Japan mwaka mmoja baada ya Fukushima | Matukio ya Kisiasa | DW | 11.03.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Japan mwaka mmoja baada ya Fukushima

Mwaka mmoja baada ya ajali kutokea kwenye kinu cha nyuklia cha Fukushima nchini Japan, swali linalozuka ni je, umeme unaohitajiwa na nchi hiyo iliyositawi kiviwanda utatoka wapi katika siku zijazo?

Fukushima

Fukushima

Inashangaza kuona kwamba nchini Japan kila kitu kinakwenda sawa licha ya kwamba sehemu ndogo tu ya umeme wa nguvu ya nyuklia iliyokuwa inatumika zamani ndio inayotumika hivi sasa. Kwa miongo mingi sana hakuna aliyefikiri kwamba Japan, ambayo ni nchi ya tatu kwa utajiri duniani, ingeweza kujimudu bila ya kuwa na umeme utokanao na nguvu ya nyuklia.

Lakini baada ya tsunami na tetemeko kuleta ajali ya Fukushima mwaka jana, vinu vya nyuklia 51 vilifungwa na sasa vimebaki vitatu tu vinavyotengeneza umeme wa nchi hiyo. Kabla ya hapo, asilimia 30 ya umeme unaotumika Japan ilikuwa inatokana na nguvu za nyuklia. Hadi kufikia April mwaka huu, serikali ya Japan inapanga kufunga vinu vyote vya nyuklia.

Japan itumie nishati gani?

Wajapan wakiandamana kupinga matumizi ya nyuklia

Wajapan wakiandamana kupinga matumizi ya nyuklia

Japan bado haina mpango kamili unaohusu nishati. Serikali, jamii na vikundi vinavyoshawishi wabunge bado havijajua ni njia gani waifuate. Bunge la Japan litapitisha maamuzi kuhusu kuendelea kutumia nishati ya nyuklia katikati ya mwaka. Waziri mkuu wa Japan, Yoshihiko Noda, anataka matumizi ya nguvu ya nishati ya nyuklia yapunguzwe na badala yake nishati mbadala zitumike. Lakini Naoto Kan, ambaye alikuwa waziri mkuu wa Japan kabla ya Noda, amesema kwamba Japan italazimika kuendelea kutumia nishati ya nyuklia hadi angalau kufikia mwaka 2030.

Kwa sasa makampuni ya umeme yanatumia zaidi umeme utokanao na makaa. Matumizi ya nishati hiyo ni ya gharama kubwa kwa wateja na pia yanaleta athari kwa mazingira. Inaelekea kwamba Japan haitaweza kutekeleza makubaliano ya mkataba wa Kyoto wa kulinda mazingira.

Nishati mbadala zaweza kuwa suluhisho

Nishati mbadala

Nishati mbadala

Japan bado haijafikia uamuzi kuhusu nishati mbadala inayoweza kutumika katika miaka ijayo. Upo mpango wa kujenga mitambo ya kutengeneza umeme kwa nguvu ya upepo karibu na pwani ya Fukushima. Hata hivyo haitarajiwi kwamba Japan ina uwezo wa kutengeneza umeme kwa kiasi kingi kama vile ilivyo Marekani au katika nchi za Ulaya. Sababu mojawapo ni vimbunga vinavyoikumba nchi hiyo kila mwaka. Nishati ya jua nayo haikubaliki sana kwa sababu ni ya ghali na kwa sababu Wajapan wanaona kwamba ni nishati ambayo haiwezi kutegemewa wakati wote.

Mbali na kuendeleza matumizi ya nishati mbadala, Japan pia imepanga kupunguza kabisa matumizi ya nishati. Ili kutekeleza mpango huo itabidi namna yq kufikiri ya Wajapan nayo ibadilike kwani wamezoe kutumia umeme kwa wingi kwa sababu inapatikana kwa bei rahisi. Matumizi makubwa ya umeme yanatokana na kuwepo kwa vifaa vingi vya elektroniki ambavyo vinahitaji umeme.

Mwandishi: Alexander Freund

Tafsiri: Elizabeth Shoo

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com