1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yazidisha mashambulizi dhidi ya Gaza

10 Julai 2024

Vikosi vya Israel vimefanya mashambulizi makali zaidi leo kwenye Ukanda wa Gaza siku moja baada ya kuilenga shule katika hujuma ambayo maafisa wa afya wa Kipalestina wamesema imewaua watu wasiopungua 29.

https://p.dw.com/p/4i6TX
Ukanda wa Gaza | Wakaazi wakitafuta manusura baada ya shambulizi.
Raia wa Ukanga wa Gaza wakitafuta manusura baada ya vikosi vya Israel kushambulia majengo kadhaa.Picha: EYAD BABA/AFP via Getty Images

Mapema leo asubuhi watu wanne waliuawa na mwengine kujeruhiwa vibaya pale makombora ya Israel yalipoishambulia nyumba moja katikati mwa mji wa Nuseirat. 

Taarifa hizo ni kulingana na duru za kiafya na kiusalama kwenye Ukanda wa Gaza.

Duru pia zinasema Israel imezidisha mashambulizi ya anga na ardhini kwenye mji wa Gaza na kusini mwa ukanda huo, eneo ambalo ilitoa amri ya kuwataka mamia kwa maelfu ya watu kuondoka.

Soma pia:Zaidi ya watu 500,000 wakimbia mapigano Rafah, UN

Ama kuhusu shambulio la jana Jumanne lililoilenga shule katika mji wa kusini wa Khan Yunis, jeshi la Israel limesema linachunguza hujuma hiyo.