Italia yajikwaa, Ufaransa yafanya kweli | IDHAA YA KISWAHILI | DW | 22.06.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

IDHAA YA KISWAHILI

Italia yajikwaa, Ufaransa yafanya kweli

Kigogo kingine cha soka barani Ulaya Italia kimeanguka dhidi ya kikosi kutoka Amerika ya kusini jana(20.06.2014) wakati Costa Rica ilipowashangaza Wataliani kwa kuizaba bao 1-0.

WM 2014 Gruppe D 2. Spieltag Italien Costa Rica

Wachezaji wa Costa Rica wakifurahia bao lao la ushindi

Kwa kipigo hicho Italia mabingwa mara nne wa kombe la dunia imejiweka katika ukingo wa kuyaaga mashindano haya na mapema. Lakini Ufaransa haikufanya mzaha kabisa na imeikandika Uswisi mabao 5-2 katika pambano ambalo Ufaransa imeonesha uwezo mkubwa.

WM 2014 Gruppe D 2. Spieltag Italien Costa Rica

Mario Barloteli akijaribu bahati yake bila mafanikio

Baada ya mshangao mwingine katika kombe hili la dunia nchini Brazil, ushindi wa Costa Rica umeiweka timu hiyo katika nafasi ya kwanza katika kundi D na hatua hiyo inamaana kwamba Uingereza, imeyaaga mashindano haya baada ya michezo miwili, wakati Italia na Uruguay sasa zitalazimika kupambana kufa kupona katika mchezo wao wa mwisho siku ya Jumanne wiki ijayo.

Luis Suarez atakuwa fit kwa mchezo huo, ikiwa ni nafasi nzuri kwa Uruguay baada ya mshambuliaji huyo kupachika mabao yote mawili dhidi ya Uingereza juzi.

WM 2014 Gruppe D 2. Spieltag Italien Costa Rica

Makocha wa Italia, Prandelli (kulia) na Jorge Luis Pinto(kushoto)

Bao lililoizamisha Italia

Mpira uliozamishwa kwa kichwa wavuni na Bryan Ruiz katika kipindi cha kwanza ulitenganisha timu hizo mbili, na kuwaacha mashabiki wa Costa Rica walishangiria na kucheza katika uwanja wa mjini Recife wa Pernambuco baada ya kupata ushindi wa pili katika michezo miwili.

Kocha wa Italia Cesare Prandelli ameeleza matumaini kabla ya pambano dhidi ya Uruguay ,ambapo kikosi chake kinahitaji sare tu kuweza kuvuka awamu hii na kuingia awamu ya mtoano ya timu 16 kutokana na kuwa na tofauti nzuri ya magoli.

WM 2014 Gruppe E 2. Spieltag Schweiz Frankreich

Wachezaji wa Ufaransa wakishangiria bao

Ufaransa iliishinda Uswisi kwa mabao 5-2, katika mchezo wa kupendeza, wa vuta nikuvute ulikuwa na nafasi kadha za mabao na ambao ulikuwa wa kupendeza mno kwa shabiki ambaye haelemei upande wowote.

Maumivu kwa kocha Hitzfeld

Kwa kocha wa Uswisi Ottmar Hitzfeld ni hali ya kuumiza wakati akiangalia ukuta wa kikosi chake ukivunjwa na wimbi baada ya wimbi la mashambulizi kutoka kwa washambuliaji wa Ufaransa.

WM 2014 Gruppe E 2. Spieltag Schweiz Frankreich

Blaise Matuidi akirejea baada ya kupachika bao

Ushindi huo wa kishindo umeendeleza ukarabati unaoendelea wa kikosi cha Ufaransa wakati wakiwania kuzika mzuka wa miaka minne iliyopita, wakati wachezaji walipoasi na kuchafua hadhi yao.

"Ulikuwa mchezo mzuri sana , tulifanya mambo mengi kwa usahihi," amesema kocha wa Ufaransa Didier Deschamps katika mahojiano.

Matokeo hayo yameiweka Ufaransa juu ya msimamo wa kundi E ikiwa na points 6, mbele ya Ecuador ambayo ina points tatu. Kundi hilo bado liko wazi , hata hivyo, ambapo Ecuador iliishinda Honduras kwa mabao 2-1 mjini Curitiba. Timu mbili zina points sawa , Uswisi na Ecuador, lakini Ecuador ikiwa na tofauti nzuri ya mabao.

WM 2014 Gruppe E 2. Spieltag Honduras Ecuador

Mchezaji wa Ecuador akilenga mkwaju langoni mwa Honduras

Argentina na Messi

Leo jioni(21.06.2014) Leonel Messi na kikosi cha Argentina watawania kukata tikiti yao katika timu 16 bora za kombe la dunia mwaka huu nchini Brazil katika mchezo dhidi ya Iran katika uwanja wa Mineiro. Baada ya hapo itakuwa zamu ya Ghana kujaribu bahati ya timu za Afrika kuweza kuingia katika duru ya mtoano ya timu 16.

Ghana inapambana na Ujerumani inayopigiwa upatu kutoroka na kombe hili. Ujerumani inaweza kukata tikiti yake kuingia katika timu 16 bora iwapo itaishinda Ghana katika mchezo wa kundi G.

WM 2014 Deutschland Löw Training

Wachezaji wa Ujerumani wakijiandaa kwa pambano dhidi ya Ghana

Mchezo wa mwisho utakuwa kati ya Nigeria na Bosnia. Nigeria ikiwa na point 1 baada ya sare ya bila kufungana dhidi ya Iran , inakutana na Bosnia, ambayo haina point baada ya kuangushwa na Argentina kwa mabao 2-1, wakitafuta ushindi ili kuendeleza matumaini ya kushika nafasi ya pili katika kundi F.

Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre / dpae

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com