1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel na Marekani zahamaki baada ya majaribio ya maroketi

Kitojo, Sekione10 Julai 2008

Baada ya Iran kufanya majaribio ya makombora yake ya masafa marefu na ya kati , Marekani na Israel zimeanza kushambulia hatua hiyo kwa kusema kuna haja ya kusitishwa kwa shughuli za kinuklia.

https://p.dw.com/p/EZmP
Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Condoleezza Rice wakati alipokuwa wakikutana na rais wa Georgia Saakashvili na kutoa onyo kwa Iran kwamba nchi yake itakuwa tayari kulinda maslahi ya washirika wake.Picha: AP



Iran imesema katika taarifa iliyotangazwa katika vyombo vya habari vya nchi hiyo kuwa imefanya majaribio tisa ya makombora yanayokwenda masafa ya kati na marefu, hali ambayo imeleta hali ya wasi wasi katika eneo hilo. Miongoni mwa makombora hayo kuna kombora jipya Shahab 3 ambalo lina uwezo wa kwenda kilometa 2,000 na kufika Israel. Kitendo hicho cha Iran kimezusha majibizano kutoka Israel na Marekani.




Ni nafasi na muda wa wale wanaopenda kutumia mabavu nchini Israel kwa sasa. Wanasiasa kama vile Juval Steinitz kutoka chama cha upinzani cha Likud anahisi baada ya majaribio hayo ya makombora nchini Iran kuwa msimamo wake umeimarika.

Steinitz amerudia madai yake kuhusiana na upinzani wake wa mpango wa kinuklia kwa Iran.



Tumeweka wazi kuwa ,wakati makombora haya siku moja yatawekwa silaha za kinuklia, itakuwa kitisho kikubwa kwa Israel na ni kitisho cha kweli kwa Ulaya yote. Ndio sababu ni lazima kufanya kila linawezekana, ili kuweza kuzuwia mpango huu wa kinuklia wa Iran, kabla makombora hayo hayajaleta athari kubwa.


Wasi wasi hata hivyo ni kuhusiana na , iwapo Israel itaishambulia Iran katika maeneo yake ya vinu vya kinuklia, ili kuharibu vinu hivyo, na kuanzia hapo hakuna mtu ambaye anafahamu hali itakuwaje. Hakuna siku inayokwenda, ambapo katika vyombo vya habari lisitajwe suala hili la uwezekano wa mashambulizi dhidi ya Iran.



Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Condoleezza Rice ameionya Iran leo kuwa nchi yake italinda washirika wake dhidi ya ushari wa Iran.

Marekani inahisi kuwa Iran inajaribu kujenga bomu la kinuklia huku ikidai kuwa mpango wake huo ni kwa ajili ya matumizi ya kujipatia nishati ya umeme.

Rice amesema wakati akikutana na rais wa Georgia Mikheil Saakashvili kuwa nchi hiyo inalichukulia kwa dhati jukumu hilo la kuwasaidia washirika wake ili waweze kujilinda na kila mtu anapaswa kulifahamu hilo.


Tumetoa ishara kwa serikali ya Iran na ni kwa njia ya maazimio matatu ya baraza la usalama ,ambayo yanasema kuwa Iran inakwenda kinyume na majukumu ya kimataifa na inahitaji kwenda katika njia sahihi ya jumuiya ya kimataifa. Pia tunatoa ishara kwa Iran kuwa tutalinda maslahi ya Marekani na maslahi ya washirika wetu katika eneo la ghuba.


Iran ilipuuzia wito wa Marekani wa kusitisha majaribio yake zaidi ya makombora kwa kutangaza baadaye kuwa inafanya mazoezi zaidi ya kijeshi usiku. Na kwa mara nyingine tena Iran imefanya majaribio mengine ya makombora leo na kupuuzia miito ya jumuiya ya kimataifa kutofanya hivyo.



►◄