Jeshi la serikali ya Kongo latandikwa na waasi wa Nkunda | Matukio ya Kisiasa | DW | 14.11.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Jeshi la serikali ya Kongo latandikwa na waasi wa Nkunda

Mgogoro wa sasa unaondelea mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo umedhirisha udhaifu wa jeshi la serikali kuweza kuilinda nchi hiyo dhidi ya uvamizi kikamilifu.

Wanajeshi wa jeshi la serikali la FARDC. Mbali na kuogopwa lakini pia linaogopa

Wanajeshi wa jeshi la serikali la FARDC. Mbali na kuogopwa lakini pia linaogopa

Hii ni kwa sababu limeshindwa kukabiliana vilivyo na wapiganaji wa Generali muasi Laurent Nkunda.

Machoni mwa raia wa mashariki mwa nchi hiyo, jeshi hilo linaonekana kama lisilo na nidhamu na ambalo limezongwa na ufisadi kutokana na madai kuwa askari wake wengi hawalipwi vizuri.

Jeshi la serikali ya Kinshasa limepata kipigo kutoka kwa wapiganaji wa Laurent Nkunda kiasi cha kuwawezesha waasi hao kuusogelea mji wa Goma.

Ukiacha kipigo cha mwezi jana,jeshi hilo limeonyesha utovu wa nidhamu kwa mara nyingine tena wiki hii wakati wapiganaji wa Nkunda wanaposogea mbele. Inasemekana wanajeshi hao wamewaibia raia mali zao.

Msemaji wa kikosi cha kulinda amani nchini humo cha MONUC,wanajeshi wa serikali wameiba magari,kupora maduka na kufanya vitendo vingine alivyoita vya kinyama katika eneo la Kanyabayonga linalopatikana kaskazini mwa mji wa Goma.

Wanajeshi wa serikali takriban 26,700 wametumwa katika eneo la Kivu kaskazini.hata hivyo wameshindwa kutamba mbele ya wapiganaji wa Nkunda ambao licha ya kuwa wachache lakini wanaonekana kuwashinda wale wa serikali.

Ari ya wanajeshi iko chini. Raia wa kawaida wanaelewa hilo kuuliza wanawezaje kufanya vizuri ikiwa hawapati mshahara wao.

Hata malipo yao kwa ujumla ni duni.Mwanajeshi wa kawaida hupokea mshahara wa dola 65 kwa mwezi.

Isitishe ufisadi inasemekana umekithiri ndani y jeshi.Wanajeshi wengi hushutumiwa kutumia vyeo vyao kujipatia pesa kinyume na sheria.Vifaa vinavyonuiwa kwa wanajeshi walio mstari wa mbele,mara nyingi huishia katika masoko ya kawaida baada ya maofisa husika kupewa kiinua mgongo.

Afisa mmoja wa ngazi za juu wa ujumbe wa kidplomasia kutoka mataifa ya magharibi ameielezea hali ya jeshi la serikali katika Kivu Kaskazini kama ya vurugu tupu.

Ameongeza kuwa wanajeshi wa kawaida mra kadhaa huachwa peke yao huku maafisa wakiwa peke yao.Wote wanaihisi kama wamepuuzwa na utawala wa Kinshasa na wakati mwingine maafisa hao huchukua uamuzi usiofaa.

Baada ya kisa cha Kanyabayonga, msemaji wa serikali Lambert Mende alisema kuwa waliohusika na wizi wa ngawira wataadhibiwa akiongeza kuwa hawawezi kuvumilia vitendo ambavyo vinailiabisha jeshi la serikali.

Hata hivyo hii sio mara ya kwanza wanajeshi wa serikali wakifanya vitendo ambavyo si vya kawaida.

Mwaka jana MONUC ilisema kuwa asili mia 40 ya visa vya uvunjaji wa haki za binadamu nchini humo vilifanywa na wanajeshi wa serikali.

Shirika linalotetea haki za binadamu duniani la Human Rights watch nalo limetoa picha mbaya ya jeshi la serikali. Shirika hilo linasema kuwa wanajeshi hawakupewa mafuso yanayostahili, wengine hawana nidhamu,na wakati mwingine malipo yao si yakuridhisha na vitendea kazi vyao ni hafifu.

Pia shirika kama vile la Amnesty International linadai kutokea visa vya ubakaji katika maeneo ya mkoa wa Kivu Kaskazini mkiwemo mji wa Goma.

Na hayo yakiarifiwa Umoja wa Mataifa umeanza kusafirisha shehena ya kwanza y chakula cha msaada katika maeneo yanayodhibitiwa na waasi.Hii ndio mara ya kwanza kufanya hivyo tangu mapigano yaanze mwezi Oktoba.

Msemaji wa shirika la mpango wa chakula WFP anasema kuwa tani zaidi ya 100 za chakula zitatolewa kwa watu elf 60 walioko katika maeneo ya kaskazini mwa mji wa Goma katika kipindi cha siku nne zijazo.

 • Tarehe 14.11.2008
 • Mwandishi Kalyango Siraj
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Fv0F
 • Tarehe 14.11.2008
 • Mwandishi Kalyango Siraj
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Fv0F
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com