1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je, ndio machweo ya chama kikongwe Tanzania?

1 Agosti 2013

Watanzania wanataka kutunga katiba itakayoongoza nchi yao bila kuwepo haja ya kufanya marekebisho. Lakini baadhi ya wanasiasa wanasemekana kuwa wameanza kampeni kutafuta nafasi za uongozi bila idhini.

https://p.dw.com/p/19IRs
Bendera ya Tanzania
Bendera ya TanzaniaPicha: Roberto Schmidt/AFP/Getty Images

Lakini suala kubwa katika vichwa vya raia ni kama sheria mama ya nchi inayoandaliwa sasa italeta mabadiliko bora zaidi au itaiweka nchi katika kibano cha watu wasiopenda mabadiliko, ambao tayari wameanza kutamka kuwa wanapinga mabadiliko yaliyo katika rasimu ya katiba.

Chama cha Mapinduzi (CCM) kinaonekana kuwa bado ni maarufu katika baadhi ya jamii na kinapendwa kiendelee kutawala angalau kwa mwongo mmoja zaidi, lakini ukweli ni kwamba wimbi la upinzani kuhusu pingamizi zake kwa mawazo mapya linainuka zaidi. Hapana shaka hakiwezi kutawala milele.

Mfuasi wa CCM Zanzibar
Mfuasi wa CCM ZanzibarPicha: picture alliance/dpa


Muda, nyenzo, fedha na raslimali watu mara nyingi vimekuwa haba kuwawezesha Watanzania watekeleze mipango na malengo yao kwa ukamilifu.

Kwa mfano, takwimu za watu zilizopo sasa ni makadirio yaliyotokana na sensa ambayo haikukamilika ya mwaka 2012 ambayo iliacha wakazi wa maeneo yasiyofikika kwa urahisi bila kurekodiwa katika orodha za makarani wa sensa.

Sababu hiyo hiyo ya kutofikika kwa maeneo hayo bado ni kikwazo katika harakati za sasa ambazo zinahitaji wananchi wote washiriki kikamilifu, ikiwa pamoja na utoaji wa maoni yao katika maboresho ya rasimu ya katiba mpya.

Kutunga katiba upya na kuandaa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 ni shughuli za gharama kubwa na hapana budi zikamilishwe katika kipindi cha miaka miwili kwa kuzingatia haki kwa raia wote na kwa njia ya kidemokrasia.

CCM yaamini itashinda 2015

Kweli Tanzania imefika mahali pagumu katika historia yake. Watu wake lazima wauthibitishie ulimwengu kwamba bado wameungana na wanauenzi muungano wa karibu nusu karne kati ya Bara, eneo ambalo lilijulikana kama Tanganyika, na Visiwa vya Zanzibar, hasa ya mawazo tofauti kuhusu siku zijazo za muungano baada ya kutangazwa kwa rasimu ya katiba.

Huo ni upande mmoja wa hali ya kisiasa katika nchi hii ya Julius Kambarage Nyerere na Abeid Amani Karume, waasisi wa taifa la Tanzania. Upande mwingine, ingawa hakuna hakika ya nani atakuwa mshindi katika kura ya maoni juu ya katiba mpya, kila chama cha siasa na washabiki wake wanachukua tahadhari wasije wakajiangamiza wenyewe kwa jinsi wanavyoendelea na harakati za sasa.

Rais wa kwanza wa Tanzania, Julius Nyerere
Rais wa kwanza wa Tanzania, Julius NyererePicha: Getty Images/AFP

Matokeo ya katiba mpya huenda yakawa na athari kwa maendeleo yao katika uwanja wa siasa, lakini pia muonekano wao kama viongozi makini, wanaoaminika na wenye upeo mbele ya vijana ambao idadi yao inazidi kuongezeka.

CCM inaamini kuwa itaibuka na ushindi mkubwa 2015, lakini kama matokeo ya uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika hivi karibuni katika kata nne za jiji la Arusha ni kielelezo cha yajayo, basi chama kianze kufikiria kuachia ngazi kwa heshima.

Kwanini CCM inapinga serikali tatu?

Washindani wake wa karibu, CHADEMA na Chama cha Wananchi (CUF), wanakipa taswira ya kuwa kiko ukingoni mwa mteremko mkali – licha ya hayo yanayoelezwa kuwa "mafanikio ya CCM’" katika historia ya Tanzania.

Bendera ya chama cha upinzani CUF
Bendera ya chama cha upinzani CUFPicha: Mohammed Khelef

Upingaji wa sera za CCM uko zaidi miongoni mwa kizazi cha vijana ambao shauku zao zaidi ni kuhusu ajira, elimu ya utaalamu katika nyanja mbalimbali na ya ufundi stadi, uhuru wa kijamii na maisha bora kuliko musuala ya uwakilishi bungeni na katika serikali za mitaa.

Kwa mawazo yao, baadhi ya vijana wanasema, CCM ni chama cha watu wanaotafuta nafasi za kujinufaisha wao binafsi bila kujali watu wengine ; na watu ambao kila mara huzungumzia harakati za ukombozi wa Afrika wakati wao wanahitaji ukombozi wa kifikra.

Wadadisi wanauliza, kwa mfano, kwa nini CCM inapinga kuwepo kwa serikali tatu za Tanganyika, Zanzibar na Muungano ambao ndio mfumo unaotakiwa na raia wengi.
Wachambuzi wa kisiasa wanaongeza kuwa kukataa mfumo wa serikali tatu kama rasimu ya katiba inavyopendekeza ni kuhujumu Muungano wa Tanzania.

Wana wasiwasi kwamba huenda chama kina dondoo ya siri, lakini katika enzi hizi za uwazi, ni Watanzania wachache wanaweza kurubuniwa na chama ambacho kinaelekea kuishiwa ujanja wa kisiasa kuvutia watu wengi wakiunge mkono.

Mwandishi: Anaclet Rwegayura
Mhariri: Josephat Charo