1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yasema iko tayari kusafirisha madini ya Uranium nje

3 Februari 2010

Msimamo mpya wa Iran unazitia wasiwasi nchi za magharibi,je ni msimamo wa dhati au porojo za kawaida za nchi hiyo zilizozoeleka?

https://p.dw.com/p/LqJC
Rais wa Iran Mahmoud AhmedinejadPicha: AP
Iran imesema iko tayari kusafirisha madini yake ya Uranium nchi za nje kwa ajili ya kurutubishwa.Tamko hilo limetolewa na rais wa nchi hiyo Mahmoud Ahmedinejad wakati ambapo nchi za magharibi hii leo zimekutana kwa lengo la kujadili jinsi gani ya kuiwekea vikwazo vigumu zaidi nchi hiyo kufuatia hatua yake ya kuendelea na mipango yake ya kinuklia. Rais wa Iran Mahmoud Ahmedinejad alitangaza msimamo huo mpya hapo jana usiku hali ambayo imeonekana kama ni kulegeza kamba kuelekea nchi za Magharibi.Tamko la rais wa Iran linatofautiana sana na misimamo ya hapo awali iliyotolewa pia na viongozi wengine wa juu wa jamhuri hiyo ya kiislamu. Akihojiwa katika kituo cha taifa cha televiesheni jana usiku rais Ahmedinejad bila shaka yoyote alionekana moja kwa moja kuunga mkono mapendekezo ya Umoja wa Mataifa akisema- ''Sina tatizo na suala la kusafirisha madini ya Uranium kwa ajili ya kurutubishwa katika nchi za nje.Nataka ushirikiana wa dhati''
Raketentest im Iran
Iran inatuhumiwa kutumia viwanda vyake vya kinuklia na vyombo vya anga kutengeneza silaha za atomikiPicha: AP
Hata hivyo katika matamshi yake hakusema wako tayari kusafirisha kiasi gani cha madini hayo kwa ajili ya kurutubishwa hasa ikizingatiwa kwamba hilo ndilo suala muhimu kutokana na mapendekezo ya Umoja wa Mataifa ya kutaka nchi hiyo isafirishe asilimia 70 ya madini hayo . Halikadhalika haijafahamika kama matamshi hayo ya rais ndio msimamo jumla wa serikali au ni maoni yake ambayo sio mara ya mwanzo kuyatoa. Nchi zenye nguvu zikiongozwa na Marekani zinaitaka Iran ikubaliane na mpango wa Umoja wa mataifa na kusafirisha madini yake ya Uranium katika nchi za Urussi na Ufaransa ili yarutubishwe na kuondoa wasiwasi kwamba nchi hiyo inalengo la kutengeneza bomu la Nuklia.
Sicherheitsrat
Baraza la Usalama linaitaka Iran isafirishe asilimia 70 ya madini yake ya Uranium yarutubishwe nje ya taifa hilo.Picha: AP
Nchi hizo za magharibi leo zinakutana kujadiliana kuhusu kuiwekea vikwazo vikali zaidi nchi hiyo ya Iran kutokana na ukaidi wake kuelekea mpango wake wa Kinuklia. Rais wa Marekani Barack Obama akizungumzia juu ya suala hilo ameionya Iran kwamba muda unayoyoma na inabidi ionyeshe kwa vitendo msimamo wake vinginevyo itakabiliwa na hatua kali.Obama amesema- ''Iran inavunja sheria zinazotakiwa kufuatwa na kila nchi.hali hiyo inatishia usalama wa eneo zima pamoja na ulimwengu kwa jumla'' Iran ambayo ilikubali kimsingi kuzingatia mapendekezo ya Umoja wa Mataifa wakati wa mkutano wa mwezi Oktoba baadae ilionekana kuukataa mpango huo na kusema kwamba inapendelea zaidi madini hayo yarutubishwe katika ardhi yake. Iran ilitoa muda wa hadi mwishoni mwa Januari kwa nchi hizo zenye nguvu kujibu mapendekezo yake.Lakini sasa mambo yanaonekana kuelekea mkondo tofauti baada ya rais Ahmedinejad kutamka kinyume na msimamo wa awali. China ambayo mwanachama wa kudumu katika baraza la usalama la Umoja wa mataifa na mshirika wa Iranc jana imesema bado kuna nafasi ya kuzungumza na Iran kuutatua mzozo huo wa kinuklia,lakini kwa upande mwingine Marekani imesema inatumai kuishawishi China na nchi zingine nne zenye nguvu siku kadhaa zijazo kuhusu suala hilo la Iran na haja ya nchi hiyo kuwekewa vikwazo. Wakati huohuo Iran imefanikiwa kufyetua salama satellaiti yake aina ya Kavoshgar 3 iliyotengezwa nchini humo.Roketi hiyo iliyokuwa imebeba chombo maalum cha majaribio inauwezo pia wa kurudisha data muhimu ardhini kutoka angani. Mwandishi Saumu Mwasimba/AFPE Mhariri Mohammed AbdulRahman