Jeshi la Myanmar lahimizwa kuwanusuru Warohingya | Matukio ya Kisiasa | DW | 27.10.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Myanmar

Jeshi la Myanmar lahimizwa kuwanusuru Warohingya

Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani Rex Tillerson ametoa wito kwa mkuu wa jeshi la Myanmar kusaidia kumaliza vurugu katika jimbo la Rakhine ambalo maelfu ya jamii ya Waislamu wa Rohingya wamelikimbia.

Waziri huyo wa mambo ya nje wa Marekani alizungumza kwa njia ya simu na mkuu huyo wa jeshi wa Myanmar, Min Aung Hlaing na alivihimiza vikosi vya usalama vya Myanmar kuisaidia serikali katika juhudi za kumaliza vurugu katika jimbo hilo la Rakhine na wakati huohuo, kuwaruhusu kurejea nyumbani  ale waliohama wakati wa mgogoro huo, hasa idadi kubwa ya jamii ya Rohingya.

Zaidi ya watu 600,000 wa jamii hiyo ya Waislamu walio wachache wamekimbilia nchini Bangladesh baada ya mgogoro ulioanza mwishoni mwa mwezi Agosti kuongezeka. Mashambulizi dhidi ya vikosi vya usalama vya Myanmar katika jimbo la Rakhine yalisabababisha msako mkubwa uliofanywa na jeshi wa kulisaka kundi la wapigananji wanaoitwa na raia wengi wa Burma kuwa ni wahamiaji haramu Kibengali. Waziri huyo wa mambo ya nje wa Marekani Rex Tillerson, ambaye alitembelea India nchi jirani ya Myanmar mnamo wiki hii, alihimiza katika mazungumzo yake na mkuu huyo wa jeshi juu ya kufanikisha misaada ya kibinadamu iweze kuwafikia wale waliopoteza makazi yao.

Wachunguzi wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wamesema kuchomwa moto vijiji, kuteswa viongozi wa jamii mauaji pamoja na ubakaji, ni vitendo vinavyoashiria hatua za kimakusudi zinazolenga kuwafukuza watu wa jamii ya Warohingya.  Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya Haki za Binadamu nchini Myanmar, Yanghee Lee, amesema Warohingya hawapati hata huduma za msingi.

Pakistan Islamabad US-Außenminister Rex Tillerson | (Reuters/A. Qureshi)

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Rex Tillerson

Tillerson ameliambia jeshi la Myanmar lishirikiane na Umoja wa Mataifa ili kuhakikisha uchunguzi kamili wa madai yote ya ukiukwaji wa haki za binadamu na pia kuhakikisha uwajibikaji. Marekani ilitangaza siku ya Jumatatu kuwa inaazimia kuwawekea vikwazo vikali maafisa wa jeshi la Myanmar waliohusika na vurugu na vilevile kuifuta mialiko ya kwenda Marekani kwa maafisa wa usalama wa ngazi ya juu.

Viongozi wa jeshi la Myanmar wapewa mzigo wa lawama

Hatua hizo zimechukuliwa baada ya Tillerson kusema Marekani inawatwika mzigo wa lawama viongozi wa kijeshi wa Myanmar na kwamba wanapaswa kuwajibika kutokana na mgogoro huo wa wakimbizi, huku akiweka tofauti serikali ya  kiraia ya Aung San Suu Kyi. Mkuu wa majeshi ya Myanmar Min Aung Hlaing mara kwa mara ameyatetea majeshi yake dhidi ya mashtaka ya kuwatendea Warohingya maovu. Katika taarifa yake moja aliyoichapisha kwenye ukurasa wake wa facebook alisema, taarifa za upande mmoja za kuilaumu Myanmar na vikosi vyake vya kijeshi kuhusu mashambulizi ya kigaidi yanayofanywa na Wabengalis wenye msiamo mkali katika jimbo la magharibi la Rakhine si za kweli.

Kwa miongo mingi Warohingya wamekuwa wananyimwa haki zao za msingi na jamii ya Mabuddha walio wengi nchini Myanmar. Katika misako ya hivi karibuni, vikosi vya usalama vya Myanmar viliwapiga risasi kiholela raia wasiokuwa na silaha, ikiwa ni pamoja na watoto. Kulingana na wachunguzi wa Umoja wa Mataifa vikosi hivyo pia viliwanyanyasa watu hao kijinsia.

Mwandishi: Zainab Aziz/DPAE/RTRE/AFPE

Mhariri: Grace Patricia Kabogo    

     

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com