Je Umoja wa Mataifa una nguvu kiasi gani Mashariki ya Kati? | Matukio ya Kisiasa | DW | 09.01.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Je Umoja wa Mataifa una nguvu kiasi gani Mashariki ya Kati?

Azimio jipya la Umoja wa Mataifa halitaleta mabadiliko yoyote

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon (kushoto) na waziri wa mashauri ya kigeni wa Misri, Ahmed Aboul Gheit mjini New York Marekani

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon (kushoto) na waziri wa mashauri ya kigeni wa Misri, Ahmed Aboul Gheit mjini New York Marekani

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limepitisha azimio kuhusu vita katika Ukanda wa Gaza kwenye mkutano wake uliofanyika jana mjini New York, Marekani. Azimio hilo linaitaka Israel iondoke kutoka eneo la Gaza. Je azimio hili jipya la Umoja wa Mataifa kuhusu mzozo wa Gaza linaweza kuzaa matunda?

Katika azimio jipya lililopitishwa na baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, Israel na Hamas zimetakiwa kusitisha mapigano mara moja. Israel imetakiwa iondoe vikosi vyake kutoka Ukanda wa Gaza na kufungua mipaka ya ukanda huo. Kundi la Hamas, kwa upande wake, limetakiwa likomeshe uingizaji silaha katika Gaza.

Kwa takriban majuma mawili baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limekuwa likitaka azimio la kusitisha mapigano huko Gaza na limepitisha azimio hilo kwa kura 14 huku Marekani pekee ikisita kupiga kura yake kuliunga mkono azimio hilo.

Mpatanishi mkuu wa Israel anataka kuona azimio jipya. Kimsingi inafaa kuwa na azimio, lakini ipo haja ya kusubiri iwapo mazungumzo yanayofanyika mjini Cairo Misri yatakuwa na matokeo ambapo wapatanishi wa Misri, Israel na Palestina wanazungumzia uwezekano wa usitishwaji wa mapigano.

Tatizo moja kwenye mazungumzo ya baraza la usalama ni kwamba kwanza kabisa nchi za kiarabu zikiwakilishwa na Libya zilitaka azimio lenye mafungamano wakati ambapo wanachama wengine wa baraza la usalama hasa Marekani walitaka azimio la pamoja la kudumu.

Baada ya mashambulizi makali dhidi ya Ukanda wa Gaza katika siku zilizopita, wakati umewadia kwa Marekani kuachana na msimamo wake wa kutotaka kuwa na mafungamano na izungumze wazi. Angalau iliachie huru baraza la usalama lizungumze wazi.

Lakini ni matokeo gani yaliyotokea? Matokeo kutoka eneo la mapigano ni jibu la wazi kabisa. Wanajeshi wa Israel na wapiganaji wa Hamas wanaendelea na vita kana kwamba hakuna chochote kilichotokea.

Kwa bahati mbaya kuna utamaduni kuhusu maazimio katika Mashariki ya Kati: Orodha ya maazimio ya Umoja wa Mataifa ni ndefu kama orodha ya mashambulio yaliyotokea huko. Na ikiwa maazimio ya aina hiyo yalifuatwa basi kwa kiwango kikubwa ni wakati upande mmoja sana sana Israel ulipoamini umeyafikia malengo yake au wakati ambapo pande zote mbili zilisitisha mapigano kutokana na uchovu.

Historia hii ya maazimio ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa yasiyoleta manufaa ni ishara ya udhaifu kwa shirika hilo la kimataifa na jumuiya nzima ya kimataifa. Kwamba miungano midogo kama Umoja wa Ulaya au jumuiya ya nchi za kiarabu haina ushawishi tayari ni jambo la kuvunja moyo. Lakini hata Umoja wa Mataifa nao washindwa?

Na sasa azimio hili lenye mafungamano lina maana gani? Kuwa na mafungamano inawezekana tu ikiwa maazimio mengine ya awali ambayo hayakutekelezwa yatafufuliwa. Lakini hali haiko hivyo. Makundi kama Hamas hunufaika kutokana na mzozo kati yake na Israel. Kundi la Hamas haliwakilishi taifa lolote na miaka miwili iliyopita imedhihirisha wazi kabisa kwamba vikwazo vinavyowekewa kundi hilo karibu vyote vina makosa. Hali inayoendelea hivi sasa inawahusu raia wa Gaza.

Israel bado haijawahi kuwa na hofu ya kuwekewa vikwazo na kwa hiyo hata wakati huu haina haja ya kuwa na wasiwasi wowote.

Mpatanishi rasmi wa Israel anashikilia kwamba vikosi vya Israel vina motisha wa kupigana na jamii yake inakataza Israel kuwekwa katika kiwango sawa na makundi kama vile Hamas. Israel kila mara inapingana na sheria za kimataifa na kwa hiyo maazimio ya Umoja wa Mataifa yasiyo na matokeo yoyote yataleta mabadiliko madogo sana huko Mashariki ya Kati.

 • Tarehe 09.01.2009
 • Mwandishi Charo Josephat
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/GVFj
 • Tarehe 09.01.2009
 • Mwandishi Charo Josephat
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/GVFj
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com