1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ireland yaukataa Mkataba wa Lisbon

Miraji Othman17 Juni 2008

Mawaziri wa Jumuiya ya Ulaya hawajui la kufanya juu ya Ireland.

https://p.dw.com/p/ELdy
Bunge la Ulaya mjini Strassbourg, UfaransaPicha: EU


Kwa mara nyingine tena mustakbali wa Umoja wa Ulaya uko gizani, na kwa mara nyingine tena kuupata ushauri mzuri wa kuitazua hali hiyo unaonekana kuwa ni jambo gumu. Mawaziri wa mambo ya kigeni wa nchi za Umoja wa Ulaya wanajaribu kupunguza makali ya pigo hilo, lakini ukweli unabakia pale pale, nao ni kwamba Jumuiya hiyo, kwa mara nyingine tena, imeingia kwenye mzozo.


Hata kama mawaziri wa mambo ya kigeni wa Jumuiya ya Ulaya, waliokutana jana mjini Luxembourg, walijaribu kutoipa sura mbaya hali ya mambo na kutamka maneno matamu, ni wazi kabisa kwamba Umoja wa Ulaya uko katika shida, na haujuwi vipi ujikwamuwe na sakata hili la nchi zote wanachama 27 kutakiwa kuupa kibali mkataba wa Lisbon wa kuifanyia marekebisho jumuiya yenyewe. Nchi zote zinatakiwa ziseme NDIO kabla ya mwisho wa mwaka huu.


Waziri wa mambo ya kigeni wa Ireland alibanwa na mawaziri wenzake wa Ulaya atoe pendekezo. Alikuwa hana, ila alishauri tu nchi yake ipewe wakati wa kutafakari na kuichambua hali ya mambo. Lakini Jumuiya ya Ulaya haiwezi kumudu kutoa wakati huo, kwani kwa mara ya pili sasa, baada ya mwaka 2005, kuna hatari ya kushindwa mradi wa kuufanyiwa umoja huo marekebisho ya kimsingi. Pindi nchi 27 wanachama zitashindwa kufikia makubaliano ya haraka, basi umoja huo hautaaminika. Lakini kipi ambacho sasa kinawezekana?


Umoja wa Ulaya unaweza ukausuka upya mkataba huo na kuanzisha mashauriano mepya juu yake. Jambo hilo litachukuwa miaka na matakwa mahsusi mepya kutoka nchi mbali yatachomoza. Jamhuri ya Ireland inaweza kuupigia tena kura mkataba huo, lakini hiyo itamaanisha kudharau uamuzi wa wapiga kura wa sasa. Na zaidi ya hayo, mbona Wafaransa na Waholanzi walipoikataa katiba ya Ulaya miaka mitatu iliopita hawajatakiwa wapige kura tena?


Mbadala mwengine labda utakuwa kwa Ireland kujitoa kutoka Umoja wa Ulaya na kuziwachia nchi nyingine 26 zilizobaki zisonge mbele na Mkataba wa Lisbon. Nchi hiyo itaweza baadae kurejea katika klabu hiyo.Taswira hiyo ndio inayoingia akilini, lakini haifikiriwi kwamba itafuatwa, kwani kwa kufanya hivyo Ireland itapoteza faida nyingi.


Mawaziri wengi wa mambo ya kigeni waliokutana jana waliegemea katika ule msemo wa Waswahili: Funika kombe mwanaharamu apite. Wameamuwa kusonga mbele na zoezi la nchi nyingine kutoa kibali kwa mkataba huo, na baadae kuangalia mambo yatakavyokuwa. Lakini faida gani ya kuukubali mkataba ambao baadae hautatekelezwa, ubakia kwenye mashubaka tu? Bunge la Jamhuri ya Cheki, nchi ambayo bado haijaamuwa juu ya mkataba huo, litauliza.


Pindi mkataba huu wa Lisbon hautafanya kazi, kuna hatari Umoja wa Ulaya utasambaratika na ndani yake kuwa na makundi ya nchi ambapo kila kundi litatafautiana na kundi lengine katika kasi na uthabiti wa kuiunganisha Ulaya. Tangu hapo hali hiyo inaonekana sasa kwani kuna kundi la nchi ndani ya Jumuiya lenye sarafu ya pamoja ya Euro, kuna kundi la nchi zilizoondosha udhibti wa mipaka baina yao, yaani lile kundi la Schengen, na kuna lile kundi la nchi zenye kushirikiana katika nyanja mbali mbali za mahakama, siasa za ndani na za kutoza kodi. Hivi sasa Uengereza, Denmark na Ireland zimejipatia kinga fulani kutokana na mwenendo unaofuatwa na nchi nyingi za Umoja wa Ulaya.


Lakini Ulaya inayokwenda kwa kasi za aina mbili haitoikuwa na maslahi kwa nchi mpya zanachama, kama vile Bulgaria na Romania, ambazo zimepiga hatua kubwa kuzifikia nchi za zamani. Kansela Angela Merkel wa Ujerumani anaikataa fikra ya kuwa na Ulaya ilio na kasi mbali mbali au kuwa na Ulaya ya kindakindaki.


Na mazungumzo yamechipuka kama Ulaya bila ya Mkataba wa Lisbon inaweza kweli kuchukuwa wanachama wepya kutoka eneo la Balkan. Ujerumani inasema HAPANA, Poland, Jamhuri ya Cheki na Austria zinasema NDIO. Kwa vyovyote, itachukuwa muda kwa nchi hizo kuingizwa, kwani mkataba wa Lisbon hautaweza kuanza kufanya kazi Januri 2009, kama ilivopangwa.


Na cha ajabu zaidi ni kwamba chaguzi za Bunge la Ulaya zitafanyika Juni mwaka 2009 bila ya wapiga kura kujuwa safari ya Ulaya inaelekea wapi.