1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yaitetea nafasi yake katika siasa za Mashariki ya kati

Jane Nyingi
20 Januari 2017

Iran inayatazama mazumgumzo ya amani nchini Syria wiki ijayo kama nafasi ya kujenga mshikamano wake wa kikanda wakati pia Urusi na Uturuki zikidai kuwa na ushawishi mkubwa nchini Syria. 

https://p.dw.com/p/2W8Kd
USA PK Hassan Rohani
Picha: picture-alliance/AP Photo/B. Matthews

Ushindi wa majeshi ya Syria mwezi uliopita baada ya kuuteka mji wa mashariki mwa Aleppo ambao ulikuwa ngome ya waasi umeitumbuza  Iran katikati mwa mvutano wa kidiplomasia unaoendelea kuhusu mustakabali wa baadaye wa taifa hilo. Ushindi huo ulitokana na msaada muhimu kutoka kwa  washauri wa jeshi la Iran na maelfu ya wapiganaji wa kujitolea. Rais Hassan Rouhani alisema wiki hii kuwa waandaaji wa mazungumzo hayo ya amani yatakayoanza mjini Astana, Jumatatu wiki ijayo, ambao ni Iran, Urusi na Uturuki, ndio mataifa pekee yenye ushawishi wa kusitisha uhasama kati ya serikali ya Syria na waasi ili kupatikana  amani ya kudumu.Lakini  kuyashughulia maslahi  ya kila mdhamini wa mazungumzo hayo ndicho kuzungumkuti.

Syrien Situation in Aleppo
Rais wa Syria wakitoroka mashambulizi AleppoPicha: Getty Images/AFP/B. Al-Halabi

Iran, mshirika mkubwa wa Rais Bashar al-Assad, inataka kupewa kipaumbele hakikisho la kusalia madarakani kwa Assad au angalau mpangilio kwa kuaminika wa serikali ya mpito, kuhakikisha Syria haitumbukii katika  mikono ya watu wenye misimamo mikali, au serikali inayounga mkono wapinzani wa Rais Assad, yaani mataifa ya Saudi Arabia na Marekani.  Iran pia inataka kudumisha njia salama kwenda Lebanon kupitia Iraq na Syria, ambapo washirika wake wa Hizbullah wamekuwa wakizozana kwa muda mrefu na Israel. "Vita vya Syria havionekani kuwa vya wenyewe kwa wenyewe nchini Iran, badala yake vinachukuliwa  kuwa vita vya kuamua siasa za Mashariki ya Kati," anasema Adhan Tabatabai - mchambuzi  kutoka Iran na mkurugenzi mtendaji na shirika la CARPO lenye makao yake nchini Ujerumani. 

Serikali ya Tehran inaamini kuwa Israel ingelifanya mashambulizi ya angani dhidi ya vinu vya nyuklia  vya Iran iwapo Hizbullah haingekuwepo kama kuzuizi katika mpaka wa Israel na Lebanon, anasema Tabatabai. 
Mazungumzo kati ya Iran na Uturuki, ambayo inayaunga mkono makundi ya waasi nchini Syria, daima yatasalia kuwa mwiba. Kinachoshangaza zaidi ni mipasuko iliyoanza kujitokeza katika mahusiano kati ya Iran na Urusi, ambayo imekuwa msadizi mkubwa wa Rais Assad. Iran ina wasiwasi kuwa Urusi inaonekana  kuegemea upande wa Uturuki kwa kushirikiana na vikosi vya Uturuki  kukabiliana na kundi lijiitalo Dola la Kiislamu (IS) na pia kuitenga Iran katika mazungumzo ya awali ya kusitisha mapigano kaskazini mwa Syria.

Irak Kampf um Mossul
Kikosi maalum cha kukabiliana na Ugaidi Iran nchini SyriaPicha: Getty Images/AFP/D. Dilkoff

Hata hivyo, Iran inaweza kujivunia kuhusu mafanikio kadhaa katika eneo la Mashariki ya Kati katika miezi  ya hivi karibuni, kuanzia vita vya Syria hadi kuchaguliwa mgombea wa urais iliyekuwa ikimuunga mkono nchini Lebanon.
Kujumuishwa katika meza ya mazungumzo ya amani kuhusu Syria ni hatua muhimu kwa Iran, ambayo ilikuwa imezuiwa katika mazungumzo ya awali yaliyosimamiwa na Umoja wa Mataifa. Makubaliano juu ya mpango wa nyuklia iliyoyatia saini 2015 na mataifa yenye nguvu duniani yaliirejesha kuwa imara na kuisaidia kupata nafasi katika mkutano wa kimataifa kuhusu Syria mjini Vienna mwezi Oktoba mwaka huo wa 2014.

Wakati huo ilikuwa vigumu  kupuuza jukumu muhimu  la Iran katika mapigano ya Syria. Iran hutoa maelezo machache kuhusu ushiriki wake nchini Syria, lakini mwezi Novemba ilifichua kuwa zaidi ya wapigaji 1,000 wa kujitolea walikuwa wameuawa nchini Syria, wengi wao wakiwa ni wale waliosajiliwa kutoka jamii za Kishia  nchini Afghanistan na Pakistan.

 

Mwandishi: Jane Nyingi/AFPE
Mhariri: Mohammed Khelef