1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yashambulia tena Gaza

Bruce Amani
15 Novemba 2019

Israel imesema imekamilisha mfululizo wa mashambulizi ya angani katika maeneo yanayohusishwa na kundi la wanamgambo la Islamic Jihad katika Ukanda wa Gaza

https://p.dw.com/p/3T5bx
Gaza Konflikt
Picha: Getty Images/AFP/A. Baba

Taarifa ya jeshi la Israel iliyotolewa mapema leo inaashiria kuwa nchi hiyo iko tayari kuheshimu mpango wa kusitisha mapigano kama hakutakuwa na mashambulizi Zaidi ya makombora. Jeshi la Israel limesema limelishambulia eneo moja la kijeshi, kiwanda cha kutengeneza makombora na makao makuu ya wanamgambo  katika mji wa Khan Younis.

Hali tete ya utulivu imeshuhudiwa jana nchini Israel na katika Ukanda wa Gaza, baada ya mpango wa kusitisha mapigano uliosimamiwa na Misri kati ya Israel na wanamgambo wa Islamic Jihad kuanza kutekelezwa katika saa za asubuhi. Kwa mujibu wa jeshi la Israel, hata hivyo, makombora yalifyatuliwa kuelekea Israel kutokea eneo hilo la pwani baada makubaliano hayo kuanza kutekelezwa.

Mos'ab al-Breim, msemaji wa Islamic Jihad, amesema kundi lake limedhamiria kuheshimu mpango uliofikiwa na Misri na kwamba kuna makubaliano ya Wapalestina ya kudumisha utulivu uliopo kwa sasa.

Gaza Deir al-Balah Raketenangriffe
Wapalestina 34 wameuawa tangu machafuko kuanzaPicha: picture-alliance/AP Photo/K. Hamra

Kwa mujibu wa msemaji huyo, makubaliano hayo ni pamoja na kusitishwa kwa mauaji yanayowalenga viongozi wa wanamgambo, kuwalinda waandamanaji wa Kipalestina katika Ukanda wa Gaza na hatua za kuumaliza mzingiro wa Gaza.

Nickolay Mladenov, mratibu maalum wa Umoja wa Mataifa kwa mchakato huo wa Mashariki ya Kati, ambaye alikuwa ameenda Cairo kusaidia kufikiwa makubaliano ya kusitisha mapigano, aliandika kwenye Twitter ujumbe wa kuzitaka pande zote "kuonyesha kiwango kikubwa cha kujizuia”.

Usitishwaji huo wa mapigano haukuthibitishwa rasmi na serikali ya Israel. Lakini msemaji wa jeshi Jonathan Conricus alisema walifahamishwa kuhusu makubaliano hayo.

Jeshi la Israel jana Alhamisi liliondoa vizuizi vya usalama dhidi ya jamii zilizoko karibu na Gaza baada ya kuitathmini hali ya sasa. Zaidi ya makombora 450 yamevurumishwa katika maeneo ya kusini mwa Israel tangu Jumanne, kwa mujibu wa jeshi la Israel, huku mengi yakiharibiwa na mfumo wa ulinzi wa angani wa Iron Dome.

Mashambulizi hayo kati ya Israel na wanamgambo wa Kipalestina yamewauwa watu 34 katika Ukanda wa Gaza wakiwemo raia 16, tangu yalipoanza Jumanne kama jibu la mauaji ya Israel yaliyowalenga viongozi wawili wa Islamic Jihad, ambapo moja lilimuua kiongozi wa Quds Brigades Rasmi Abu Malhous, ambalo ni tawi la wapiganaji la Islamic Jihad katika Ukanda wa Gaza.