Jakarta yatengemaa baada ya mashambulizi ya IS | Matukio ya Kisiasa | DW | 15.01.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Jakarta yatengemaa baada ya mashambulizi ya IS

Mitaa ya mji wa Jakarta imerejea katika hali ya kawaida baada ya watu wasiopungua saba kuuwawa katika mashambulizi ya silaha na mabomu katika mji huo mkuu wa Indonesia yaliyofanywa na magaidi wa Dola la Kiislamu (IS)

Askari wa kikosi cha mabomu akiwasili kwenye eneo la tukio la miripuko mjini Jakarta siku ya Alhamisi.

Askari wa kikosi cha mabomu akiwasili kwenye eneo la tukio la miripuko mjini Jakarta siku ya Alhamisi.

Haya ni mashambulizi ya kwanza kufanywa na kundi hilo la itikadi kali dhidi ya nchi yenye idadi kubwa zaidi ya Waislamu duniani. Lakini watano kati ya waliouawa ni washambuliaji.

Ilivichukulia vikosi vya usalama karibu masaa matatu kudhibiti hali karibu na mkahawa wa Starbucks, baada ya kundi la karibu wapiganaji saba kujibizana kwa risasi na askari polisi, na kujiripua.

Vyombo vya habari vya Indonesia vimeripoti kuwa afisa mmoja wa polisi na raia wa Canada wameuawa katika mashambulizi hayo - ambao kwa pamoja na washambuliaji wamefanya idadi ya waliokufa kuwa watu saba.

Watu wengine saba akiwemo raia wa Uholanzi wamejeruhiwa, na wapiganaji wawili wamekamatwa wakiwa hai.

Askari polisi wa Indonesia wakijipanga kukabiliana na magaidi waliokuwa ndani ya jengo la maduka.

Askari polisi wa Indonesia wakijipanga kukabiliana na magaidi waliokuwa ndani ya jengo la maduka.

Shirika la habari la Aamaaq linalofungamana na kundi la Dola la Kiislamu, lilisema katika chaneli yake ya Telegram, kuwa wapiganaji wa Dola la Kiislamu ndio wamefanya shambulizi hilo la asubuhi wakiwalenga hasa raia wa kigeni na vikosi vya usalama vyenye dhima ya kuwalinda katika mji mkuu Jakarta.

Mkuu wa polisi wa mji wa Jakarta Tito Karnavian, amethibitisha kuwa IS ndiyo walifanya shambulizi hilo, na kumtaja mpiganaji wa ki Indonesia Bahrun Naim kama mtu aliefanya mipango yote.

Mashambulizi yaonyeshwa moja kwa moja

Mashambulizi hayo yaliyokuwa kama sinema ya kuigiza yalionyeshwa kwenye vituo vya televisheni vya Indonesia, yakihusisha miripuko isiyopungua sita na mapambano ya silaha. Lakini watalaamu wamesema idadi ndogo ya vifo imeashiria ushiriki wa wapiganaji wa ndani, ambao wanatumia silaha duni.

"Tunaamini kuwa Daesh ndiyo kitisho halisi kwa jamii ya kimataifa na kadiri tunavyotatua mapema mgogoro wa Syria kwa njia za kisiasa, na kuelekeza juhudi zetu, vikosi vya kimataifa vikiwemo vya Urusi, utawala wa Syria na wapiganaji wa upinzani wa Syria, kupambana dhidi ya Shetani Deash, ndivyo itakuwa bora kwetu sote," alisema waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Philip Hammond akiwa ziarani nchini Ugiriki.

Wafanyakazi wa Indonesia wakikimbia kunusuru maisha yao kufuatia miripuko ya mabomu na mashambulizi ya risasi.

Wafanyakazi wa Indonesia wakikimbia kunusuru maisha yao kufuatia miripuko ya mabomu na mashambulizi ya risasi.

Indonesia ndiyo nchi idadi kubwa zaidi ya Waislamu duniani, ambao wengi wao wanatekeleza Uislamu wenye mtazamo wa wastani. Nchi hiyo ilipitia mkururu wa mashambulizi ya wapiganaji katika miaka ya 2000, kubwa zaidi likiwa kwenye kisiwa cha mapumziko cha Bali ambamo watu 202 waliuawa, wengi wao wakiwa watalii.

Ulimwengu wataliwa na hofu

Hofu katika maeneo mbalimbali ya dunia kuhusiana na hatari kutoka kwa IS iliongezeka kufuatia mashambulizi ya Paris na mauaji ya watu 14 jimboni Califonia mwezi Desemba. Siku ya Jumanne, mripuaji wa kujitoa muhanga kutoka Syria aliwauwa watalii 10 wa Kijerumani mjini Istanmbul, na maafisa wa serikali walisema alikuwa na mahusiano na kundi la Dola la Kiislamu.

Mtaalamu wa masuala ya mapambano Harits Abu Ulya, ambaye anamhamu Bahrun Naim, mpiganaji alietajwa na maafisa wa Indonesia kuhusika na mashambulizi ya leo, amesema anatarajia mashambulizi zaidi.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre,afpe
Mhariri: Saumu Yusuf

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com