1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jaji wa Mahakama ya Juu Marekani Ruth Ginsburg afariki

Bruce Amani
19 Septemba 2020

Jaji wa Mahakama ya Juu ya Marekani Ruth Bader Ginsburg, mpiganiaji wa haki za wanawake ambaye alikuwa jaji wa pili mwanamake katika mahakama hiyo, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 87

https://p.dw.com/p/3ii2W
Ruth Bader Ginsburg
Picha: Getty Images/S. Silbiger

Kifo chake ambacho kimetokea wiki sita tu kabla ya Uchaguzi wa Rais huenda kikaanzisha mapambano makali ya kisiasa kuhusu kama Rais Donald Trump anapaswa kumteuwa, na baraza la Seneti linalodhibitiwa na Warepublican liidhinishe, mrithi wake, au kama kiti hicho kibaki wazi hadi baada ya kujulikana matokeo ya kinyang'anyiro chake dhidi ya Mdemocrat Joe Biden. Ginsburg ni Mliberali alijetambulika kwa kutetea haki za wanawake na jamii za walio wachache.

Kiongozi wa Maseneta wa Republican Mitch McConnell amesema Seneti itapiga kura ya kuidhinisha au kupinga jaji atakayependekezwa na Trump kumrithi Ginsburg, hata ingawa ni mwaka wa uchaguzi. 

US-Richterin Ruth Bader Ginsburg gestorben
Waombolezaji wakusanyika nje ya Mahakama ya JuuPicha: Tasos Katopodis/Getty Images

Trump amemuita Ginsburg "mwanamke wa ajabu" na hakutaja kuhusu kujaza kiti chake kilichobaki wazi katika Mahakama ya Juu wakati akizungumza na wanahabari baada ya mkutano wa hadhara mjini Bemidji, Minnesota.

Biden alisema mshindi wa uchaguzi wa Novemba anapaswa kumchagua mrithi wa Ginsburg. "Hakuna shaka -- acha niwe wazi -- kwamba wapiga kura wanapaswa kumchagua rais naye rais anapaswa kumchagua jaji atakayeidhinishwa na Seneti," Biden aliwaambia wanahabari baada ya kurejea katika mji wake wa nyumbani wa Wilmington, Delaware, akitokea kampeni za Minnesota.

Siku chache kabla ya kifo chake, Ginsburg alimwambia mjukuu wake wa kike Clara Spera, kuwa matamanio yake makubwa ni kuwa nafasi yake haitajazwa hadi pale rais mpya atakapoapishwa. Hayo ni kwa mujibu wa radio ya umma nchini Marekani ya NPR

Jaji Mkuu John Roberts aliomboleza kifo cha Ginsburg. "Taifa letu limempoteza mwanasheria wa hadhi ya kihistoria. Sisi katika Mahakama ya Juu tumempoteza mwenzetu aliyependwa. Leo tunaomboleza, lakini na imani kuwa vizazi vya usoni vitamkumbuka Ruth Bader Ginsburg kama tulivyomfahamu -- mpiganiaji imara na asiyechoka wa sheria."

USA Ruth Bader Ginsburg und Bill Clinton 1993
Ginsburg aliteuliwa na Clinton 1993Picha: Imago Images/ZUMA Press/R. Sachs

Ginsburg alitangaza Julai mwaka huu kuwa anafanyiwa matibabu kwenye ini lake, ikiwa ni mapambano yake kadhaa ya karibuni na ugonjwa wa saratani.

Alikataa miito ya Waliberali kumtaka astaafu wakati wa urais wa Barrack Obama katika wakati ambao Wademocrat walikuwa na udhibiti wa Seneti na mrithi wake mwenye misimamo sawa na yake angeidhinishwa. Badala yake, Trump atajaribu kushinikiza kupatikana mrithi wa Ginsburg katika Seneti inayodhibitiwa na Warepublican na kuisogeza mahakama hiyo ya kihafidhina kwa mrengo wa kulia hata zaidi.

Uteuzi wake na Rais Bill Clinton mwaka wa 1993, ulikuwa wa kwanza kufanywa na Mdemocrat katika miaka 26.

ap, afp, reuters, dpa