1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Israel na Sudan zaafikiana kuboresha uhusiano wao

3 Februari 2023

Israel na Sudan zimekamilisha makubaliano ya kusawazisha uhusiano wa kidiplomasia huku Israel ikiarifu kuwa makubaliano hayo yatasainiwa mara tu Jeshi litapokabidhi madaraka kwa viongozi wa kiraia.

https://p.dw.com/p/4N3Wx
Fahnen Israel - Sudan NAH
Picha: Jack Guez/AFP/Getty Images

Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel Eli Cohen ambaye alifanya ziara ya ghafla nchini Sudan, ametoa tangazo hilo siku ya Alhamisi akiwa kwenye uwanja wa ndege wa Tel Aviv na kusema mkataba wa kihistoria utatiwa saini mjini Washington baadaye mwaka huu. Cohen amesema makubaliano hayo ni muhimu kwa mataifa yote mawili:

"Nina furaha kutangaza kwamba kama sehemu ya ziara hiyo, tulikubaliana kutia saini mkataba wa amani kati ya Sudan na Israel. Sudan ni nchi ya Kiarabu, ya Kiislamu, na ya kimkakati kwa Israel. Kutiwa saini kwa makubaliano ya amani kutanufaisha nchi zote mbili, kutaimarisha usalama wa taifa la Israel, kuimarisha utulivu wa kikanda na kuchangia kunako uchumi."

Soma zaidi:Sudan yasema serikali ya mpito haina mamlaka ya kurejesha mahusiano na Israel 

Sudan | General Abdel Fattah al-Burhans mit Eli Cohen in Khartum
Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel Eli Cohen (Kushoto) akisalimiana na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, Mtawala wa Kijeshi nchini SudanPicha: SOUVEREIGN COUNCIL OF SUDAN/HO/AFP

Uongozi nchini Sudan umetangaza kuwa mkutano huo umejadili kuhusu kuanzishwa kwa mahusiano mema na Israel lakini wakati huo huo Israel ikitakiwa kufikia hali ya utulivu kati yake na watu wa Palestina.

Serikali ya Marekani ilikuwa tayari imetangaza mwaka 2020 kuwa Israel na Sudan zilidhamiria kuanzisha mahusiano kamili ya kidiplomasia chini ya mfumo wa kile kiitwacho "Makubaliano ya Abraham".

Baadaye Sudan ilitia saini makubaliano na Marekani lakini sio Israel. Chanzo kikiwa mvutano wa ndani wa kutokubaliana kuhusu masuala nyeti katika nchi hiyo yenye Waislamu wengi.

Israel yashinikiza utawala wa kiraia Sudan

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Israel imesema makubaliano hayo yatatiwa saini katika miezi ijayo baada ya kuanzishwa kwa serikali ya kiraia ambayo itakuwa sehemu ya kuendelea kwa mchakato wa mpito nchini Sudan.

Soma zaidi:Israel, nchi za kiarabu wajadili usalama Abu Dhabi 

Nchi hiyo imekuwa katika mgogoro wa utawala tangu kung´atuliwa kwa kiongozi wa muda mrefu Omar al-Bashir mnamo mwaka 2019. Awali, serikali ya mpito ilijaribu kuanzisha mchakato wa kidemokrasia. Hata hivyo miaka miwili baadaye, jeshi likiongozwa na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan lilipindua tena serikali na kuhodhi mamlaka tangu wakati huo. Lakini Desemba 2022, Burhan alikubali kugawana kwa awamu madaraka kati ya wanajeshi na wanasiasa wa kiraia.

Soma zaidi: Israel na UAE zasaini makubaliano ya biashara huru

Mnamo mwaka 2020, Falme za Kiarabu na Bahrain yalikuwa mataifa ya kwanza ya Ghuba kusaini makubaliano ya kuanzisha mahusiano ya kidiplomasia na Israel, yakifutaiwa baadaye na nchi ya Morocco.

Kwa wakati wote, mataifa pekee ya Kiarabu yaliyodumisha uhusiano wa kidiplomasia na taifa hilo la Kiyahudi walikuwa majirani zake ambao ni Misri na Jordan.