1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je, Emmerson Mnangagwa kuwa rais wa pili wa Zimbabwe?

16 Novemba 2017

Nchini Zimbabwe, baadhi ya waangalizi wamemtaja makamu wa rais wa zamani Mnangagwa kuwa ndiye mwenye nafasi kubwa ya kuchukua uongozi kutoka kwa Robert Mugabe.

https://p.dw.com/p/2nkk6
Emmerson Mnangagwa Politiker aus Simbabwe
Picha: Getty Images/AFP/A. Joe

Mugabe na Mnangagwa wamekuwa wakipatana na kuhasimiana kwa miaka mingi huku Mugabe akimtimua makamu wake wiki moja iliopita. Je Mnangagwa ana nafasi ya kurudi?

Machoni mwa wazimbwabwe wengi, aliyekuwa makamu wa rais Emmerson Mnangagwa anaonekana kuwa kiongozi wa nchi mtarajiwa. Mnangagwa mwenye umri wa miaka 75 amekuwa na mchango mkubwa wa kisiasa kwa miaka mingi, akiwa kama mtu aliyekuwa kwenye kivuli cha Mugabe wakati wote ingawa baadhi ya wakati wakivutana.

"Mnangagwa amekuwa upande wa Mugabe kwa miaka 50.  Derek Matyszak, mchambuzi na taasisi ya mafunzo ya usalama (ISS) nchini Afrika Kusini aliiambiwa DW, "Alikuwa ni mtu wa Chanda na pete na kiongozi huyo.

Mamba

Nchini Zimbabwe, Mnangagwa anafahamika kwa jina la utani "mamba” kutokana na ukatili na usiri alionao.

Kama Mugabe, alipata sifa  kama mwanaharakati wa kisiasa wakati wa mapigano ya miaka mingi dhidi ya utawala wa wazungu wachache katika nchi yake, kisha ukoloni wa Uingereza ya Kusini mwa Rhodesia.

Mnangagwa alijiunga na chama cha Zimbabwe African National Union (ZANU) katika kupambana na serikali ya waziri Mkuu wa zamani wa Ian Smith. Chama cha ukombozi ZANU baadaye kiligeuka kuwa chama tawala cha Zimbabwe -ZANU-PF .

Mnamo mwaka wa 1965, Smith alikuwa ametangaza uhuru wa Rhodesia kutoka Uingereza na kuanzisha mfumo wa utawala wa wazungu wachache. Mnangagwa, ambaye alipata mafunzo ya kijeshi nchini Misri na China, aliongoza kundi la wapiganaji wakiitwa Kundi la Mamba ambalo lilifanya vitendo vya hujuma dhidi  ya serikali ya Smith.

Mnangagwa alikamatwa mwaka 1965 na kuhukumiwa kifo, lakini hukumu yake ilibatilishwa kuwa kifungo cha miaka 10 jela kutokana na umri wake mdogo. Baadaye alitumia muda wa ziada gerezani, wakati mwengine akiwa chumba kimoja na Mugabe jela.

Emmerson Mnangagwa und Robert Mugabe in Simbabwe
Picha: picture alliance/dpa/AP Photo/T. Mukwazhi

Mnangagwa aliendelea kujifunza sheria katika nchi jirani ya Zambia. Baada ya nchi yake kupata uhuru rasmi kama Zimbabwe mwaka 1980, alichaguliwa kuwa waziri wa usalama wa taifa, kisha akahudumu kama waziri wa fedha na waziri wa ulinzi, pamoja na msemaji wa bunge.

 

Maarufu kwa ukandamizaji wa matumizi ya nguvu

Alitajwa kuwa ni mtu katili alipokiongoza kikosi kilichopewa mafunzo na Korea kaskazini  kilichojulikana kama kikosi cha tano kilichoitwa "Gukurahundi" na kuwaandama wapinzani kutoka kabila la wachache la Ndebele. Inakadiriwa watu 20,000 waliuawa.

"Mnangagwa anaonekana kuwa mtu ukatili sana, mjanja na watu wanamtazama kwa uwoga na tahadhari," mchambuzi wa ISS Matyszak alisema kuhusu makamu huyo wa zamani.

"Kwa hakika sio mtu wa kidemokrasia. Watu hawapaswi kuwa na wazo kwamba Mugabe anaweza kurithiwa na mtu mwenye sifa nzuri za kidemokrasia."

Katika miaka ya awali, makamu huyo wa rais wa zamani alikuwa ameonekana kama mrithi wa Mugabe, lakini aliondolewa kutoka  nafasi yake kama katibu wa utawala wa ZANU PF mwaka 2004.

Baada ya kutokuwa na wadhfa wowote chamani, miaka mine baadaye, Mugabe alimrudisha Mnangagwa  kuwa mkuu wa kampeni yake ya uchaguzi wa rais alipoamua kugombea tena.

Emmerson Mnangagwa und Robert Mugabe in Simbabwe
Picha: Getty Images/AFP/J. Njikizana

Baada ya uchaguzi, Mnangagwa alilengwa na vikwazo vya Marekani na Umoja wa Ulaya na kulaumiwa na makundi ya haki za binadamu kwa kuongoza ukandamizaji wa kikatili  dhidi ya wapinzani, lakini aliendelea kupendelewa na kuchukua nafasi nzuri ndani ya serikali ya Mugabe.

Uhusiano wa Mugabe na Mnangagwa

Kulingana na mchambuzi Matyszak, "uhusiano wa Mugabe na Mnangagwa uiionekana kama wa maslahi ya pamoja kuliko urafiki."

Mnamo mwaka wa 2014, aliteuliwa  mahala pa aliyekuwa makamu wa rais Joyce Mujuru na alionekana tena kama mrithi wa Mugabe.

Uhusiano kati ya Mugabe na Mnangagwa uligeuka na kuwa shubiri baada ya Mnagangwa na mkewe Mugabe Grace walipojikuta katika mvutano mkali juu ya nani angepaswa kumrithi rais Mugabe.

Grace Mugabe alimshawishi mumewe kuwa Mnangagwa alijaribu kumpindua. Wafuasi wa Mnangagwa kwa upande wao walimshutumu Bibi Mugabe kwamba alitaka kumuua kwa sumu.

Mnamo novemba 6 Mugabe alimtimua Mnangangwa kama makamu wa rais.

Baada ya shoka hilo, Mnangagwa alimjibu Mugabe akimwambia kuwa "chama tawala cha Zanu PF si  mali yako na mkeo kama unavyopenda." Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari, baada ya kuondolewa umakamu wa rais  Mnangagwa alikimbilia nchi Jirani ya Afrika Kusini, ingawa hajulikani aliko.

Mwandishi: Fathiya Omar/Daniel Pelz/DW

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman