1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

150210 Iran Menschenrechtsrat

Josephat Nyiro Charo15 Februari 2010

Malumbano yatarajiwa wakati wa maswali namajibu

https://p.dw.com/p/M1HF
Maandamano ya upinzani IranPicha: DW

Iran leo inalazimika kukabiliana na mtihani wa baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa huko mjini Geneva, Uswisi, ambapo itawasilisha ripoti yake kuhusu hali ya haki za binadamu na kujibu maswali. Kunatarajiwa kuwepo malumbano makali kati ya Iran na nchi za magharibi wakati Iran katika mkutano huo.

Kila baada ya miaka minne nchi zote 192 za Umoja wa Mataifa zinalazimika kuwasilisha taarifa mbele ya baraza la haki za binadamu na kujibu maswali kuhusu ukiukaji wa haki za binadamu. Mwishoni mapendekezo hutolewa ambayo nchi iliyofanyiwa uchunguzi inaweza kuyafanyia kazi au kuyakataa na baada ya miaka mingine minne kufanyiwa tena uchunguzi kubaini iwapo hali ya haki za binadamu imeboreka. Leo ni zamu ya Iran, na kwa muda wa saa tatu mjumbe wa nchi hiyo atalazimika kuhutubia na kujibu maswali. Balozi wa Ujerumani katika baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa, Reinhard Schweppe anataka leo kuzungumzia mambo yafuatayo.

"Kwanza ni jinsi Iran inavyowashungulikia wanasiasa wa upinzani na jumuiya ya kiraia. Lakini pia vitendo vya kikatili vinavyofanywa na vyombo vya usalama dhidi ya waandamanaji, ukamataji wa watu kiholela na kuwanyonga. Na ukiukaji wa haki za binadamu nchini Iran, ambao ndio kitu kibaya zaidi, unawaathiri watu wa tabaka zote."

Kabla kufanyika kikao cha leo cha baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa mjini Geneva nchi kadhaa zimeandaa orodha ya maswali kuiuliza Iran. Jamhuri ya Cheki na Danemark zinataka kujua kwa nini Iran imevunja sheria ya Umoja wa Mataifa inayopiga marufuku matumizi ya nguvu na mateso.

Sweden kwa upande wake inataka kufahamu ikiwa Iran imechunguza visa vya mateso baada ya uchaguzi wa rais wa mwezi Juni mwaka jana uliozusha utata. Hukumu ya kifo, hususan dhidi ya watoto chini ya umri wa miaka 18 inatarajiwa kukosolewa vikali katika kikao cha leo, pamoja na hukumu kama vile kuwapiga watu mawe, kuwakata viungo na kuwachapa viboko.

Msingi wa mjadala wa leo katika baraza la haki za binadamu ni ripoti tatu: moja iliyoandaliwa na serikali ya Iran yenyewe na nyengine mbili zimeandaliwa na kamishna mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na haki za binadamu ambazo zinajumulisha maoni ya vyombo huru vya habari na asasi zisizo za kiserikali.

La kusisimua katika mkutano wa leo litakuwa jukumu la Marekani ambayo kuanzia mwaka jana ni mwanachama wa baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa. Mjumbe wa wizara ya mashauri ya kigeni wa Marekani anayehusika na haki za binadamu nchini Iran, John Lambert, ameeleza wazi kabla kikao cha leo kwamba mjadala kuhusu hali ya haki za bidanamu nchini Iran ni vigumu kuutenganisha na mpango wake wa nyuklia. Lengo la baraza la haki za binadamu sio kuihujumu serikali ya Iran, lakini bwana Lambert ana tashuishi ikiwa baraza hilo litafaulu katekeleza wajibu wake.

"Wasiwasi wetu ni kazi hii ya baraza la haki za binadamu na uchunguzi wake iwe ya kuaminika na ifanyike kwa uadilifu ili itoe picha ya matarajio ya Wairan na hali yao inayowakabili hivi sasa."

Ripoti iliyoandaliwa na Iran inalieleza taifa hilo kuwa la kidemokrasia na linaloheshimu haki za binadamu hususan haki za wanawake na haki za uhuru wa kidini kwa watu walio wachache nchini humo. Iran inasema idadi ya watu wasiojua kusoma na kuandika imeshuka kwa asilimia 15 ikilinganishwa na zaidi ya nusu ya wananchi wote wa Iran ambao hawakujua kusoma na kuandika baada ya mapinduzi ya kiislamu.

Wachambuzi wa mambo wanaamini katika mtihani wa leo Iran itaungwa mkono na nchi wanachama wa jumuiya ya nchi za kiislamu, OIC, na nchi zinazoendelea kiuchumi. Nchi za magharibi zitataka kuendeleza ukosoaji wake dhidi ya utawala wa Tehran.

Mwandishi:Charo,Josephat-ZPR-LECHLER

Mhariri:Abdul-Rahman,Mohammed