1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yashutumu mataifa ya magharibi kwa ghasia.

Sekione Kitojo30 Desemba 2009

Mwakilishi wa kiongozi mkuu wa kidini nchini Iran Ayatollah Ali Khamenei amesema jana kuwa viongozi wa upinzani ni maadui wa Mwenyezi Mungu na wanapaswa kuadhibiwa kwa mujibu wa Sharia.

https://p.dw.com/p/LGyB
Rais wa Iran Mahmoud Ahmadinejad (kati) akipiga kura katika uchaguzi uliobishaniwa nchini humo na kuzua maandamano ambayo yanaendelea hadi leo.Picha: picture-alliance/ dpa

Mwakilishi wa kiongozi mkuu wa kidini nchini Iran Ayatollah Ali Khamenei amesema jana kuwa viongozi wa upinzani ni maadui wa Mwenyezi Mungu, ambao wanastahili kuuwawa kwa mujibu wa sheria ya dini ya Kiislamu ya Sharia. Taarifa hiyo iliyotolewa na kiongozi wa kidini Abbas Vaez-Tabasi imeingiliana na maandamano ya mamia kwa maelfu ya waungaji mkono Serikali ambao walikuwa wakitoa wito kwa viongozi wa upinzani kuadhibiwa kwa kuchochea ghasia baada ya uchaguzi wa rais mwezi Juni.

Matamshi ya Vaez-Tabasi yamekuja siku mbili baada ya watu wanane kuuwawa katika maandamano ya kuipinga serikali yaliyotokana na uchaguzi uliobishaniwa wa Juni mwaka huu ambapo rais aliyeko madarakani mwenye msimamo mkali Mahmoud Ahmedinejad alishinda.

Vurugu za kisiasa zimeingia katika awamu mpya nchini Iran kukiwa na mapambano yaliyomwaga damu pamoja na kukamatwa kwa wapinzani , huku majeshi ya usalama yakitoa wito kwa maafisa kuchukua hatua kali dhidi ya viongozi wa upinzani.

Kiasi watu maarufu 20 kutoka upande wa upinzani wamekamatwa tangu siku ya Jumapili, ikiwa ni pamoja na washauri waandamizi wa kiongozi wa upinzani Mir Hossein Moussavi, shemeji yake pamoja na dada yake mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel Shirin Ebadi, imeeleza tovuti ya upinzani.

Ebadi amesema katika radio ya Ufaransa kuwa viongozi wa Iran wanajaribu kumnyamazisha kwa kumkamata dada yake.

Baada ya rais wa Marekani Barack Obama kushutumu siku ya Jumatatu ukatili wa viongozi wa Iran dhidi ya waandamanaji, rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy jana Jumanne ameshutumu ukandamizaji wa kumwaga damu dhidi ya waandamanaji nchini Iran.

Sarkozy amesema katika taarifa kuwa Ufaransa inatoa wito wa kusitishwa kwa ghasia, kuachiliwa huru kwa wanaharakati wa upinzani waliokamatwa na kuheshimiwa kwa haki za binadamu.

Sarkozy 35 Milliarden Plans
Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy ameitaka serikali ya Iran kusitisha matumizi ya nguvu dhidi ya waandamanaji.Picha: AP

Nae naibu waziri wa mambo ya kigeni nchini Ujerumani Werner Hoyer amesema kuwa serikali ya Ujerumani inawasi wasi mkubwa kuhusiana na matukio ya hivi karibuni nchini Iran na kushutumu tabia ya jeshi la usalama nchini humo.

Serikali ya Ujerumani inashutumu vikali matumizi ya nguvu dhidi ya waandamanaji na kutoa wito kwa viongozi wa Iran kufanya kila linalowezekana kusitisha hali hiyo. Kile kinachotokea mjini Tehran kinaathari kwa eneo lote. Na Iran ina uwezo wa kuboresha ama kuporomosha hali ya usalama katika eneo hilo. Kwa hiyo ni wajibu wa viongozi wa serikali ya Iran kuchukua jukumu la uongozi na hili litawezekana tu iwapo taasisi za kidemokrasia na kisheria zitafanyakazi.

Wakati huo huo rais Ahmedinejad wa Iran amezishutumu Marekani na Israel jana kwa kuchochea maandamano dhidi ya serikali, akisema kuwa ni mchezo unaokera na kutia kichefuchefu. Amesema kuwa huu ni mchezo wa kuigiza, uliodhinishwa na kupata watazamaji uliotayarishwa na nchi mbili hasimu.

Wairan wamekwisha ona michezo mingi ya aina hii, amesema rais huyo akinukuliwa na shirika la habari la Iran IRNA.

Jeshi la nchi hiyo limevishutumu vyombo vya habari vya mataifa ya kigeni kwa kujiunga pamoja na upinzani kuliletea madhara taifa hilo la Kiislamu. Balozi wa Uingereza mjini Tehran aliitwa na serikali ya Iran na kushutumiwa kuwa anaingilia mambo ya ndani ya nchi hiyo. Iwapo Uingereza haitaacha kuzungumza upuuzi itaadhibiwa kwa kupigwa kofi , amesema waziri wa mambo ya kigeni wa Iran Manouchehr Mottaki. Uingereza imesema kuwa balozi wake amejibu shutuma zote kwa ukali.

Mwandishi : Sekione Kitojo / RTRE / AFPE

Mhariri : Mwadzaya thelma