Israel yapiga maeneo zaidi ya Hamas | Matukio ya Kisiasa | DW | 30.05.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Israel yapiga maeneo zaidi ya Hamas

Israel imesema imeyashambulia maeneo 25 ya kundi la Hamas usiku kucha baada ya msururu wa mashambulizi ya makombora yaliyofyetuliwa kutoka Ukanda wa Gaza

Majibizano hayo yamezusha uwezekano wa kutokea tena vita vingine katika Ukanda huo wa Kipalestina unaodhibitiwa na vuguvugu la itikadi kali la Hamas, ambavyo vinaweza kuwa vya nne tangu mwaka wa 2008.

Israel imesema iliyalenga maeneo zaidi ya 60 ya kijeshi katika Ukanda wa Gaza katika kipindi cha masaa 24 yaliyopita, ikisema karibu makombora 70 yalivurumishwa katika ardhi yake siku nzima ya Jumatatu, ambapo kadhaa yalizuiwa na mifumo ya ulinzi wa makombora ya angani.

Lakini baada ya hali kuongezeka, ikifuatiwa na milio ya ving'ora na milipuko usiku kucha, kukawa na madai ya Wapalestina ya kufikiwa makubaliano ya kusitisha mapigano.

Jana usiku, msemaji wa kundi la Islamic Jihad ambalo ndilo la pili kubwa lenye silaha katika Ukanda wa Gaza baada ya Hamas, alisema makubaliano ya kuweka chini silaha yamefikiwa, na leo afisa wa ngazi ya juu wa Hamas Khalil al-Hayya akazungumzia muafaka huo.

Gazastreifen Protest gegen israelische Seeblockade (picture-alliance/ZumaPress/M. Ajour)

Wanaharakati wa Kipalestina wakifanya maandamano

Jeshi la Israel halijazungumza, lakini Waziri wa Ujasusi Yisrael Katz alikanusha madai ya kufikiwa makubaliano hayo. Ameiambia redio ya taifa kuwa Israel haitaki hali kuendelea kuwa mbaya, lakini wote walioanzisha machafuko lazima wayasitishe.

Katika taarifa ya pamoja isiyo ya kawaida, Hamas na Islamic Jihad walidai kuhusika na mashambulizi ya maroketi wakisema yalikuwa ya kulipiza kisasi mashambulizi ya Israel yanayofanywa na Israel yakiyalenga maeneo yao. Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu aliapa jana "kujibu mashambulizi hayo kwa nguvu”  muda mfupi baada ya kuzungumza, jeshi la Israel likaanzisha mashambulizi ya angani Gaza.

Jeshi la Israel lilisema liliyashambulia maeneo ya kijeshi ya Hamas likiwemo handaki linalotokea upande wa Gaza hadi upande wa Israel, maghala ya silaha na vituo vya kijeshi.

Rais wa Palestina Mahmoud Abbas alisema hatua ya Israel kulipiza kisasi mashambulizi hayo inaashiria kuwa Israel haitaki Amani.

Kipindi kilichokuwa na vurugu kimeshapita katika Ukingo wa Magharibi, Jerusalem na hasa kwenye Ukanda wa Gaza. Israel ilifanya leo mashambulizi makali ya maroketi kwenye ukanda wa Gaza. Hii inaashiria kuwa Israel haitaki Amani. Hata hivyo sisi tunataka Amani na tunadai Amani.

Kumekuwa na utulivu kiasi leo asubuhi katika Ukanda wa Gaza. Machafuko ya jana yalifuatia wiki za vurugu na maandamano kwenye mpaka kati ya Israel na eneo la Kipalestina linalozingirwa. Baraza za usalama la Umoja wa Mataifa linatarajiwa kukutana leo kuyajadili machafuko hayo ya Gaza, kufuatia ombi la Marekani la kuandaliwa mkutano wa dharura.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Josephat Charo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com