha RSF, Mohammed Hamdan Dagalo ambaye ni naibu wa Burhan katika utawala wa sasa wa kijeshi wa Sudan.Picha: Bandar Algaloud/Mahmoud Hjaj/AA/picture alliance

Idadi ya vifo, majeruhi yaongezeka

Takriban watu 459, wakiwemo raia na wapiganaji, wameuawa, na zaidi ya 4,000 wamejeruhiwa tangu mapigano kuanza, limesema shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO, likinukuu Wizara ya Afya ya Sudan. Shirika la Madaktari ambalo linafuatilia vifo vya raia, limesema takriban raia 295 wameuawa na wengine 1,790 kujeruhiwa.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameonya kwamba mzozo wao wa madaraka sio tu unaweka mustakabali wa Sudan hatarini, bali "unawasha fuse ambayo inaweza kulipuka mbali ya mipaka ya Sudan, na kusababisha mateso makubwa kwa miaka mingi, na kurudisha maendeleo nyuma kwa miongo kadhaa."

Soma pia: Nchi za kigeni ziko mbioni kuwaokoa raia wao Sudan

Guterres alitaja ripoti za mapigano ya silaha kote nchini, na watu wanaokimbia makazi yao katika majimbo ya Blue Nile na Kordofan Kaskazini na katika Darfur Magharibi pia. Joyce Msuya, msaidizi wa katibu mkuu wa masuala ya kibinadamu, aliliambia Baraza la Usalama "kumekuwa na ripoti nyingi za unyanyasaji wa kingono na kijinsia."

Msuya alisema Umoja wa Mataifa umepokea ripoti "za makumi ya maelfu ya watu wanaowasili katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, Chad, Misri, Ethiopia na Sudan Kusini."

Usitishaji mapigano wa saa 72 uliotangazwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken ungedumu hadi Alhamisi usiku. Wengi wanahofia kwamba mapigano yataongezeka mara tu uhamishaji wa wageni, ambao ulionekana kuwa katika hatua zao za mwisho, utakapokamilika.

Mapigano mapya yaua watu takribani 100 Sudan

Hofu ya kuvuja kwa kemikali za kibayolijia

Shirika la Afya Duniani, wakati huo huo, limeonyesha wasiwasi kwamba moja ya pande zinazopigana umechukua udhibiti wa maabara kuu ya afya ya umma mjini Khartoum, ambapo sampuli za polio, surua na kipindupindu huhifadhiwa. Dk. Nima Saeed Abid, mwakilishi wa WHO nchini Sudan alionya kwamba baada ya wafanyakazi kufukuzwa na kukatwa kwa umeme, haiwezekani kusimamia ipasavyo nyenzo za kibaolojia.

Soma pia: Sudan: Guterres atoa wito wa kusitishwa mapigano

Burhan na Dagalo waliingia madarakani baada ya ghasia za mwaka 2019 kusababisha majenerali kumuondoa mtawala wa muda mrefu wa Sudan Omar al-Bashir. Wasudan tangu wakati huo wamekuwa wakijaribu kuunda utawala wa kidemokrasia, lakini mnamo 2021 Burhan na Dagalo waliungana katika mapinduzi ambayo yaliiondoa serikali ya mpito.

Wametofautiana sasa kutokana na mvutano kuhusu mpango mpya wa kuanzisha tena utawala wa kiraia. Wanajeshi na RSF wana historia ndefu ya kuwatendea ukatili wanaharakati na waandamanaji pamoja na ukiukwaji mwingine wa haki.

Chanzo: Mashirika