1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroIsrael

Israel yashambulia Gaza baada ya wanamgambo kurusha roketi

Sylvia Mwehozi
27 Januari 2023

Waziri wa ulinzi wa Israel Yoav Gallant ameashiria kuwa jeshi la nchi yake litasitisha mashambulizi ya anga kama wanamgambo wa Kipalestina nao watasitisha ufyatuaji wa makombora.

https://p.dw.com/p/4MnU4
Gaza | Israelische Luftangriffe auf Gaza
Picha: Arafat Barbakh/REUTERS

Mapema siku ya Ijumaa, wanamgambo wa Kipalestina walifyatua maroketi kadhaa kutokea ukanda wa Gaza kuelekea kusini mwa Israel huku Israel nayo ikifanya mashambulizi ya anga kuelekea Gaza. Swala ya Ijumaa katika Msikiti wa Al-Aqsa mjini Jerusalem, ambayo mara nyingi huchochea vurugu baina ya Wapalestina na polisi wa Israel, leo imefanyika kwa utulivu, ingawa kulikuwa na ulinzi mkali.

Mashambulizi ya Ijumaa ya kila upande yametokea baada ya uvamizi uliofanywa na Israel katika eneo linalokaliwa la Ukingo wa Magharibi siku ya Alhamis na kusababisha vifo vya Wapalestina 9. Kuongezeka kwa machafuko katika eneo hilo kunatoa mtihani wa mapema kwa serikali ya mrengo mkali wa kulia ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahuna kutia dosari ziara ya waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken anayotarajiwa kuifanya wiki ijayo.

Uvamizi huo pia umechochea ghasia katika maeneo mengine ambako vikosi vya Israel vimemuua kijana wa miaka 22 katika mji wa kaskazini mwa Jerusalem wa Al-Ram. Kwenye taarifa yake jeshi la Israel limesema kati ya maroketi matano yaliyofyatuliwa kuelekea Israel, matatu yamezuiliwa, moja limeanguka katika eneo la wazi na jingine liliangukia ndani ya eneo la Gaza. Mashambulizi ya anga ya Israel yalilenga kiwanda cha chini ya ardhi cha kutengeneza maroketi cha Hamas pamoja na maeneo ya mafunzo ya wanamgambo.

Konflikte im Westjordanland
Wapalestina wakikagua sehemu ya jengo lililoharibiwa katika uvamizi wa Israel huko JeninPicha: Ayman Nobani/dpa/picture alliance

Awali, kundi la Hamas lilikuwa limetishia kulipiza kisasi dhidi ya uvamizi huo. Rais wa mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas ametangaza siku tatu za maombolezo, na katika kambi hiyo wakaazi walichimba kaburi la watu wengi kwa ajili ya mazishi.

Baada ya uvamizi wa Alhamis Mamlaka ya Wapalestina ambayo ina uwezo mdogo wa kiutawala katika Ukingo wa Magharibi ilitangaza kusitisha mpango wa uratibu wa kiusalama na Israel ambao umekuwa ukisifiwa kusaidia kuweka utulivu na kuzuia mashambulizi dhidi ya Israel.Palestina yalaani ziara ya waziri wa Israel eneo la Al-Aqsa

Msemaji wa Mamlaka ya Wapalestina Nabil Abu Rudeineh amesema kuwa wanapanga kuwasilisha malalamiko kwa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, mahakama ya kimataifa ya uhalifu pamoja na mashirika mengineyo. Kwa upande wake waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ambaye amerejea mamlakani mwaka huu, alisema kuwa Israel haitafuti kuzidisha mvutano huo, ingawa ameamuru vikosi vya usalama kuwa katika hali ya tahadhari.Wapalestina wawili wauawa kwenye operesheni ya kijeshi

Miezi kadhaa ya vurugu ambazo ziliongezeka baada ya mkururo wa mashambulizi ya vifo dhidi ya Israel mwaka jana, imezusha hofu kwamba mvutano huo unaweza kuenea na kushindwa kudhibitiwa na kusababisha makabiliano makali baina ya Wapalestina na Israel.

Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imetoa taarifa hapo jana ikisema kuwa "ina wasiwasi" na machafuko katika Ukingo wa Magharibi na kuzitaka pande zote kupunguza mvutano.