Jeshi la Somalia lawauwa al-Shabba 16, kuwakomboa watoto 40 | Matukio ya Afrika | DW | 28.09.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Jeshi la Somalia lawauwa al-Shabba 16, kuwakomboa watoto 40

Jeshi la Somalia limewauwa wanamgambo 16 wa kundi la itikadi kali la Al Shabaab katika mkowa wa Lower Shabelle katika juhudi za kuwakombowa watoto kadhaa waliokuwa wakishikiliwa na kundi hilo.

Kamanda mwandamizi wa jeshi la Somalia Ahmed Hassan amesema watoto hao walitekwa nyara na kundi hilo  kama sehemu ya uwezekano wa kuwatumia kama wapiganaji baadae.

Wanajeshi hao walikikomboa kijiji cha Nuunay ambako kundi hilo la wanamgambo lilikuwa likiwashikilia watoto takriban 40 ambao walipanga kuwatumia kama washambuliaji wa kujitowa muhanga na wapiganaji wa siku za baadae. Watoto hao walikombolewa na jeshi hivi sasa linatarajia kuwarudisha kwa familia zao,kwa mujibu wa kamanda wa Jeshi.

Tukio hilo limeshuhudiwa siku ya Jumamosi. Kadhalika wanajeshi wa Somalia na Kenya walifyetuliana risasi kwa muda wa dakika kadhaa siku ya Jumamosi katika eneo la mpaka baina ya mataifa hayo mawili. Tukio hilo limefanyika baada ya jeshi la Kenya kufyetua risasi kuwazuia waandamanaji waliokuwa upande wa Somalia kuelekea upande wa Kenya.