Jamhuri ya Ireland inasema HAPANA kwa Mkataba wa Lisbon | Matukio ya Kisiasa | DW | 17.06.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Jamhuri ya Ireland inasema HAPANA kwa Mkataba wa Lisbon

Wananchi wa Ireland kwa wingi wanasema hawautaki Mkataba wa Lisbon wa Jumuiya ya Ulaya.

Jose Manuel Barroso, rais wa Komisheni ya Umoja wa Ulaya

Jose Manuel Barroso, rais wa Komisheni ya Umoja wa Ulaya"Kura zilizopinga pendekezo ni 862,415"


Hayo ni matokeo ya kura ya maoni iliofanywa alhamisi iliopita ambapo wananchi wa Jamhuri ya Ireland, kwa wingi, walisema hawautaki mkataba wa Marekebisho wa Umoja wa Ulaya uliofikiwa Lisbon. Uamuzi huo ulikuwa mtetemeko mkubwa wa kisiasa hapa Ulaya, ambao athari zake zitabakia kwa muda mrefu.

Msingi wa kisheria wa mkataba huo uliochukuwa juhudi nyingi na muda mrefu kuufikia sasa unakosekana, kwani kuweza kuanza kufanya kazi hapo mwanzoni mwa mwakani ulitakiwa upewe kibali na nchi zote 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya. Mkataba huo unataka Umoja huo uwe na nguvu zaidi na taasisi zake ziwe za kidemokrasia zaidi. Sasa juhudu zinafanywa ili kunusuru kile kinachoweza kunusurika. Jee mkataba huo utawekwa kando? Jee Ireland itapewa muda wa kutafakari au kutakuwa na uwanachama wa tabaka mbili ndani ya Umoja huo? Hayo ndio masuali yanayowaumiza vichwa wanasiasa wa Ulaya, kama vile vichwa vyao vilipouma pale mwaka 2005 wananchi wa Ufaransa na Uholanzi waliikataa katiba ya Umoja wa Ulaya.


Matokeo hayo ya huko Dublin yalikuwa pigo la kibinafsi kwa waziri mkuu wa Jamhuri ya Ireland, Brian Cowen, aliyeingia madarakani mwezi mmoja tu iliopita:

"Matokeo haya yanaleta hali ya kutatanisha sana. Hakuna suluhisho la haraka, na si rahisi kuikiuka hali hiyo. Hatutochukuwa hatua ya haraka, tunahitaji kupumua ili kufahamu nini kilichotokea na kwanini. Tunahitaji kushauriana kwa utulivu nyumbani hapa na pamoja na washirika wetu wa Ulaya."

Magazeti ya Ireland yalisema kura hiyo ya HAPANA imekuja kwa vile serekali ya nchi hiyo ilikawia kuwashawishi wananchi juu ya faida za mkataba huo; wengi wa wananchi walihisi hawajaarifiwa vya kutosha, na zaidi ni kwamba watu wa nchi hiyo hawaridhiki na hali ya uchumi ilivyo na wanazidi kuwa na hofu wakiangalia mbele kwamba Umoja wa Ulaya unawaletea sheria nyingi zilizo ngumu na taasisi za umoja huo ziko mbali na wananchi.


Declan Ganley, mfanya biashara wa Ireland, na mtu aliyekuwa usoni kabisa akibeba biramu la kampeni ya kusema HAPANA, alisema uamuzi wa Wa-Ireland wengi sio kwamba wanaupinga Umoja wa Ulaya, lakini hasa wanaupinga mkataba wa Lisbon. Aliwataka wakuu wa serekali za nchi za Umoja huo warejee mezani kufanya mashauriano mepya:

"Kura hii ya HAPANA sio risala ya kuwa na ati ati kuelekea Ulaya, lakini Umoja wa Ulaya lazima uwe wenye kutabirika, ulio wa kidemokarsia na ueleweke kwa wananchi. Hali hiyo haiko hivi sasa."


Kwa kiasi fulani, rais wa komisheni ya Umoja wa Ulaya, Jose Manuel Barroso, hajaingiwa na wasiwasi mkubwa:

"Uchaguzi huu usiangaliwe kuwa ni uamuzi dhidi ya Ulaya. Wakati wa kampeni pande zote mbili zilisisitiza uwanachama wa Jamhuri ya Ireland ndani ya Umoja wa Ulaya upewe kipa umbele, na mimi naamini kwamba Ireland itaendelea kusaidia kuijenga Ulaya ilio na nguvu na kwamba nchi hiyo itatoa mchango madhubuti katika Umoja wa Ulaya."

Nini sasa cha kufanya? Jee kauli ya wananchi wa Ireland kweli itatiliwa maanani na nchi hiyo iwekwe kando, hadi pale busara itakaporejea vichwani vya wananchi wake? Ikumbukwe kwamba kwa miaka 30 sasa tangu ilipokuwa mwanachama Jamhuri ya Ireland imefaidika kutokana na misaada ya kifedha ya Umoja huo. Kuitoa Ireland kutoka Umoja huo, jambo ambalo haliwezi kulazimishwa juu ya nchi hiyo, ndio hatua ilio bora, lakini kila mtu anajuwa vika kwamba jambo hilo halitafanyika.


Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani, Frank-Walter Steimeier, anakiri kwamba kura hiyo ya HAPANA ya Ireland imeuingiza Umoja wa Ulaya katika mzozo mkubwa, lakini alisema yale ambayo yasiosemwa na wanadiplomasia, yaani kuwa na Umoja wa Ulaya bila ya Jamhuri ya Ireland:

"Inaweza kuwa pia Ireland ikajitafutia njia, kuwa kwa kipindi fulani nje ya mafungamano na Ulaya na kushuka kutoka mwenendo wa kuiunganisha Ulaya, ili njia iwe wazi uweze kufanya kazi Mkataba wa Lisbon miongoni mwa nchi 26."


Ufaransa, Poland na Uengereza zimeshadokeza kwamba fikra kama hiyo ina hatari zake, inaweza ikapiga jeki fikra za kuukataa mkataba huo katika nchi nyingine ambazo bado hazijaamua.


Nchini Uengereza,ambako serekali ya chama cha Labour inahepa kuitisha kura ya maoni na kuliachia jambo hilo liamuliwe na bunge, kiongozi wa chama cha upinzani cha Conservative, David Camweron, anahisi sasa amepata nguvu katika msimamo wake kutokana na kura iliopigwa huko Ireland:

"Maafisa wakubwa huko Brussels, kwenye makao makuu ya Umoja wa Ulaya, lazima wawasikilize raia wa Ulaya ambao hawataki kusalimisha madaraka ya mataifa yao bila ya kikomo kwa Umoja huo. Hawazitaki katiba na mikataba hii isiokwisha."


David Cameron amemtaka waziri mkuu wa nchi yake, Gordon Brown, awachane na mpango wa kuupatia kibali mkataba huo wa Lisbon. Lakini waziri wa mambo ya kigeni wa Uengereza, David Miliband, alihakikisha kwamba nchi yake mwishowe itaukubali mkataba huo.

"Naamini ni sawa kwamba tusonge mbele kulikamilisha zoezi hili, na tulikubali wazo la Ireland kuzungumzia juu ya hatua ya baadae."


Taswira inayofikiriwa baada ya kura hiyo ya Ireland ni kwamba nchi zanachama nyingine zote zitaukubali Mkataba wa Lisbon, vipengele fulani vitawekwa kwa ajili ya Ireland tu kutilia maanani hali yake na baadae nchi hiyo itapewa nafasiy a pili ya kupiga kura . Hali kama hiyo iliwahi kufanya kazi. Kwa mfanno, Wa-Ireland waliukataa mwanzo mkataba wa Nizza, na walipopiga kura mara ya pili waliukubali. Lakini yaonesha mara hii haitokuwa rahisi kwa Wa-Ireland kupewa nafasi ya pili. Na fikra ya kwamba wapatiwe vipengele fulani vya kuwaridhisha ndani ya mkataba huo ni jambo ambalo litaleta shida, kwani hiyo itamaanisha nchi 14 ambazo tayari zimeshaukubali mkataba huo kikamilifu zikariri tena zoezi la kupata kibali kipya kutoka kwa wananchi au mabunge yao. Hamna mtu anayetaka hivyo.


Fikra nyingine huenda ikawa kuuahirisha mpango wote wa kuurekebisha Umoja wa Ulaya, na baada ya kupita miaka kuufufua tena. Na ikiwa hivyo, ina maanisha umoja huo utaendelea kukabiliana na mizozo na wakati mwengine hata na ulemavu, jambo ambalo halitatoa sura nzuri kwa Ulimwengu. Matokeo yake huenda yakapelekea kuchaguliwa watu wengi ndani ya Bunge la Ulaya ambapo watapinga Ulaya kuungana zaidi; na hiyo ina maana kuyazima matumaini ya nchi kama Kroatia, Uturuki na zile nyingine zilioko katika eneo la Balkan kuingizwa katika Umoja huo.


Sakata hili la Mkataba wa Lisbon limedhihirisha kwamba Umoja wa Ulaya ulio na nchi wanachama 27, zote zikiwa na kura za turufu, ndani yake mkiweko raia milioni 500, lakini walio wachache wakiwa na uwezo wa kutia munda maamuzi muhimu, uko mwisho wa uwezo wake wa kujigeuza. Licha ya mzozo huu, haifikiriwi kwamba Umoja wa Ulaya, umoja wa pekee ulioleta amani, mafungamano na neema ya kiuchumi barani Ulaya utasambaratika.

 • Tarehe 17.06.2008
 • Mwandishi Othman, Miraji
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/ELes
 • Tarehe 17.06.2008
 • Mwandishi Othman, Miraji
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/ELes
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com