1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yashambulia maeneo ya Iran, Syria

Sekione Kitojo
11 Februari 2018

Israel imeshambulia kile ilichosema ni maeneo ya Iran ndani ya Syria Jumamosi (10.02.2018)katika shambulio kubwa baada ya  moja kati ya ndege zake za kivita kushambuliwa na mfumo wa ulinzi wa nga wa Syria na kuanguka.

https://p.dw.com/p/2sT95
Israel Air Force F-15
Picha: picture-alliance/AP/A. Schalit

Kufuatia  makabiliano   makubwa  kabisa  baina ya mahasimu  hao wakubwa  Israel na  Iran  tangu  vita  vya  wenyewe  kwa  wenyewe nchini  Syria  kuanza  mwaka  2011, waziri  mkuu  Benjamin Netanyahu  aliapa  kuizuwia  Iran  kuweka majeshi  yake katika  taifa hilo  la  Kiarabu.

Libanon | Reste einer Rakete in Kaoukaba
Mabaki ya kombora katika eneo la Kaoukaba nchini SyriaPicha: Getty Images/AFP/A. Dia

Mashambulizi  ya  Israel  yamekuja  baada  ya  kuingilia  kati  kile ilichosema  kuwa  ni  ndege isiyokuwa  na  rubani  ya  Iran  iliyoingia katika  anga  lake  kutoka  Syria, na  kuiita  kuwa  ni  "shambulio".

Marekani  imeiunga  mkono  Israel  na  kuilaumu  Iran kwa kuchochea uhasama. Katibu  mkuu  wa  Umoja  wa  Mataifa  Antonio Guterres alitoa  wito wa  "kuachana  na  hali  ya  kuchochea  ghasia haraka  na  bila  ya masharti" nchini  Syria, msemaji  wa  Umoja  wa Mataifa  Stephane Dujarric  alisema  katika  taarifa.

Äthiopien Addis Abeba Afrikanische Union Gipfel Guterres
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio GuterresPicha: Getty Images/AFP/S. Maina

Uongo wa Israel

Ilikuwa  mara  ya  kwanza  Israel  kukiri  hadharani  kwamba imelenga   kile  ilichokieleza  kuwa  ni  maeneo  ya  Iran nchini  Syria tangu  mzozo  huo  kuanza. Iran imeshutumu  kile  ilichosema  kuwa ni  "uongo"  wa  Israel  na  kusema  Syria  ina  haki  ya  kujilinda dhidi  ya  mashambulizi. Katika  hali  tofauti, Iran  imetoa  taarifa pamoja  na  washirika  wakuu  wengine  wa  Syria, Urusi  na  kundi la  wanamgambo  wa Lebanon  la  Hezbollah, wakikana madai  ya ndege  isiyokuwa  na  rubani  yaliyotolewa  na  Israel.

Israel Benjamin Netanjahu
Waziri mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: picture-alliance/AP Photo/A. Sultan

Wizara  ya  mambo  ya  kigeni  ya  Urusi  imetaka  kuwepo  na "kujizuwia" kutoka  pande  zote, na  kuongeza  kwamba "haikubaliki kuanza  kutengeneza  mazingira  ya  vitisho kwa  maisha  na usalama  ya  wanajeshi  wa  Urusi" ndani  ya  Syria.

Msemaji  wa  jeshi  la  Israel Jonathn Conricus ameonya  kwamba Syria  na  Iran "zinacheza  na  moto", lakini alisisitiza kwamba  nchi yake haitaki kuendeleza mzozo  huo. "Huu ni ukiukaji  mkubwa kabisa  wa  mipaka  ya  Israel  kufanywa  na  Iran"  katika  historia ya  miaka  ya  hivi  karibuni, Conricus  aliwaambia  waandishi habari.

ISRAEL-SYRIA-CONFLICT-GOLAN
Mabaki ya ndege ya Israel iliyoshambuliwa nchini Syria katika picha iliyochukuliwa kaskazini mwa IsraelPicha: Getty Images/AFP/J. Guez

Israel  ilisema  kulipiza  kisasi  ilifanya  "mashambulizi  makubwa" dhidi  ya  mfumo  wa  ulinzi  wa  anga  wa  Syria na  maeneo  ya Iran. "maeneo  kumi  na  mbili, ikiwa  ni  pamoja  na  vifaa  vitatu  vya ulinzi  wa  makombora ya  angani  pamoja  na  maeneo  manne ambayo  ni  sehemu ya  jeshi  la  Iran  nchini  syria  vilishambuliwa," taarifa  ya  jeshi  imesema. Marubani  wawili  waliokuwamo  katika ndege  chapa  F16 wako  hai baada  ya  kuruka  kutoka  katika ndege  hiyo, licha  ya  kuwa  walijeruhiwa  vibaya, jeshi  lilisema.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / afpe

Mhariri: Bruce Amani