1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je vita vya Korea Kaskazini vyanukia

Saumu Mwasimba
28 Aprili 2017

Marekani ikiionya Korea Kaskazini kutoijaribu Kijeshi,utawala wa Korea Kaskazini nao unajibu mapigo kwa jeuri kubwa

https://p.dw.com/p/2c68U
Nordkorea Militärparade
Picha: Reuters/KCNA

Kuongezwa kwa wanajeshi, majibizano ya maneno ya vitisho na kitisho cha vita vya kinyuklia yanazidi kuongeza wasiwasi kaskazini mashariki mwa Asia.

Marekani, kwa upande mmoja, inaimarisha juhudi zake katika eneo la kimkakati na Korea Kaskazini haionekani kusalimu amri wakati diplomasia na juhudi za kuzuia shambulio la nyuklia zikigongana. Kimsingi kunashuhudiwa wingu zito limeifunika rasi hiyo ya Korea.

Ikiwa ni kauli za jeuri na  kujiamini zinazotolewa na serikali ya Korea Kaskazini au upepo wa kishindo unaovuma upande wa Trump au majaribio ya kawaida ya makombora na mazoezi ya kijeshi, yote yanasababisha wasiwasi kote ulimwenguni huku hali ikionesha dalili za mambo kuelekea kufikia katika kiwango kibaya.

Ubabe wa Marekani unapojaribiwa

Makamu wa Rais wa Marekani, Mike Pence, alitowa hotuba yake wiki iliyopita akiwa katika ndege ya USS ambayo ilitumiwa na Ronald Reagan huko Japan na kusema kwamba upanga umeshawekwa tayari.

USA Donald Trump
Picha: Getty Images/AFP/Brendan Smialowski

Kauli hiyo imeonekana moja kwa moja kulenga kuionya Korea Kaskazini kutothubutu kuijaribu Marekani kijeshi akiongeza kusema kwamba "Marekani itajibu kwa kutumia nguvu kubwa ikiwa itashambuliwa."

Siku chache baadaye, katika hatua za kujibu mazoezi ya kijeshi ya wanamaji kati ya Marekani na Japan, gazeti rasmi la serikali Korea Kaskazini la Rodong Sinmun likaandika kwamba vikosi vya kimapinduzi viko tayari kuizamisha meli ya kubeba ndege za kijeshi za Marekani inayoendeshwa kwa nguvu za kyuklia kwa kombora moja tu.

Na hiyo ni baada ya kuripotiwa kwamba meli hiyo ya Marekani ya kundi la USS Carl Vinson itatia nanga  katika bahari ya pwani ya Rasi ya Korea, Korea Kaskazini ilijibu kwa kusema kwamba kupelekwa kwa zana hizo ni kitendo cha hatari kabisa kinachofanywa na wale wanaopanga kuanzisha vita vya nyuklia.

Kikosi hicho cha Vinson kitaungana na USS Michigan, nyambizi iliyosheheni makombora aina ya 144 Tomahawk ambayo ilishawasili katika bandari ya Korea Kusini ya Busan tangu Jumanne wiki hii.

Hali isiyoweza kupuuzwa

Hata hivyo, hadi wakati huu wasiwasi uliopo haujafikia kiwango cha kubadili mambo yalivyo ingawa kuna kitisho kinachozidi kuongezeka katika kanda hiyo ambacho hakiwezi kupuuzwa.

Uwezo wa jeshi la Korea Kaskazini unazidi kuimarika na hakuna ishara yoyote inayoonesha kwamba utawala huo utabadili msimamo wake wa jazba na mabavu, ambao kimsingi unauona ni muhimu kwao na unaostahili kuwepo kwa ajili ya kuuwezesha  kuendelea kuwepo.

USA China Spionage Stealth Fighter F 22
Picha: LEE JIN-MAN/AFP/Getty Images

Wiki hii pia, nchi hiyo ilionesha nguvu zake za kijeshi wakati ikiadhimisha miaka 85 tangu kuasisiwa jeshi la nchi hiyo ambapo zana nzito nzito zilioneshwa.

Kwa mujibu wa shirika rasmi la habari la Korea Kaskazini, KCNA, hilo lilikuwa ni tukio kubwa kuwahi kufanyika la maonesho ya nguvu za kijeshi likihusisha mizinga na makombora ya masafa marefu 300 pamoja na nyambizi zinazoweza kutumiwa katika kushambulia meli za kivita.

KCNA halikuishia hapo tu, bali lilikwenda mbali zaidi na kuandika kwamba mazoezi hayo ya kijeshi yameonesha ni kwa jinsi gani Korea Kaskazini ina uwezo wa kuwamiminia mvua ya makombora bila hesabu wale lililowaita ''mabeberu'' yaani Marekani na "wafuasi wao wachafu."

Mwandishi:Saumu Mwasimba/DW English

Mhariri: Mohammed Khelef