Je.Mashariki ya Ujerumani kuna neema ? | IDHAA YA KISWAHILI | DW | 04.11.2009
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

IDHAA YA KISWAHILI

Je.Mashariki ya Ujerumani kuna neema ?

Kansela Helmut Kohl,alietawala kipindi cha kuanguka ukuta wa Berlin na kuungana kwa nchi 2, aliahidi kuwa ,ile sehemu ya Mashariki ya Ujerumani, ingegeuka pepo ya neema ya maendeleo ya kiuchumi.

default

Kansela Helmut Kohl aliyetawala katika kipindi cha kuanguka ukuta wa Berlin

Utabiri wake huo, aliutoa haraka mno,kwani ,pepo na neema hiyo, haikuja haraka hivyo huko Ujerumani Mashariki.

Hivi sasa lakini,Ujerumani Mashariki na Magharibi, zimejongeleana kimaendeleo . Kwa kadiri gani basi ,mikoa mipya ya Mashariki mwa Ujerumani, imestawi kiuchumi mnamo miaka 20 tangu kuanguka UKUTA WA BERLIN ,ni mada ya taftishi mbali mbali zilizofanywa.

Uchunguzi uliochapishwa hivi punde, umetokana na Taasisi ya uchumi ya (IFO-INSTITUT). Taftishi za Taasisi hiyo, zimegundua kuwa maendeleo ya uchumi huko Mashariki mwa Ujerumani, hadi sasa hayaiwezeshi sehemu hiyo kusimama miguu miwili. Sehemu 1/5 ya mahitaji ya ndani ya Ujerumani Mashariki, yategemea msaada wa fedha kutoka serikali kuu ya shirikisho,msaada wa serikali za mikoa za magharibi na bima za kuwasaidia wanyonge.

Kabla ya uchunguzi wa IFO, HypoVereinsbank,ilichapisha uchunguzi wake: Njia ya kuelekea kustawi kwa uchumi huko Mashariki, ilikuwa na imesalia kuwa ngumu,lakini hatua kwa hatua , kuna maendeleo hapa na pale yanayomurika kile kilichotabiriwa "pepo ya neema ya maisha bora":

Pato jumla la kila mkaazi huko likichukuliwa kama kipimo,Poland imefikia 30% ya pato jumla la sehemu ya magharibi mwa Ujerumani.Mikoa ya mashariki ya Ujerumani,ingawa iko mbali zaidi kuliko Poland, kwa kima chao cha 71%,haikufikia hata thuluthi-nne ya pato jumla la kiuchumi la Magharibi mwa Ujerumani.Na hali ni hivyo,licha ya kutiwa jeki kwa mabilioni ya fedha kutoka magharibi mnamo miaka 20 iliopita.

Mjumbe wa Bodi ya HypoVereinsbank,Lutz Diederichs ,anatoa sababu nyingi zilizopelekea hali hiyo:

"Kumesalia matatizo makubwa. Viwanda vingi vimesalia mno kuwa vya kuseleleza nafasi za kazi tu.Ukosefu wa kazi nao kama hapo kabla, umesalia kupindukia kima cha wastani cha Magharibi mwa Ujerumani.Na tatizo lililoselelea, ni kuhama huko kwa wakaazi kuja magharibi.Na hii, inaharibu fursa za mustakbala mwema kwa mikoa hiyo mipya ya mashariki mwa Ujerumani."

Sehemu moja ambayo HypoVereinsbank limeonesha hamu nayo, ni benki ya kibinafsi,ambayo huko Ujerumani Mashariki ina wateja wengi wenye biashara za wastani. Hazina ya benki hiyo , katika msukosuko wa sasa wa uchumi,inatoa matumaini.Ni hapo ndipo maendeleo ya kiuchumi ya mikoa ya mashariki mwa Ujerumani tangu kuanguka kwa Ukuta wa Berlin, miaka 20 iliopita yalipo.

Bw.Diderichs anaongeza:

"Kwa maoni yetu,sehemu ya Mashariki ya Ujerumani, ina masharti mema kujipatia mafanikio endelevu.Na hii yatokana na sababu mbali mbali:Miundo mbinu huko ni ya kupigiwa mfano.Viwanda viliopo huko hivi sasa, vina uwezo wa kushindana katika masoko ya dunia. Mishahara kama hapo kabla, ni ya chini ukilinganisha na kima cha mishahara ya sehemu ya Magharibi.Na kuna msingi imara wa maendeleo ya kiviwanda."Alisema mjumbe huyo wa bodi kuu ya Vereinsbank, Lutz Diedrichs.

Mtayarishi: Ramadhan Ali

Mhariri: Abdulrahman

DW inapendekeza

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com