Ivory Coast wanyukwa na Brazil | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 21.06.2010
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Ivory Coast wanyukwa na Brazil

Brazil ambao ni mabingwa mara tano wa dunia, na pia wanaoredheshwa nambari moja, wameingia katika duru ya pili ya dimba la dunia linaloendelea nchini Afrika Kusini.

default

Brazil yajikatia tiketi ya raundi ya pili- Afrika Kusini.

Brazil walijikatia tiketi hiyo baada ya kuwanyuka Ivory Coast mabao 3-1, katika ushindi ambao ni ule mfano wa kitumbua kuuingia mchanga, pale mahiri wao Kaka alipolishwa kadi nyekundu. Huku Samba ikichezwa Brazil- Afrika wamebakia na laiti- timu nne za Afrika zina shika mkia katika makundi yao- huku Simba ya Nyika Cameroon wakiwa timu ya kwanza kuyaaga mashindano hayo yanayofanyika kwa mara ya kwanza katika bara la Afrika.

Fahari ya Afrika dhidi ya usogora wa kabumbu ya Brazil, ndivyo magazeti Afrika Kusini, yalianikiza kabla ya Samba kuingia uwanjani dhidi ya tembo wa Ivory Coast jana usiku. Brazil waliingia uwanjani, katika uwanja wa Soccer City mjini Johannesburg wakiwa na ari ya kuonyesha wengi kuwa Samba bado wanatamba, baada ya Korea Kaskazini kuwatoa kijasho katika mechi yao ya kwanza.

Flash-Galerie WM-Stars Didier Drogba

Didier Drogba alifunga bao moja dhidi ya Brazil

Na katika dakika ya 25 Luis Fabiano, anayesakata dimba nchini Spain akawaadhibu Ivory Coast aliporuka juu ya beki Kolo Toure kutia wavuni pasi safi ya baada ya Gwiji wa Brazil Kaka. Fabiano alikuwa ndio mwanyo anaanza kazi- lakini bao lake la pili katika dakiki ya 50 lilikuwa la ubishi kwani picha za televisheni zilionyesha wazi alikuwa kaunawa mara mbili mpira.

Elano alifunga awamu ya mabao ya Brazil alipotingisha wavu la Ndovu wa Ivory Coast kwa mara ya tatu- baada ya pia kupata pasi safi kutoka kwa Kaka. Ivory Coast walipata bao la kufuta machozi katika dakika ya 79 kupitia mshambulizi na nahodha wao Didier Drogba.

Ushindi wa Brazil hata hivyo ulikuwa kama ule mfano wa kitumbua kuingia mchanga pale Kaka alipolishwa kadi nyekundu baada ya kumrushia mkono Kader Keita.

Brazil sasa imejikatia tiketi ya raundi ya pili, ikiwa na pointi sita. Hatma ya Ivory Coast itategemea sana leo mechi kati ya Ureno na Korea Kaskazini. Mabingwa Itali pia jana wlaikuwa uwanjani dhidi ya New Zealand na walisalia sare ya bao moja kwa moja.

Ghana - Australien Fußball WM Weltmeisterschaft

Kevin-Prince Boateng wa Ghana katika mechi yao na Australia.

Kushindwa jana kwa Ivory Coast ni pigo kubwa kwa Afrika- hasa baada ya Simba wa Nyika Cameroon kuwa timu ya kwanza kubanduliwa kutoka mashindano hayo, Jumamosi waliposhindwa mabao 2-1 na Denmark. Ghana ndio matumaini pakee yake ya Afrika yaliandika magazeti baada ya Cameroon kufungishwa virago na Ivory Coast kuonyeshwa namna ya kusakata dimba na Brazil.

Waakilishi wanne wa Afrika katika michuano hii- wanashikilia mkia katika makundi yao. Na ingawa Ghana wana pointi nne baada ya kushinda mechi moja na kutoka sare mechi ya pili- wana mechi ya kufa na kupona na Ujerumani Jumatano.

Ni sura hii kuwa pengine Afrika itakumbukwa kwa kuwa mwenyeji mzuri wa dimba la kwanza la dunia Afrika- kuliko wengi walivyotaraji- Afrika itatamba uwanjani- ndio inakuwa sababu ya sauti za Vuvuzela kufifia viwanjani.

Mwandishi: Munira Muhammad/ AFPE; RTRE

Mhariri: Abdul-Rahman

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com