1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi la Iraq limeingia kwa amani katika kiunga cha Sadr City

Kalyango Siraj20 Mei 2008

Pia Tariq Aziz mahakamani leo kujibu shtaka la mauaji

https://p.dw.com/p/E30H
Tariq Aziz akiwa kizimbani nchini Iraqi jumanne April 29, 2008 katika picha hii iliochukuliwa kutoka runinga wakati jaji akisoma jina lake. Aziz na wenzake wanakabiliwa na shtaka la mauaji ya mwaka 1992 ya wafanya biashara 42 walioshutumiwa kupandisha bei ya vyakula wakati nchi hiyo ilikuwa inakabiliwa na vikwazo vya kimataifa.Anatarajiwa kurejeshwa mahakani leo jumanne 20 Mai,2008.Picha: AP

Vikosi vya serikali ya Iraq vimeingia leo jumanne katika mtaa wa washia wa Sadr City bila ya upinzani kutoka kwa wanamgambo.

Mtaa huo unapatikana katika mji mkuu wa nchi hio wa Baghdad na umeshuhudia mapigano makali kati ya wanamgambo wa Kishia dhidi ya vikosi vya Marekani kwa mda wa wiki kadhaa.

Askari wa Iraq walioingia katika mtaa wa washia wa Sadr City walikuwa wamejihami na silaha nzito nzito.

Na hii ndio mara ya kwanza, katika kipindi cha wiki nane, kwa askari hao kufanya hivyo, tangu mapigano makali yazuke kati ya wanamgambo watiifu kwa kiongozi wa kidini Moqtada al-Sadr anaepinga Marekani dhidi ya vikosi vya usalama vya Marekani.

Maafisa wa usalama wa Iraq wanasema wameanzisha kile walichoita 'operesheni ya amani' katika mtaa huo ili kuondoa mabomu yaliyofichwa ardhini na wanamgambo katika vita vyao na wanajeshi wa Marekani.

Hatua ya vikosi vya Iraq kuingia katika mtaa wa washia, inakwenda sambamba na makubaliano yaliyofikiwa mapema mwezi huu kati ya serikali na vuguvugu la Sadr yenye nia ya kumaliza mapigano ya mitaani yaliyoanza mwezi machi mwaka huu.

Afrisa wa kijeshi aliokuwa anaongoza kikosi cha kwanza cha askari wa Iraq walioingia katika mtaa huo,ameliambia shirika la habari la AFP kuwa hali katika mtaa huo ilikuwa shwari na wananchi wanawakaribisha kwa mikono miwili, wanajeshi wake na kulikuwa hakujatokea shambulio lolote dhidi ya vijana wake.

Ni wanajeshi wa Iraq tu ndio walioingia huko huku wanajeshi wa Marekani wakiwa wamebaki nje ya kiunga hicho wakishika doria.

Mtaa huo wa washia unawakazi wanaokaribia millioni mbili, na watu mamia kadhaa wameuliwa tangu Waziri Mkuu,Nuri al-Malik, aamuru wanamgambo kuchukuliwa hatua kali za kuwapokonya silaha , katika mji wa Basra ulioko kusini mwa nchi hiyo.Amri hiyo ilianza machi.

Mapigano yalisambaa katika maeneo yote ya washia,hususan katika mtaa wa Sadr City,kunakopatikana kwa wingi,wanamgambo wa Sadr wanaoitwa,jeshi la Mahdi.

Maafisa wa Marekani na Iraq wanakiri kuwa visa vya ghasia vimepungua katika mtaa wa Sadr City tangu wafuasi wa Sadr walipokubaliana na serikali kusitisha hujuma siku tisa zilizopita,na badala yake kuvikubalia vikosi vya Iraq kuingia huko.

Hatua ya sasa ya majeshi ya Iraq ya kuingia mta wa Sadr City imekuja siku moja tu baada ya jeshi la Iraq kufanya upekuzi mkali wa nyumba hadi nyumba, katika mtaa mwingine wa Al-Shaab ambako liliwatia mbaroni washukiwa watano ambao ni wanachama cha jeshi la Mahdi.

Na hayo yakiarifiwa,kesi dhidi ya aliekuwa naibu wa waziri mkuu wa Iraq enzi za Saddam, Tariq Aziz na watu wengine saba wa utawala wa wakati huo, ilikuwa imepangwa kuanza kusikizwa leo,baada ya kuahirishwa kwa sababu za kiuratibu.

Aziz na wengine wanashtakiwa kwa kuamuru kuuawa kwa wafanyabiashara 42, mwaka wa 1992, baada ya kushtumiwa kuongeza bei ya vyakula wakati Iraq ilipokuwa chini ya vikwazo vya kimataifa.

Miongoni mwa washtakiwa wengine ni Watban Ibrahim al-Hassan, nduguye Saddam Hussein, mkuu wa zamani wa Benki kuu ya Iraq, Issam Hawshi, bila kusahau binamu wa Saddam Hussein, Ali Hassan al-Majid, maarufu kama Chemical Ali.

Chemical Ali, mwezi juni, alihukumiwa kunyongwa kutokana na mchango wake wakati wa vita dhidi ya WaKurdi, kaskazini mwa Iraq, ambapo wakati fulani ilitumiwa gesi ya sumu dhidi ya wakurdi hao.