Iran yatishia kuongeza urutubishaji Urani | Media Center | DW | 19.05.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Suala la Nuklia la Iran bado ni mgogoro

Iran yatishia kuongeza urutubishaji Urani

Kitisho cha Iran kinafuatia hatua ya kuwekewa vikwazo na Marekani,wakati ambapo msimamo wa Umoja wa Ulaya ukiwa sio wazi kwa Iran.Iran yasema ikiwa EU haitoendeleza makubaliano ya 2015 itachukua hatua.

Mkuu wa shirika la Atomiki nchini Iran amesema nchi hiyo huenda ikaanza tena kurutubisha madini ya urani ikiwa nchi za Umoja wa Ulaya zilizotia saini makubaliano ya Nyuklia ya mwaka 2015 zitashindwa kuyaendeleza kufuatia hatua ya Marekani ya kujiondoa katika mkataba huo. Ali Akbra Salehi amewaambia waandishi habari leo Jumamosi 19.05.2018 kwamba ikiwa Umoja wa Ulaya utaendelea kuunga mkono makubaliano ya Nyuklia Iran pia itazingatia ahadi zake ingawa kwa sasa sera kuu ya Iran ni kusubiri na kutazama kitakachotokea.

Ameonegeza kusema kwamba kuna hatua nyingi zinazoweza kufuatwa na Iran ikiwemo kuanza kurutubisha Urani kwa kiwango cha asilimia 20. Salehi pia amebaini kwamba Umoja wa Ulaya umeahidi kuyaokoa makubaliano hayo yaliyofikiwa kati ya nchi hiyo na nchi zenye nguvu duniani licha ya Uamuzi wa rais wa Marekani Donald Trump kuiondoa nchi yake katika makuabaliano hayo na kuvirudisha vikwazo dhidi ya serikali ya mjini Tehran.

Katika mkutano na waandishi wa habari uliofanywa kwa pamoja na Ali Akbar Salehi na Kamishna wa Umoja wa Ulaya wa masuala ya nishati na Mazingira Miguel Arias Canete, mkuu huyo wa shirika la Atomiki la Iran amesema wanataraji kwamba juhudi zao zitafanikiwa na kwamba vittendo vya Marekani vimeonesha kwamba sio nchi inayoweza kuaminika katika mikataba ya kimataifa.

Kamishna wa Umoja wa UIaya Miguel Arias Canete aliwasili Tehran leo(Jumamosi) kuwasilisha mipango ya kuendeleza  biashara ya mafuta na gesi  sambamba na hatua za kulindwa makampuni ya Ulaya licha ya vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran.

Kwa mtazamo wa Canete kuyalinda makubaliano ya 2015 ya Nyuklia ni hatua muhimu ya msingi kwa ajili ya amani katika kanda hiyo. Canete ni afisa wa kwanza wa ngazi ya juu kutoka nchi za Magharibi kenda Iran tangu Marekani ilipotowa uamuzi wake,na anatarajiwa kuwa na mkutano na waziri wa Iran wa mazingira Isa Kantari na waziri wa mafuta Bijan Namdar Zanganeh baadae na  hapo kesho Jumapili amepangiwa kukutana waziri wa mambo ya nje Javad Zarif.

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wameahidi kuyaendeleza makubaliano hayo ya Nyuklia na kuanzisha hatua za kuhimiza biashara na kulindwa kwa makampuni ya Umoja wa Ulaya kutokana na vikwazo vya Marekani.

Hata hivyo tayari makampuni mengi ya Umoja wa Ulaya ikiwemo Total ya Ufaransa na Maersk ya Uholanzi zimeshasema kwamba itakuwa vigumu kuendela kubakia nchini Iran pindi vikwazo vya Marekani vitaanza kutekelezwa kikamilifu katika kipindi cha miezi sita ijayo isipokuwa ikiwa makampuni hayo yatapewa uthibitisho na Marekani kwamba hayatoguswa katika vikwazo hivyo.

Biashara kati ya Iran na Umoja wa Ulaya inathamani ya kiasi yuro bilioni 20 ikiwa ni kwa nchi zote mbili ikihusisha uingizaji  na usafirishaji wa bidhaa.

Nchi nyingi za Umoja wa Ulaya hununua bidhaa  kutoka Iran ikiwa ni asilimia 90, nchi hizo zikiwa ni Uhipania, Ufaransa, Italia, Ugiriki, Uholanzi na Ujerumani. Urusi na China pia zimeahidi kuendelea kufanya biashara na Iran na kwasababu nchi hizo hazina ushirikiano na masoko ya Marekani hazipo sana katika hatari kushinikizwa kibiashara na  Marekani.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri:Caro Robi