Israel na Syria zaridhishwa na hatua iliyofikiwa katika mazungumzo | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 22.05.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Israel na Syria zaridhishwa na hatua iliyofikiwa katika mazungumzo

Israel huenda ikaamua kufanya maamuzi magumu juu ya suala la ardhi ya Golan

default

Waziri mkuu Ehud Olmert asema sio ndoto bali inawezekana kufikia mwafaka wa amani na Syria

Uturuki ambayo imeongoza mazungumzo ya amani yasiyo ya moja kwa moja kati ya Israel na Syria imesema pande hizo mbili zimeridhishwa na matokeo ya mazungumzo hayo.Mazungumzo hayo yalianzishwa tena jumatatu baada ya kuvunjika miaka minane iliyopita.Hii leo waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Ali Babacan amesema siku tatu za majadiliano kati ya pande hizo mbili zimeonekana kuzaa matunda ya kheri kuelekea amani baina ya mahasimu hao wa jadi.Akaongeza kusema kwamba Syria na Israel zimeafikiana katika masuala kadhaa na kwamba mazungumzo hayo yataendelea kufanyika baada ya kipindi cha muda fulani.Kwa upande mwingine Syria kupitia waziri wake wa mambo ya nje Walid Muallem imedai kwamba imehakikishiwa na Israel kwamba itaondoka kabisa katika ardhi yake ya milima ya Golan ambayo iliinyakua miongo minne iliyopita.Hata hivyo Israel haijasema lolote kuhusu suala hilo ingawa waziri mkuu Ehud Olmert alitangaza wazi jana mjini Tel Aviv kwamba wako tayari kufanya maamuzi magumu kuiridhia Syria ili kwa lengo la kufikia amani.Mpatanishi katika mazungumzo kati ya nchi hizo mbili Ali Babacan amekataa kusema chochote kuhusu masuala yaliyojadiliwa na pande hizo mbili lakini amesema muhimu kilicholeta mazungumzo hayo ni kutafuta amani katika suala linalohusu ardhi. Aidha amesema itawezekana Syria na Israel kuingia katika mazungumzo ya ana kwa ana ikiwa hatua ya kuridhisha itapigwa katika mpango huu.

Hisia kali lakini zimeanza kujitokeza nchini Israel kuhusiana na tetesi kwamba huenda ikaondoka katika ardhi ya Syria ya eneo la milima ya Golan kama alivyodokeza waziri mkuu Ehud Olmert ambaye amekiri haitokuwa rahisi kuchukua uamuzi huo lakini sio ndoto.Amesema anaamini kwamba uwezekano wa mafanikio ni mkubwa kuliko hatari iliyopo.Kufuatia matamshi hayo Eli Yishai, kiongozi wa chama cha Shas chenye itikadi kali ya dini ya kiyahudi na ambacho ni mshirika katika serikali ya muungano ameikosoa hatua hiyo akidai kwamba Syria inayounga mkono makundi ya Hezbollah na Hamas ni sehemu ya mhimili wa uadui dhidi ya Isreal.

Uchunguzi wa maoni unaonyesha kwamba wabunge pamoja na raia hawatafautiani katika mtazamo huo.

Imebainika kwamba asilimia 70 ya waisrael wanapinga kuachia ardhi ya Golan kwa ajili ya amani.Wanasiasa wengi nchini Isreal wanamshutumu Olmert kwa kutangaza uwezekano huo wa kurudisha ardhi ya Golan kwa Syria wakidai kwamba ni juhudi zake za kutaka kuwasahaulisha watu juu ya tuhuma za rushwa zinazozidi kumuandama.Hata upinzani wa mrengo wa kushoto ambao unaunga mkono suala la kuachia ardhi hiyo unahoji ikiwa kweli Olmert anakubalika kimaadili kuanzisha juhudi kama hizo.Lakini afisi ya waziri mkuu huyo imesisitiza kwamba mazungumzo hayo hayahusiani kabisa na madai kwamba Olmert amepokea hongo kutoka kwa mfanyibiashara mmoja wa Kimarekani.Olmert ambaye kesho atahojiwa tena na kikosi maalum cha kupambana na rushwa ameshasema atajiuzulu ikiwa atakutikana na hatia.

 • Tarehe 22.05.2008
 • Mwandishi Saumu Mwasimba
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/E4PY
 • Tarehe 22.05.2008
 • Mwandishi Saumu Mwasimba
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/E4PY
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com