Italia, Malta zaizuia meli ya wahamiaji kutia nanga | Matukio ya Kisiasa | DW | 11.06.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Italia, Malta zaizuia meli ya wahamiaji kutia nanga

Meli ya uokozi inayowabeba wahamiaji 629 imekwama baharini kati ya Italia na Malta, baada ya nchi hizo kuikatalia kutia nanga. Viongozi wa nchi hizo wanatupiana mpira, kila upande ukiutaka mwingine kuipokea meli hiyo.

Helping hand (DW/F. Warwick)

Miongoni mwa wahamiaji hao ni watoto wanaosafiri peke yao

 

Watu 629, miongoni mwao wakiwemo watoto na wanawake wajawazito waliokolewa baharini na shirika la SOS Mediterranee na kupakiwa katika meli ya Aquarius siku ya Jumamosi. Meli hiyo hivi sasa iko katika eneo lililo kati Malta na Sicily, ikisubiri ruhusa ya kutia nanga. Hapo jana Malta iliendelea na msimamo wake wa kukataa kata kata kuipokea meli hiyo, ikikataa wito wa Italia kufanya hivyo.

Waziri wa mambo ya ndani wa Italia mwenye msimamo mkali dhidi ya wahamiaji Matteo Salvini pamoja na mwenzake ahusikaye na mamlaka za bandari Danilo Tonineli, wamesema Malta haiwezi kuendelea kutazama pembeni, kila inapohitajika kuheshimu mikataba ya kimataifa kuhusu kuwalinda binadamu. Amesema ni kwa mantiki hiyo kwamba wanaitaka serikali ya Malta mjini Valetta kupokea meli ya wahamiaji ili iweze kuwapatia msaada wa kwanza.

Italien | Matteo Salvini (Reuters/T. Gentile)

Matteo Salvini, waziri wa Italia wa mambo ya ndani mwenye sera kali dhidi ya wahamiaji

Serikali ya Malta imejibu kwamba waziri wake mkuu Joseph Muscat amefanya mazungumzo kwa njia ya simu na mwenzake wa Italia Giuseppe Conte, akisisitiza kwamba nchi yake haijakiuka kwa njia yoyote majukumu yake ya kimataifa.

Kusaidiwa huko huko waliko

Maafisa wa meli ya Aquarius waliarifu jana usiku kupitia mtandao wa twitter, kwamba wameombwa na mamlaka ya Italia kubaki walipo. Waziri mkuu wa nchi hiyo Giuseppe Conte amethibitisha kwamba Italia imetuma meli mbili za doria na madaktari mahali ilipo meli hiyo, ili waweze kuwapa huduma ya kwanza ya matibab wale wanaoihitaji.

Msemaji wa serikali ya Malta ameliambia shirika la habari la AFP kwamba  wahamiaji hao wameokolewa katika eneo la la Bahari ya Mediterania lililo chini ya himaya ya Libya, na baadaye walikuwa wakisafirishwa kuelekea Italia, na kwa hivyo serikali ya nchi yake haikuwa na jukumu lolote lile kisheria kuwapokea wahamiaji hao.

Mittelmeer - Flüchtlinge - Boot (Getty Images/M. Bicanski)

Kila mwaka maelfu ya wahamiaji huvuka Bahari ya Mediterania wakitafuta hifadhi barani Ulaya

Mapema leo mmoja wa wafanyakazi wa meli ya Aquarius Alessandro Porro amekiambia kituo cha televisheni cha Sky TG24 kwamba meli yao ilikuwa Kaskazini mwa kisiwa cha Malta, na kwamba walikuwa hawajapata mawasiliano yoyote na mamlaka ya nchi hiyo.

Swali lisilo na jibu

Alisema watu waliowaokoa waliwakuta katika hali ya ngumu, huku takribani 50 miongoni mwao wakikabiliwa na hatari ya kuzama. Porro alisisitiza kuwa wanachotaka kufahamu ni mahali bandari wanayoweza kutia nanga, na kwamba hadi wakati huo walikuwa hawana jibu kwa swali hilo.

Miongoni mwa wahamiaji walio katika meli hiyo, 123 no watoto wanaosafiri peke yao na 11 ni watoto wadogo. Melini humo pia wapo wanawake 7 wajawazito.

Hata hivyo nchini Italia zinasikika sauti za kutaka kuwasaidia wahamiaji hao. Meya wa mji wa Kusini wa Taranto amesema hawawezi kuwapa kisogo watu walio hatarini, naye meya wa mji wa Napoli amesema kupitia mtandao wa twitter kwamba ikiwa waziri asiye na moyo hajali masaibu ya watoto na akina mama wajawazito, Napoli itakuwa tayari kuwakaribisha.

Mwandishi: Daniel Gakuba/ape, afpe

Mhariri: Iddi Ssessanga

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com