Jeshi la Iraq lasherehekea ushindi Mosul | Matukio ya Kisiasa | DW | 10.07.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Jeshi la Iraq lasherehekea ushindi Mosul

Wanajeshi wa Iraq wanapambana kuikomboa sehemu iliyobaki mjini Mosul ambako wanamgambo wa kundi linalojiita Dola la Kiislamu – IS wanaidhibiti magharibi ya Mto Tigris.

Brigedia Jenerali Haider Fadhil wa jeshi la Iraq anasema askari wake wakisaidiwa kwa karibu na mashambilizi ya angani ya Marekani, wanaendelea kusonga mbele na kusafisha maeneo ya mji mkongwe wa mkoa huo. Makamanda wa Iraq wanaamini kuwa mamia ya wapiganaji wa IS bado wako kwenye vitongoji na wanazitumia familia zao – wakiwemo wanawake na watoto – kama ngao za binaadamu.

Mosul, mji wa pili kwa ukubwa, ulianguka mikononi mwa IS mwaka wa 2014, wakati kundi hilo lilifanya mashambulizi ya kasi kaskazini magharibi mwa Iraq na kutangaza ukhalifa katika mipaka iliyodhibitiwa na wanamgambo wa itikadi kali nchini Iraq na Syria. Hapo jana, wanajeshi wa Iraq walisherehekea mafanikio hayo ya karibuni, ijapokuwa Waziri Mkuu Haider al-Abadi hakutangaza ushindi wa moja kwa moja wa kuukomboa mji huo.

Al-Abadi alizuru Mosul jana na kukutana na makamanda wake, akawabusu watoto na kufungua upya soko moja la mjini humo. "Wapiganaji wa IS wamechagua kuzingirwa kwa sababu walipewa nafasi mbili, wasalimu amri ama wauawe. Wengi wao walichagua kufa, hawakutaka kujisalimisha isipokuwa idadi ndogo lakini wengine waliauwa.

Irak Mossul Rückeroberung Besuch Premier Al-Abadi (picture-alliance/Zuma/ Iraqi Prime Ministery)

Waziri Mkuu wa Iraq Haider al-Abadi alifika mjini Mosul kuwapongeza wanajeshi wake

Wapiganaji wengi wa IS mjini Mosul wameuawa na tumebakia na wachache. Nnawapa nafasi askari wetu shupavu wakamilishe operesheni hii ili tuweze kutangaza ushindi haraka, Mungu akipenda".

Lakini wakati hayo yakiendelea, mashambulizi ya angani na milio ya risasi za walenga shabaha iliendelea kurindima katika baadhi ya maeneo. Jeshi la Iraq lilizindua operesheni ya kuukomboa Mosul Oktoba mwaka jana na kufikia mwishoni mwa Januari, nusu ya upande wa mashariki wa mji huo – ambao Mto Tigris unapita katikati ya upande wa magharibi na mashariki – ikatangazwa kukombolewa.

Harakati za kuingia upande wa magharibi mwa Mosul zilianza mwezi uliofuata na kufikia Juni, wanajeshi wa Iraq walianza mapambano ya wiki nzima ya kuingia katika mji Mkongwe ambao ndio wenye idadi kubwa kabisa ya watu Mosul.

Makabiliano makali ya Mosul yamesababisha vifo vya maelfu ya watu na kuwaacha wengine karibu laki nane bila makaazi. Mwezi uliopita, wakati jeshi la Iraq lilipoingia katika Mji Mkongwe, wanamgambo waliharibu Msikiti wa kale wa al-Nouri.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ni miongoni mwa viongozi wa kwanza wa dunia kutuma salamu za pongezi. Waziri wa Ulinzi wa Uingereza Michael Fallon alimpongeza Abadi na jeshi la Iraq ambalo amesema limekuwa likipambana kwa ujasiri mkubwa. Umoja wa Ulaya uliutaja ushindi huo kuwa "hatua muhimu katika kampeni ya kuwaangamiza kabisaa magaidi katika maeneo ya Iraq”.

Mwandishi: Bruce Amani/AP
Mhariri: Iddi Ssessanga

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com