Japan yakata tiketi ya kwanza ya Kombe la dunia 2010 | Michezo | DW | 08.06.2009
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Japan yakata tiketi ya kwanza ya Kombe la dunia 2010

Kombe la mashirikisho kuanza Afrika kusini jumapili ijayo:

Rais wa FIFA na Mbeki(Rais wa zamani Afr.kusini)

Rais wa FIFA na Mbeki(Rais wa zamani Afr.kusini)

-Uwanja mpya wa dimba uliojengwa na Afrika Kusini kwa Kombe lijalo la dunia, ulifunguliwa rasmi jana huko Port Elizabeth-wiki kabla Kombe la mashirikisho-Confederations kuanza.

-Japan ni timu ya kwanza kukata tiketi yake kwa kombe lijalo la dunia 2010 nchini Afrika Kusini -

- Brazil imekomea Uruguay mabao 4:0 kanda ya Amerika kusini wakati kanda ya Afrika, Nigeria yaizaba Harambee Stars-Kenya mabao 3-0 mjini Abuja. Simba wa nyika Kamerun watoka suluhu na simba wa Atlas -Morocco mjini Yaounde.

Katika kinyanganyiro cha kuania tiketi za Kombe lijalo la dunia , mwishoni mwa wiki kanda mbali mbali duniani-wiki kabla kombe la mashirikisho litakalojumuisha mabingwa wa dunia-Itali,mabingwa wa Amerika Kusini Brazil na mabingwa wa Ulaya Spain kuanza nchini Afrika Kusini,Japan imeapa kuangusha majabali katika Kombe lijalo la dunia baada ya kuibuka timu ya kwanza kabisa ulimwenguni kukata tiketi yake ya kwenda Afrika kusini Juni mwakani. Japan iliizaba Uzbekhistan bao 1-0 hapo jumamosi n a kutia mfukoni tiketi yake.

Kurasa za mbele za magazeti ya jana ya Japan, zilisheheni vichwa vya habari vikipongeza kufuzu kwa Japan kwa mara ya 4 mfululizo kucheza finali ya Kombe la dunia.Shabaha ya Samurai hao sasa ni kuwasili alao nusu-finali ya Kombe la dunia huko Afrika kusini. Sifa zinakwenda kwa kocha wa Japan, Takeshi Okada, alieiongoza Japan katika Kombe la dunia Ufaransa,1998 ilipotolewa bila ushindi wowote.

Ikiwa chini ya kocha mfaransa PhilippeTroussier, Japan ,iliwasili duru ya pili ya Kombe la dunia mwaka 2002 kombe lilipochezwa nyumbani kwa ubia na Korea ya Kusini.Katika Kombe lililopita la dunia hapa Ujerumani 2006 na chini ya uongozi wa mbrazil Zico, Japan ilipigwa kumbo katika duru ya kwanza .

Sasa kwa muujibu wa FIFA,Australia na japan kutoka kundi la kwanza kanda ya Asia na Korea ya Kusini katika kundi la pili,zimekuwa timu za kwanza kutia mfukoni tiketi zao za Kombe la dunia 2010 huko Afrika kusini.

Ama mabingwa mara kadhaa Brazil, walitamba nyumbani walipoikomea Uruguay, mabingwa wa kwanza kabisa wa dunia, mabao 4-0.Mahasimu wao wakubwa Argentina,wakiongozwa na kocha Diego Maradona, walishinda nao nyumbani ingawa kwa bao 1:0 dhidi ya Columbia.Matokeo hayo yanaiweka Brazil na Paraguay kileleni mwa ngazi ya kanda ya Amerika kusini huku Argentina ikiwa nyuma yao.Changamoto nyengine katika kanda hiyo zilimalizika hivi: Venezuela waliitandika Bolivia bao 1-0 mjini La Paz na hii imefufua matumaini yao ya kwenda Afrika kusini Juni mwakani.

Katika kanda ya Afrika, hakuna timu mbali na wenyeji Bafana Bafana, iliotia tayari mfukoni tiketi yake ya Kombe la dunia :Mounira Mohammed atufunulia kawa mambo yalivyo mezani:

Super Eagles-Nigeria, ikiwa na kiu cha kwenda Afrika Kusini mwakani hawakuwa na huruma na Harambee Stars-Kenya. Wakitamba nyumbani Abuja, Nigeria waliikomea Kenya mabao 3 bila majibu.Mabao 2 ya Ikechukwu na moja la Obinna Nsofor,yalipiga msumari mwengine katika jeneza la Kenya nje ya Kombe lijalo la dunia .Macho yalikodolewa mpambano kati ya simba 2-simba wa nyika Kamerun na simba wa milima ya Atlas-Morocco.Ugomvi wao mwishoe ulimalizwa kwa suluhu (0:0) mjini yaounde.katika mpambano mwengine wa kundi hili A, gabon iliikomea Togo mabao 3:0 na sasa ndio inayoongoza kundi hili kanda ya Afrika.Kamerun inaburura mkia wa kundi hili pamoja na Morocco.

