Jee Israel na Chama cha Hamas watasitisha kweli mapigano? | Matukio ya Kisiasa | DW | 18.06.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Jee Israel na Chama cha Hamas watasitisha kweli mapigano?

Israel inataka utulivu katika mpaka wake wa Kaskazini na Kusini

default

Rais wa Syria, Bashar al-Assad

Kupitia hatua mbili, Israel inataka utulivu katika mpaka wake wa kaskazini na kusini. Israel imeyakubali mapatano ya kusitisha mapigano na Chama cha Hamas katika Ukanda wa Gazi, mkunga wa makubaliano hayo ni Misri. Mapatano hayo yataanza kufanya kazi kesho, alhamisi. Pia Israel itafanya mazungumzo ya amani na Lebanon. Na pamoja na Syria, tayari kuna mashauriano yanayoendela chini kwa chini. Juhudi hizo zote zina faida gani?


Mtu anaweza kuyachukulia mapatano hayo ya kusitisha mapigano baina ya Israel na Chama cha Wapalastina cha Hamas kuwa ni kama tashtiti. Hadi yatakapoanza kufanya kazi hapo kesho asubuhi, bado pande hizo mbili zinaruhusiwa kutwangana. Baadhi ya wapiganaji wa Kipalastina walikitumia kipengee hicho na jana pia walifyetua maroketi walioyatengeneza wenyewe hadi kwenye ardhi ya Israel.


Kitendo hicho kilionesha mfano wa msingi unaolegalega wa juhudi za sasa za kutafuta utulivu na amani baina ya Israel na jirani zake wa Kiarabu. Nao upande wa Israel umeelemewa na hali ya kutokuwa na amani. Pia haijulikani kwa muda gani waziri mkuu wa nchi hiyo, Ehud Olmert, anayekabiliana na tuhuma za ulaji rushwa, ataweza kubakia madarakani. Hivi sasa mwanasiasa huyo anapigania uhai wake wa kisiasa. Lakini ukilinganisha na matatizo baina ya Israel na wapalastina, yale baina ya nchi hiyo ya kiyahudi na Syria au na Lebanon ni magumu zaidi kuweza kutanzuliwa kwa muda mfupi. Zaidi ni kwamba umaarufu wa Ehud Olmert miongoni mwa wananchi wa Israel, hasa kutokana na siasa zake hizi za kutafuta amani, unapungua. Katika miezi iliopita,idadi imepungua ya wananchi wa Israel wanaokubali kufanyika mapatano na Hamas au kuiachilia Milima ya Golan iliotekwa kutoka Syria mwaka 1967.


Mapatano ya kusitisha mapigano baina ya Israel na Hamas ambayo yamesimamiwa na Misri yamewaimarisha wazi wazi Waislamu wenye siasa kali wa Chama cha Hamas na ambao walikuwa wametengwa, na kwa hivyo kichinichini yamekidhoofisha Chama cha Fatah cha rais wa Wapalastina, Mahmud Abbas. Kama kweli pande mbili hizo zitaweza na zitataka kuyatekeleza mapatano hayo itaoonekana mnamo siku zijazo. Kuna taswira mbili zitakazojitokeza: Moja ni kwamba Chama cha Hamas kinaweza kuyatumia mapatano hayo ya kusitisha mapigano na kufunguliwa kwa sehemu mpaka wa Gaza kwa ajili ya kujizatiti zaidi kijeshi na kuyaachia makundi mengine ya kisilaha yaendelee na harakati zao. Pili ni kwamba kwa mapatano haya, Hamas inaweza ikahisi hii ni nafasi ya kubeba dhamana ya kisiasa ya kikweli juu ya mustakbali wa watu katika Ukanda wa Gaza, na hatua kwa hatua kujikwamua kutokana na hali ya kutengwa, kimataifa. Kuhusu taswira hii ya pili ni wakati utakaoamua. Ukweli wa mambo ni kwamba utaratibu wowote wa amani baina ya Israel na Wapalastina hautakuwa na nafasi bila ya kuwemo Chama cha Hamas.


Na hata kama yatakuja mazungumzo ya amani baina ya Israel na Lebanon, jambo hilo halitakuwa rahisi, sio tu kutokana na masuala magumu ya ardhi, lakini kutokana na makambi makubwa ya wakimbizi wa Kipalastina yalioko Lebanon, ambayo yatatia munda mapatano yeyote ya amani ya kipekee. Na mambo ni magumu sasa katika kuundwa serekali itakayokuwa na mawaziri wanaoelemea nchi za Magharibi na wale wanaoipendelea Syria. Hamna mwanasiasa yeyote kati ya wale wanaobishana huko Lebanon atakayeruhusu kuiregezea kamba Israel; hiyo itakuwa sawa na kujivua madaraka katika siasa za ndani za nchi hiyo. Chama cha Hizbullah ambacho kinashiriki katika serekali mpya kinaona ni halali kabisa kwake kuendeleza mapambano ya kijeshi dhidi ya Israel.


Matarajio yamebakia pindi mazungumzo ya amani yanayoendeshwa sasa kichini chini baina ya Israel na Syria yatafanikiwa. na hadi kufikia jambo hilo kuna njia ndefu mbele yetu. Lakini hata hivyo, kuna ishara kwamba Rais Bashir al-Asad anataka kufungua milango ya nchi yake na kuacha kuigemea Iran. Lakini Bashir al-Asad anajulikana kuwa ni taabu kumtabiri na mjanja. Kuuwa na mkataba wa amani na Israel, atataka pia Marekani ilipie, kwa mfano nchi yake ipatiwe msaada wa kiuchumi au dhamana kwamba utawala wake utabakia.
 • Tarehe 18.06.2008
 • Mwandishi Othman, Miraji
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/EMP2
 • Tarehe 18.06.2008
 • Mwandishi Othman, Miraji
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/EMP2
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com