1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jamhuri ya Afrika ya Kati yaonywa kuepusha mauaji ya halaiki

6 Aprili 2014

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amewasihi viongozi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati iliokumbwa na mzozo kuzuwiya kuzuka kwa mauaji mapya ya halaiki barani Afrika ikiwa ni miaka 20 baada ya mauaji ya Rwanda.

https://p.dw.com/p/1Bcrk
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon akiwasili katika uwanja wa ndege wa Bangui na kupokewa na Rais wa mpito wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Catherine Samba-Panza. (05.04.2014)
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon akiwasili katika uwanja wa ndege wa Bangui na kupokewa na Rais wa mpito wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Catherine Samba-Panza. (05.04.2014)Picha: MIGUEL MEDINA/AFP/Getty Images

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon Jumamosi(05.04.2014) amewasihi viongozi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati iliokumbwa na mzozo kuzuwiya kuzuka kwa mauaji mapya ya halaiki barani Afrika ikiwa ni miaka 20 baada ya mauaji ya Rwanda.

Ban alifanya ziara fupi katika mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Bangui Jumamosi (05.04.2014) akiwa njiani kuelekea Rwanda kuhudhuria kumbukumbu ya miaka 20 ya mauaji ya halaiki nchini humo, amewaambia wabunge wana wajibu wa kuzuwiya kuibuka upya kwa unyama uliogharimu maisha ya takriban watu 800,000 hapo mwaka 1994.

Amekaririwa akisema " Ni wajibu wenu kama viongozi kuhakikisha kwamba hakutakuwepo na kumbukumbu za aina hiyo nchini humo" na kuonya kwamba tayari "mauaji ya kuangamiza jamii kwa misingi ya kidini" yanatokea Jamhuri ya Afrika ya Kati.Ban amewaambia wabunge hao " Msirudie makosa yaliyopita na mjifunze.Hatima ya nchi yenu imo mikononi mwenu."

Wanahitajika wanajeshi 12,000

Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ametaka kutumwa kwa wanajeshi 12,000 wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa katika koloni hilo la zamani la Ufaransa ambapo maelfu ya watu wameuwawa tokea kuzuka kwa matumizi ya nguvu chini ya misingi ya kidini mwaka mmoja uliopita.

Katika hotuba yake amesema Jamhuri ya Afrika ya Kati hivi sasa iko katika hali ya machafuko ambapo makundi yakiwa na umma mkubwa wa watu yamekuwa yakiuuwa watu ovyo,watu kukatwa vichwa na dhuluma za ngono,mambo yanayofanyika bila ya wahusika kuchukuliwa hatua.

Wanajeshi wa Ufaransa wakiwa katika doria Bangui.
Wanajeshi wa Ufaransa wakiwa katika doria Bangui.Picha: picture-alliance/dpa/ECPAD

Baada ya kukutana na Rais wa mpito wa nchi hiyo Catherine Samba Panza ameliambia bunge hilo la mpito maangamizi ya jamii chini ya misingi ya kidini na ukabila ni jambo linalotokea kikweli nchini humo ambapo Waislamu walio wachache nchini humo wameikimbia nchi hiyo.

Ban pia amesema Waislamu na Wakristo wamewekwa kwenye hatari kubwa sana kutokana tu na sababu za kuwa vile walivyo au kile wanachokiamini na kwamba usalama wa taifa umetoweka na nafasi yake kuchukuliwa na machafuko.

Katibu Mkuu huyo ambaye mwanadiplomasia mmoja wa Umoja wa Mataifa amesema alikuwa ameshtushwa sana na uwezekano wa kuzuka kwa Rwanda mpya amekuwa akijaribu kulipigia debe msaada wa kimataifa kwa ajili ya operesheni kubwa ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Afrika ya Kati ambayo pia itawajumuisha wajumbe wa kiraia.

Hali ni ya hatari

Ban amesema Jumuiya ya Kimataifa imeshindwa kuwasaidia watu wa Rwanda miongo miwili iliopita na hivi sasa iko katika hatari ya kutochukuwa hatua za kutosha kwa watu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Amesema amesikia juu ya habari za kutisha kutoka kwa watu waliopotezewa makaazi yao katika mji mkuu wa Bangui ambapo chakula ni haba na hali ya maisha ni mbaya sana na kuonya kwamba msimu wa mvua unaokaribia unaweza kuifanya hali kuwa mbaya sana.

Maelfu kwa maelfu ya Waislamu wamelazimika kuyakimbia makaazi yao kutokana na mkondo wa mashambulizi na kujibu mashambulizi kati ya kundi la Seleka na la anti-Balaka lililoundwa na wanamgambo wa Kikristo kulipiza kisasi kwa waasi hao wa zamani.

Fatu Abduleimann mwenye umri wa miaka 84 mmojawapo wa wakimbizi wakongwe wa Bangui.
Fatu Abduleimann mwenye umri wa miaka 84 mmojawapo wa wakimbizi wakongwe wa Bangui.Picha: Kriesch/Scholz/DW

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wiki ijayo linatarajiwa kuidhinisha uwekaji wa wanajeshi 12,000 wa kulinda amani Jamhuri ya Afrika ya Kati kuchukuwa nafasi ya ya wanajeshi 2,000 wa Ufaransa na 6,000 wa Umoja wa Afrika ambao tayari wako nchini humo hivi sasa ambapo inaelezwa kuwa wameelemewa na hali ya machafuko nchini humo.

Kikosi hicho kitakuwa na jukumu la kurudisha utulivu katika nchi hiyo ya kimaskini jukumu ambalo ni kubwa sana kutokana na kwamba takriban theluthi moja ya wananchi wake milioni 4.6 wamepotezewa makaazi yao.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP/Reuters

Mhariri : Bruce Amani