Changamoto za kundi C baina ya wenyeji Algeria na mabingwa wa Afrika Misri, ilimalizika kwa ushindi wa mabao 3:1 wa Algeria.Zambia au Chipolopolo walifyatua risasi zao na kuilaza Ruanda bao 1:0.sasa Zambia iko nyuma ya Algeria inayoongoza kundi hili.

Mjini bamako,wenyeji mali walichezeshwa kindumbwendumbwe na waghana "Black Stars".Mabao ya Asamoah mnamo dakika ya 67 ya mchezo na Matthew Amoah dakika ya 77,yalitosha kuwatupa Mali mkiani mwa kundi hili.Ghana inaongoza ikifuatwa na Benin na Sudan.

Huko Conackry, Guinea, ilikanyagwa na Tembo wa Ivory Coast kwa mabao 2:1 na sasa tembo wanaongoza kundi hili E wakifuatwa na Burkina Faso.Malawi inaburura mkia pamoja na Guinea.

Timu zinazoibuka juu nafasi ya kwanza katika kila kundi zakata moja kwa moja tiketi zao kwa Kombe lijalo la dunia huko Afrika kusini pamoja na wenyeji Bafana bafana ambao mwishoni mwa wiki walitamba kwa bao 1:0 mbele ya Poland katika dimba la kirafiki.

Kombe la mashrikisho-Confederations Cup :

Wiki kabla ya firimbi kulia kuanzisha kombe la mashirikisho-Confederations Cup-kombe linalofungua pazia la kombe lijalo la dunia Juni,mwakani, Uwanja mpya uliojengwa mahsusi kwa Kombe jilo-uwanja wa Port Elizabeth.

Mechi 8 pamoja na mapambano ya robo-finali zitachezwa katika uwanja huo.Pia mpambano wa kutafuta timu ya 3 na ya 4 utachezwa hapo.Uwanja wa Port Elizabeth ,unachukua hadi mashabiki 48,000.

Kombe la mashirikisho linalofungua pazia la Kombe la 2010 la kwanza barani Afrika litachezwa kuanzia Jumapili ijayo huko Johannesberg,Pretoria,Bloemfontein na Rustenburg.

Miongoni mwa timu zinazoania kombe hilo mbali na timu 2 za Afrika-mabingwa Misri na wenyeji Afrika Kusini, ni mabingwa wa dunia-Itali, mabingwa wa Amerika kusini-Brazil na mabingwa wa Ulaya Spian.Isitoshe, New Zealand itawakilisha kanda ya Oceania wakati Marekani ile ya Amerika kaskazini.

Dimba la Confederations Cup Jumapili ijayo, litafunguliwa na wenyeji Bafana bafana-Afrika Kusini na mabingwa wa kusangaza wa bara la Asia-Iraq.Brazil wenye miadi na mabingwa wa dunia-Italy, wanaania kombe hili wakiwa mabingwa wa Amerika kusini waliitimua Argentina kwa mabao 4-1 katika finali ya kombe hili hapa Ujerumani kabla Kombe la dunia mwaka mmoja baadae.Katika kundi lao B pia kuna Marekani.Brazil itafungua dimba na Misri siku 1 baadae-Jumatatu ijayo huko Bloemfontein.Itali inaanza na Marekani siku hiyo hiyo mjini Pretoria.

Timu 2 zitakazoibuka juu ya kila kundi zaingia nusu-finali na finali itakuwa Juni 28.Mastadi wa dimba kama vile Kaka,Robinho wa Brazil, Fernando Torres,Fabregas wa Spian; Fabio Cannavaro na Daniele De Rossi wa Itali watakuwa miongoni mwa wale watakaokodolewa macho huko Afrika kusini. Kwa ufupi homa ya kombe la dunia itaanza hasa jumapili ijayo-nasi tutakuwa nawe viwanjani.

Muandishi: Ramadhan Ali/DPAE

Mhariri: M.Abdul-Rahman